Je, kubadilisha sheria kuhusu kujiua kutabadilisha mitazamo Kenya?

Chanzo cha picha, FAMILY HANDOUT
- Author, Makuochi Okafor
- Nafasi, BBC Africa -Afya
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Charity Muturi alikabiliana na mawazo ya kujiua tangu akiwa na umri wa miaka 14.
Katika miaka yake ya 30, Charity, kutoka Kenya, aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa bipolar. Lakini badala ya kuruhusu mawazo yake kumuondolea uhai, alikua mtetezi wa masuala ya afya ya akili.
Kwa kuelewa kwa kina athari ya aibu na kutengwa, Charity alifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha kwamba serikali inazingatia suala hili na kuwaweka mbele watu wanaohitaji msaada ili wapokee huduma, sio adhabu.
Wale waliomfahamu Charity wanasema alikuwa mkarimu na thabiti, kila wakati yuko tayari kutoa muda wake kusaidia wengine.
"Kama jina lake linavyosema, Charity, alikuwa amejaa upendo, mkarimu na mtoaji mwenye kujitolea," anasema nduguye, Tom Muturi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo Novemba 6 mwaka jana, Charity alijiua.
Lakini kampeni yake ya kubadilisha mtazamo kuhusu afya ya akili nchini Kenya iliendelea. Wanaharakati wa afya ya akili wanasema kazi ya Charity ilikuwa muhimu katika kusaidia kubadilisha sheria kuhusu kujiua nchini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mnamo Januari mwaka huu, Mahakama Kuu ya Kenya ilitangaza Kifungu cha 226 cha Kanuni ya Adhabu, ambacho kilikuwa kinahukumu jaribio la kujiua, kuwa hakifai kikatiba.
Kabla ya hapo, mtu yeyote ambaye alijaribu kujiua alikuwa akijumuishwa na kifungo cha hadi miaka miwili jela, faini, au vyote viwili. Watu waliokuwa na jaribio la kujiua walikamatwa na kufikishwa mahakamani badala ya kupokea msaada wa afya ya akili.
Uamuzi wa Januari, uliofanywa na Jaji Lawrence Mugambi, ulionesha kuwa sheria hiyo ilikuwa inawadhibiti watu wanaokabiliana na matatizo ya afya ya akili, na kuwakosesha haki yao ya huduma ya afya.
Mtaalamu wa saikolojia na mtetezi wa afya ya akili Amisa Rashid, ambaye alifanya kazi kwa karibu na Charity, aliupokea uamuzi huo kama ushindi kwa Wakenya na kumheshimu Charity kwa mchango wake katika kufanikisha hilo.
"Ilikuwa ni kipindi cha maumivu makubwa kwetu tuliomjua, huu utakuwa urithi wake," anasema.
Hata hivyo, Rashid anasema kuwa mapambano ya kuleta uelewa na kukubalika zaidi kuhusu masuala ya afya ya akili yanaendelea.
"Kuna mambo ambayo tunahitaji kubadilisha na hiyo inajumuisha mabadiliko ya kijamii, tabia na mtazamo kuhusu kujiua," anasema.
Kuharamisha inatosha?
Uharamishaji wa jaribio la kujiua una historia ngumu.
Wakati wa ukoloni, koloni nyingi za Kiafrika zilikuwa na sheria dhidi ya kujiua, na ingawa nchi nyingi zimefuta sheria hizi sasa, baadhi ya nchi zilizishikilia baada ya uhuru.
Nchini Ghana, ambapo kujiua kulifutwa kuwa kosa mwaka 2023, wataalamu wa afya ya akili wanaripoti dalili za mapema za kuboreka kwa mtazamo wa umma, ingawa imani kali za kitamaduni bado ni changamoto.
Dkt. Akwasi Osei, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya masuala ya Afya ya Akili ya Ghana, aliiambia BBC kwamba ingawa inaweza kuwa "mapema sana kuwa na ushahidi wa maandishi" wa mabadiliko kamili ya mitazamo kuhusu kujiua, kuna hisia wazi kuwa hatua hiyo imesababisha "mtazamo bora kuhusu kujiua na jaribio la kujiua" nchini humo.
Nchini Kenya, wataalamu wa afya ya akili wanatumaini kuwa uamuzi huo utahamasisha watu kutafuta msaada bila hofu ya kushtakiwa.
Hata hivyo, wengi wanaamini kwamba aibu inayosababishwa na hatua ya kujiua itaendelea kuwepo isipokuwa jitihada zaidi zifanyike kuwafundisha wananchi.
"Kufutia uhalifu ni hatua moja, lakini sasa tunahitaji kuingia katika mazungumzo wazi na ya ukweli kuhusu afya ya akili kwa ujumla," anasema Dkt. Chido Madzvamutse, daktari wa afya ya akili katika ofisi ya kanda ya Afrika ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Kubadilisha mitazamo ya kijamii kunahitaji elimu, uhamasishaji, na mifumo ya msaada yenye huruma," anasema.
Vikwazo vya Kitamaduni kuelekea mabadiliko

Chanzo cha picha, FAMILY HANDOUT
Katika jamii nyingi za Kiafrika, kujiua bado ni suala la aibu kubwa.
Imani za kidini na kitamaduni mara nyingi huliangalia kama kushindwa kimaadili badala ya suala la kiafya, na kufanya iwe vigumu kwa familia zilizoathirika kuomboleza waziwazi.
Nchini Kenya, si jambo la kawaida kwa familia kuficha chanzo cha kifo kutokana na hofu ya aibu.
Katika baadhi ya jamii, wale wanaojiua wanakosa haki za maziko za kitamaduni, wakati familia zinaweza kukutana na ubaguzi na kutengwa.
Vikwazo hivi vya kitamaduni vinafanya iwe vigumu kwa watu kutafuta msaada, hata mbele ya mabadiliko ya sheria.
Viongozi wa dini katika nchi nyingi za Afrika bado wanasimama dhidi ya jaribio la kujiua.
Askofu Mkuu Peter Ogunmuyiwa, afisa mkuu katika Shirikisho la Kikristo la Nigeria (CAN), moja ya makundi makubwa ya kidini nchini humo, anasema ni Mungu pekee anayeweza kuchukua uhai kama adhabu kwa kosa.
"Moja ya sheria kuu katika Biblia ni kwamba 'hautakiwi kuua,'" anasema.
"Ni dhambi mbele za Mungu, dhambi isiyoweza kusamehewa kamwe, hasa inapofanyika kwa makusudi."
Hata hivyo, Askofu Mkuu Ogunmuyiwa anasema kuwa kutakuwa na msamaha kwa watu walio na ugonjwa wa akili waliothibitishwa kitaalamu.
Vilevile, Sheikh Ibrahim Lithome, mtaalamu wa elimu ya Kiislamu kutoka Kenya na mshauri wa kisheria na kidini wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya, anasema kujiua kuna marufuku katika imani ya Kiislamu.
"Maisha ni ya Allah, na hakuna mtu anayekubalika kuharibu. Ingawa hakuna adhabu ya kidunia, lakini kuna adhabu kali katika maisha ya baadaye," anasema.
"Wale wanaojaribu kujiua lakini wanaokoka bila kuaga dunia bila shaka wamefanya dhambi," anasema, akiongeza kuwa wanapaswa kutafuta msamaha.
Anasema waathirika wanahitaji msaada, si adhabu, ushauri na muongozo wa kiroho ili kuwasaidia kupata tumaini.
Zaidi ya dini, mtetezi wa afya ya akili kutoka Kenya, Amisa Rashid, anaamini kwamba sababu za kitamaduni, kama vile lugha, pia zinadumisha aibu.
Anaeleza kwamba neno la Kiswahili linalotumika kwa ajili ya psychosis linatafsiriwa kama "mtu aliye kichaa." Lugha hii, anasema, inahatarisha kuwatenga zaidi wale wanaoishi na matatizo ya afya ya akili.
Anasema kubadilisha lugha inayotumika kwa afya ya akili, hasa katika lugha za kienyeji, kutasaidia kukuza huruma na uelewa.
Mafunzo Kutoka kwa nchi nyingine
Uzoefu wa Ghana unatoa mitazamo muhimu kwa mabadiliko ya Kenya.
Tangu kuondoa uhalifu wa jaribio la kujiua, Ghana imeanzisha kampeni za kitaifa za uhamasishaji na kuboresha huduma za afya ya akili ili kuhamasisha tabia za kutafuta msaada.
Hata hivyo, nchi hiyo inaendelea kukabiliana na rasilimali chache za kushughulikia changamoto ya afya ya akili na aibu kubwa katika jamii.
Nchini Nigeria, ambapo kujiua bado ni kosa la jinai, vikundi vya utetezi vinashirikiana na serikali kubadilisha sheria.
Timu ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Kufutia Uhalifu wa Kujiua ilianzishwa mwaka 2024, na lengo ni kuwasilisha muswada bungeni ndani ya mwaka mmoja.
Wataalamu nchini Nigeria wanataja uamuzi wa mahakama wa Kenya kama chanzo cha msukumo kwa mageuzi kama hayo nchini mwao.
"Tumepatiwa mwaka mmoja; tayari tunafanya kazi kulingana na masharti yetu ya rejea," anasema Cheluchi Onyemelukwe, mwenyekiti wa timu ya utekelezaji ya Nigeria.
"Tunatumai kwamba ndani ya mwaka mmoja, tutashuhudia hili likitokea kwetu."
Mustakabali wa Kenya
Ingawa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Kenya ni hatua muhimu, bunge la nchi hiyo sasa linahitaji kuchukua hatua ili kufuta sheria rasmi.
Wanaharakati wa masuala ya afya ya akili wanasisitiza hatua za haraka za kisheria ili kuhakikisha kuwa uamuzi wa mahakama unaleta mabadiliko ya sera yanayoonekana.
Shirikisho la Kimataifa la Kuzuia Kujiua (IASP) linashirikiana na washirika wa Kenya kusukuma mageuzi zaidi.
Kulingana na Katherine Thomson kutoka IASP, kufutia uhalifu ni hatua ya kwanza, lakini serikali lazima pia ziwekeze katika huduma za afya ya akili na kampeni za uhamasishaji kwa umma.
"Uhamasishaji kwa wahudumu wa kwanza; polisi, mahakama, viongozi wa jamii na wafanyakazi wa afya ili kuwasaidia watu kwa huruma," anasema.
"Vyombo vya habari pia vina jukumu muhimu katika jinsi vinavyoshughulikia habari za kujiua ili kusaidia kubadilisha mtazamo."
Kwa wanaharakati kama Amisa Rashid, kumbukumbu ya Charity Muturi inatoa ukumbusho wa umuhimu wa utetezi endelevu.
"Sauti ya Charity ilikuwa na nguvu kwa sababu alizungumza kutokana na uzoefu wa maisha. Tunahitaji kuendeleza moyo huo na kuhakikisha kuwa watu wenye matatizo ya afya ya akili pia wanakuwa mbele katika mijadala ya sera."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga








