Ni nchi zipi zinazozimiliki ndege muhimu ya kivita aina ya F-35?

Chanzo cha picha, F35
Rais wa Marekani Donald Trump, akizungumza na waandishi wa habari mjini Ankara kabla ya mkutano wake na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, alisema vikwazo dhidi ya Uturuki kupata silaha za ulinzi wa anga zitaondolewa.
Marekani iliweka vikwazo hivyo dhidi ya Uturuki mwezi Disemba mwaka wa 2020 baada ya Uturuki kuamua kununua mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kutoka Urusi.
Trump alisema watazingatia tena suala la Uturuki kupata ndege za kivita aina ya F-35.
Uturuki ilikuwa miongoni mwa washirika waanzilishi wa mradi wa ndege za F-35.
Hata hivyo, kutokana na sababu hiyo hiyo, Uturuki pia iliondolewa katika mpango wa ndege za kivita aina ya F-35.
Kutokana na hilo, iliibidi Uturuki kuachana na mfumo wa S-400 ili waweze kurejea katika mpango wa ndege za kivita za F-35.

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images
Sifa za kiufundi za F-35
F-35 ni ndege ya kivita ya kisasa yenye matumizi mbalimbali ya kizazi cha tano yenye teknolojia ya hali ya juu, ikiwa na mifumo inayotumia akili mnemba (AI) na uwezo wa kupata taarifa kwa wakati halisi.
Ndege hizi zinaweza kuruka kasi ya takriban kilomita 1,900 kwa saa, lakini hiyo siyo sifa yake kuu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
F-35 inaweza kugundua na kushambulia malengo kwa uwezo wake yenyewe, huku pia ikikusanya taarifa kupitia mifumo yake na kuzituma kwa ndege nyingine au mifumo mingine ya kivita.
Uwezo huu unachukuliwa kuwa hatua muhimu katika uendeshaji wa operesheni za kisasa za kivita angani. Uwepo wa F-35 katika operesheni husika huongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa ndege za zamani zinazoshiriki katika misheni hiyo.
Ikiwa imeundwa kwa teknolojia ya kuepuka kutambuliwa na ufuatiliaji wa rada, ndege hii inaelezwa kuwa mojawapo ya ndege za kivita zilizo na mifumo ya juu zaidi duniani.
Ndege hii huuzwa takriban dola million 80 za Marekani, n ani miongoni mwa ndege ghali sana za kivita duniani.
Jeshi la Anga la Marekani linasema kuwa toleo la F-35A lina uwezo wa kuhimili nguvu ya 9g .
Hii ina maana kwamba rubani anaweza kustahimili nguvu ya mivutano(gravity) inayofikia mara tisa ya nguvu ya kawaida ya uvutano wa dunia wakati wa kufanya mizunguko au miondoko ya kasi angani.
Kwa sasa, F-35 ndiyo mpango mkubwa na wenye gharama kubwa zaidi wa utengenezaji wa silaha za kivita duniani.
Mpango huo unatarajiwa kuendelea kwa takriban miaka 30 hadi 40.
Ila mpango huo pia umekumbwa na changamoto.
Ripoti ya majaribio ya Pentagon iliyowekwa wazi kwa umma mnamo mwezi Novemba 2024 inaelezea kuwepo kwa wasiwasi kuhusu ucheleweshaji wa kutengeneza ndege hizo, usahihi wa silaha zinazoundwa, na uwezo wa mfumo wa ulinzi dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni.
Nchi zipi zinamiliki ndege za F-35?
Kwa mujibu wa mpango wa F-35, zaidi ya ndege 550 za F-35 zinatarajiwa kuwa barani Ulaya ifikapo mwaka 2030.
Kando na Marekani, ndege za F-35 zinatumika au zimeagizwa na nchi nyingine 19.
Nchi zinazoshiriki katika mpango wa F-35 ni Marekani, Uingereza, Italia, Uholanzi, Kanada, Australia, Denmark na Norway.

Chanzo cha picha, F35
Nchi ambazo tayari zimepokea ndege za F-35 ni:
- Marekani
- Uingereza
- Italia
- Uholanzi
- Norway
- Australia
- Japan
- Korea Kusini
- Israel
- Denmark
- Ubelgiji
- Poland
Nchi ambazo zimesaini mikataba, ziko katika hatua za uzalishaji na zinatarajiwa kupokea ndege zao za kwanza katika miaka ijayo ni:
- Ujerumani
- Kanada
- Finland
- Uswisi
- Singapore
- Ugiriki
- Jamhuri ya Czech
- Romania
Kwa nini Uturuki iliondolewa kwenye mpango wa F-35?
Uturuki ilijiunga na mradi wa F-35A Lightning II, ndege ya kivita ya kizazi cha tano iliyotengenezwa na kampuni ya Lockheed Martin, moja ya wazalishaji wakubwa wa silaha duniani, chini ya Mpango wa Joint Strike Fighter (JSF) mwaka 2002.
Nchi zilizoshiriki katika mpango huo ni pamoja na Uturuki, Marekani, Uingereza, Italia, Uholanzi, Australia, Denmark, Canada na Norway.
Uturuki iliagiza ndege 100 za kivita aina ya F-35 ili kuimarisha jeshi lake la anga, huku pia ikishiriki katika utengenezaji wa baadhi ya vipuri vya ndege hizo.
Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, İsmet Yılmaz, alisema mwaka 2014 kuwa jumla ya dola bilioni 25 zingelipwa kwa ajili ya ununuzi wa ndege hizo.
Mwaka 2018, umiliki wa ndege nne za F-35 ulihamishiwa Uturuki. Hata hivyo, ndege hizo ziliendelea kubaki nchini Marekani kwa ajili ya programu za mafunzo, ambapo marubani wa Uturuki pia walishiriki.

Chanzo cha picha, Yasin AKGÜL / AFP
Baadaye, umiliki wa ndege nyingine mbili za F-35 pia ulihamishiwa Uturuki.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Bunge la Marekani walifanya juhudi za kuzuia uuzaji wa ndege za F-35 na vifaa vya kijeshi kwa Uturuki kwa ujumla.
Sababu zilizotolewa zilijumuisha kudorora kwa hali ya demokrasia nchini Uturuki, kuzuiliwa kwa baadhi ya raia wa Marekani, pamoja na ununuzi wa mfumo wa ulinzi wa anga wa S-400 kutoka Urusi.
Hatimaye, aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo, Donald Trump, alisaini sheria mnamo mwezi Agosti 2018 iliyositisha kwa muda utolewaji wa ndege za kivita aina ya F-35 kwa Uturuki.
Ndege hizo sita hazikuwahi kukabidhiwa Uturuki, na hatimaye nchi hiyo iliondolewa kwenye mpango wa F-35.
Ilibainika kuwa kufikia mwezi Desemba 2020, Marekani ilikuwa imepata watu wapya ambao wangewauzia vipuri vyote 1,005 ambavyo awali vilikuwa vinazalishwa na Uturuki chini ya mpango huo.
Baada ya Uturuki kuondolewa kwenye mpango wa F-35, ndege ambazo zilikuwa zimeagizwa na kumilikiwa na Uturuki zilibaki zikiwa zimehifadhiwa nchini Marekani na hazikuwahi kukabidhiwa Jeshi la Uturuki.
Uturuki ilikuwa imelipa Marekani dola bilioni 1.7 kwa ajili ya ununuzi wa ndege sita za kivita aina ya F-35A.















