Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku 100 za utawala wa Ruto: Mambo 8 ambayo rais William Ruto ameyafanya kinyume na matarajio ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili
Siku 100 baaada ya Rais wa Kenya William Ruto kuchukua hatamu ya uongozi amekuwa mbioni kufanya kazi ya kurekebisha kile ambacho alidai mtangulizi wake Uhuru Kenyatta alikosea wakati akiwa madarakani.
Na ili kudhihirisha kwamba uhasama uliokuwepo kati yake na mtangulizi wake haukuwa jambo la mzaha, kiongozi huyo alipangua baadhi ya maagizo yaliofanywa na mtangulizi wake.
Miongoni mwao ni suala la usajili wa majaji sita wa mahakama kuu ambao rais Uhuru Kenyatta alikataa kuwateua akidai walikuwa hawana maadili.
Pamoja na suala hilo haya hapa maagizo nane ya Uhuru Kenyatta yaliobadilishwa na mrithi wake Rais William Ruto.
1. Kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na unga
Awali Rais Ruto aliahidi kurekebisha uchumi kwa kupunguza deni la serikali, kupunguza bei ya bidhaa muhimu, na kuunda "hustler fund" kutoa mikopo ya kibinafsi kwa Mkenya yeyote aliye na simu ya rununu na akaunti ya pesa ya rununu.
Lakini kitendo chake cha kwanza baada ya kushika wadhifa huo ilikuwa kupunguza ruzuku ya chakula na mafuta iliyoletwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.
Hatua hiyo ilipokelewa kwa hisia tofauti nchini Kenya kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha kote duniani.
Licha ya kwamba ruzuku hizo zilelanga kuwapeusha wakenya wa kipato cha chini dhidi ya makali ya kupanda kwa bei za bidhaa ulimwenguni , Rais William Ruto alitofautiana.
Rais Ruto alisema kwamba ruzuku ya mafuta pamoja na ile ya chakula haijawasaidia Wakenya , akiongezea kwamba ruzuku ya mafuta pekee imemgharimu mlipa kodi ksh. 144b, huku ksh.7b zikitumika katika kipindi cha miezi minne iliopita kabla ya serikali yake kuchukua madaraka.
Ruto aidha alisema ruzuku hizo "hazikuzaa matunda yoyote", akiongeza kuwa kuondolewa kufuatia ombi kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, mkopeshaji mkuu wa shirika lenye nguvu la kiuchumi la Afrika Mashariki.
Ruzuku hizo ziliwekwa na rais Uhuru Kenyatta wakati wa utawala wake huku kukabiliana na bei za juu za mafuta na unga wa mahindi huku akitafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo hilo.
Hatahivyo ,Ruto alisema kwamba mbali na kuwa ghali , ruzuku hiyo ilikuwa ikitumiwa vibaya , imefnya uharibifu wa soko na imekuwa ikitumika kutengeneza uhaba bandia wa bidhaa hiyo.
2.Kuondoa marufuku ya vyakula vya GMO
Mnamo mwezi Oktoba mwaka huu serikali ya Kenya iliondoa marufuku ya miaka 10 dhidi ya mazao yaliyotokana na mbegu kisaki za GMO ili kukabiliana na uhaba wa chakula.
Hatua hiyo hata hivyo imekosolewa vikali na baadhi ya wakulima na makundi ya wanaharakati, ambao wanatilia shaka usalama wa mazao hayo.
Kuondolewa kwa marufuku hiyo kunamaanisha kuwa wakulima wa Kenya sasa wanaweza kulima kwa uwazi mazao ya GM, pamoja na kuagiza chakula kutoka nje ya nchi na vyakula vya mifugo vinavyozalishwa kupitia kwa njia ya GMO, kama vile mahindi meupe ya GMO.
Mahindi ni chakula kikuu nchini Kenya, na hulimwa katika asilimia 90 ya mashamba yote ya Kenya. Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya, na kinatoa asilimia 80 ya ajira kwa wakazi wa mashambani.
Wakulima wa Kenya wanategemea mazao yao sio tu kwa mapato bali kama chanzo cha chakula kwa familia zao.
3. Kuuangazia upya mfumo wa elimu wa CBC
Serikali ilipoamua kubadilisha mtaala wa 8-4-4 na kuweka mtaala unaozingatia Umahiri (CBC), habari hizo zilipokelewa kwa mitazamo tofauti.
Wadau wakuu, kama vile Tume ya Utumishi wa Walimu, Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Vyuo vya Ualimu, Wakuu wa Shule na walimu walishiriki kwa kiasi kikubwa katika uzinduzi, uanzishaji na utekelezaji endelevu wa CBC.
Wote waliruhusiwa kueleza wasiwasi wao na kushiriki michango katika kufanikisha mtaala.
Ni kutokana na manung'uniko hayo ambayo yalimshinikiza Rais William Ruto kuanzisha jopo ambalo litsaidia katika kuwauliza Wakenya iwapo mfumo huo wanadhania unapaswa kuendelea kuhudumu na maeneo yapi yalipaswa kurekebishwa .
Rais pia aliahidi kutatua suala la mpito la wanafunzi wa darasa la nane chini ya mfumo wa 8-4-4 na Gredi ya sita chini ya mfumo wa CBC hadi katika shule ya upili mwezi Januari.
KIongozi huyo amsema kwamba kuna mazungumzo ya kiwango cha juu yanayoendelea nchini hususan katika kuidhinisha CBC.
4. Kupakua na kuondoa mizigo bandarini Mombasa
Kufuatia hatua ya serikali iliopita kutangaza kwamba ilikuwa inafungua bandari ndogo ya nchi kavu katika eneo la Naivasha na kwamba baadhi ya huduma za badanri ya Mombasa zingeathiriwa kulikuwa na hisia kali mjini humo huku baadhi ya wafanyabiashara wakiamua kufanya maandamano.
Hatahivyo utawala ulioondoka haukuridi nyuma katika uamuzi wake huo , na kilichotokea ni kwamba raia wengi wa eneo la pwani walipoteza ajira zao huku wale wa Naivasha wakipata ajira hizo.
Hatahivyo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita rais William Ruto aliapa kurudisha huduma za bandari hiyo Mombasa, ili wakaazi wanedelea kufaidika nazo. Na muda mfupi tu baada ya kuapishwa Rais Ruto alitoa agizo la mara moja la kurudishwa kwa huduma hizo kinyue na mtangulizi wake rais Uhuru Kenyatta.
Huduma hizo ni pamoja na upakuzi wa shehena kutoka bandarini humo ambalo litaruhusu kuondolewa kwa bidhaa zote na masuala mengine ya kiutendaji kurejea katika bandari ya Mombasa, hivyo basi kubatilisha agizo la awali la aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta. Hii, alisema, itarejesha maelfu ya kazi katika jiji la Mombasa.
5. Komesha Kufungiwa kwa wenye mikopo CRB
Zaidi ya watu milioni nne waliokosa mikopo wataondolewa kwenye orodha zisizoruhusiwa za Credit Reference Bureau (CRB) chini ya mipango iliyopendekezwa na Rais William Ruto ya kurekebisha soko la mikopo nchini.
Rais aliagiza Benki Kuu ya Kenya (CBK) kukomesha kuorodhesha wakopaji na badala yake iwe na mbinu ya kupata alama ambapo wanaokiuka watapata alama za chini badala ya kufungiwa nje ya mfumo wa kifedha.
Rais Ruto alisema serikali inaunga mkono utaratibu wa kutoa mikopo lakini inataka mfumo ambapo wakopaji wanaweza kufuzu kutoka mkopaji wa kiwango cha chini hadi bora zaidi, ambapo wataruhusu kukopa kulingana na hatari.
Rais alisema utawala wake utahamisha mfumo wa Bodi ya Mikopo (CRB) kutoka kwa utaratibu wake wa sasa wa kuwaorodhesha wakopaji kiholela kwa lengo la kuwanyima mikopo.
6. Majaji sita waliokataliwa, ufadhili wa Mahakama
Katika hatua ambayo iliwashangaza wakenya wengi wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi huyo alikataa katakata kuwaapisha majaji sita ambao walikuwa wameteuliwa na tume ya huduma za mahakama ili kuhudumu kama majaji.
Taarifa kutoka Ikulu ilisema kuwa Rais alikataa uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Juu Joel Ngugi, George Odunga, Aggrey Muchelule na Weldon Korir kwa mahakama ya Rufaa "kwa kukosa kuafikia kiwango kinachohitajika".
Wengine ambão pia walikosa kuorodheshwa ni Msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange na Hakimu Mkuu Evans Makori, ambaye alikuwa ameteuliwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
Lakini katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita rais Ruto aliahidi kubadili uamuzi huo na kuamua kuwaapisha punde atakapochukua madaraka.
Na ili kudhihirisha zaidi kujitolea kwake kwa uhuru wa Idara ya Mahakama, Rais Ruto aliwateua majaji hao sita na kuwaapisha mara moja
Zaidi ya hayo, alisema utawala wake utaongeza mgao wa bajeti kwa Idara ya Mahakama hadi bilioni 3 kila mwaka kwa miaka mitano ijayo.
Rasilimali hizi, alisema, zitasaidia kuongeza kiwango cha chini cha haki kwa kuongeza idadi ya mahakama ndogo kutoka 25 za sasa hadi 100.
7. Kuondolewa Wizara ya Ugatuzi
Wakati huohuo Rais William Ruto aliiondoa wizara moja - wizara ya ugatuzi - ambayo ilikuwa katika baraza la mawaziri la mtangulizi wake, Rais Uhuru Kenyatta.
Kuondolewa kwa wizara ya ugatuzi kuliibua mijadala ya umma kuhusu iwapo Kenya itaafikia malengo ya ugatuzi ipasavyo, jinsi inavyotazamiwa katika katiba ya 2010.
Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alikashifu uamuzi huo akishangaa kwa nini Ruto hakuuona kama kipaumbele.
Hata hivyo baadhi ya raia walisema kwamba ilikuwa ni Wizara ambayo ilihusishwa na serikali ya kitaifa ikisisitiza kung'ang'ania baadhi ya majukumu ambayo yalipaswa kugatuliwa.
Raia hao walisema kwamba shughuli zote ambazo zimegatuliwa zinafaa kwenda kaunti kwa hivyo hakuna sababu ya kuwa na wizara kama hiyo.
8. Kuongezeka kwa Malipo ya NHIF
Rais William Ruto ameunga mkono msukumo wa kutaka matajiri walipe michango ya juu zaidi ya kila mwezi kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF), miezi kadhaa baada ya pendekezo sawia kutupiliwa mbali na Bunge.
Bw Ruto alisema kuwa michango ya NHIF itaegemezwa kwenye malipo ya kila mwezi ya wafanyikazi, katika azma ya kuongeza ufadhili wa mpango huo.
NHIF mapema mwaka huu ilipendekeza kwamba michango ya wafanyikazi wanaopata zaidi ya Sh100,000 inapaswa kuhesabiwa kuwa asilimia 1.7 ya malipo yao. Lakini hii ilikataliwa na Bunge lililopita , na kulazimisha bima hiyo kutafuta mbinu mbadala.
Hatua ya Dkt Ruto, ambaye sasa anaungwa mkono na wabunge wengi kuunga mkono pendekezo la NHIF, inajiri kama afueni kuu kwa bima ya kitaifa ambayo imekuwa ikitafuta mbinu za kuongeza ufadhili wake kutekeleza mpango wa afya kwa wote.
Rais Ruto alitangaza kuwa michango iliyotolewa na Wakenya kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) sasa itategemea mapato ya mtu binafsi.
Hii ni habari njema kwa watu wa kipato cha chini kwani ina maana sasa wanaweza kulipa kidogo.
Kwa sasa, wafanyakazi wanaopata zaidi ya Sh100,000 watalipa mchango uliopangwa wa kila mwezi wa Sh1,700 huku wafanyakazi wanaolipwa chini kabisa wakichangia Sh150.