Kutothaminiwa kwa wanafunzi wa udaktari Kenya kunavyochangia kujitoa uhai

Chanzo cha picha, Kiambu county's Department of Health Services
Hali ya huzuni ilitanda kijiji kimoja katika Bonde la Ufa nchini Kenya wiki iliyopita huku madaktari kadhaa wakijumuika na waombolezaji wengine katika mazishi ya mwenzao aliyejitoa uhai.
Mzungumzaji mmoja baada ya mwingine waliomboleza kumpoteza Francis Njuki, mfanyabiashara mwanafunzi wa tiba mwenye umri wa miaka 29, ambaye familia yake iliambia BBC kuhusu hisia zake za kuchoka na kufadhaika kutokana na kutolipwa mshahara wake na serikali tangu aanze kufanya kazi rasmi katika eneo hilo Agosti.
Ni daktari wa tano kujiua nchini Kenya katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kwa sababu ya "msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa mazingira ya kazi na kutohakikishiwa bima ya maisha", kulingana na Dkt Davji Atellah, katibu wa Muungano wa Madaktari na Madaktari wa Meno Kenya (KMPDU) - anayeongeza kuwa haikuwa kitu ambacho umoja huo ulikuwa umewahi kushuhudia hapo awali.
Pia kulikuwa na majaribio matano ya kujiua yaliyofanywa na wanachama wa KMPDU mwaka huu, shirika hilo la matatibu lilisema.
Bado hakuna takwimu zinazopatikana kuhusu idadi ya watu waliojiua nchini Kenya mwaka huu.
Njuki alikuwa akifanya mazoezi ya mafunzo yake katika hospitali ya serikali katika mji wa Thika karibu na mji mkuu, Nairobi, alipojiua mwezi uliopita.
Alikuwa ameripoti kuota ndoto na huzuni kutokana na kukosa usingizi, mjombake Tirus Njuki aliambia BBC.
"Katika barua yake ya kujitoa uhai alitaja kuwa kucheleweshwa kwa mishahara ya miezi minne ni miongoni mwa masuala yaliyozidisha ugonjwa wake wa kiakili, hivyo kumfanya akatishe maisha yake," mjomba huyo aliongeza.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mzaliwa wa kwanza katika familia yake, mwanafunzi huyo alikuwa akipambana na msongo wa mawazo na alikuwa akipokea matibabu, kulingana na ripoti ya polisi.
Njuki alikuwa miongoni mwa mamia ya wanafunzi ambao waliwekwa kwenye vituo vya afya mwezi Agosti kufanya mafunzo yao ya lazima ya mwaka mmoja ili kufuzu.
Lakini wafanyakazi hao wanasema hawakuwa wamepokea mishahara yao kwa miezi minne ya kwanza, huku serikali ikitaja changamoto za kifedha.
Hii ni licha ya ukweli kwamba wanafunzi waliohitimu mafunzo ni sehemu muhimu ya wafanyikazi katika hospitali za umma - zinazotumiwa na Wakenya wengi ambao hawawezi kumudu bima binafsi ya matibabu.
Waliofunzwa ni takriban 30% ya madaktari katika sekta ya afya serikalini.
Wanafanya kazi nyingi katika hospitali za umma, lakini chini ya uangalizi wa karibu.
Wanapiga simu, wakati mwingine kwa saa 36, na hutoa huduma nyingi za afya ambazo wagonjwa wanahitaji.
"Kama wenzake wengi, Dkt Njuki alikabiliwa na changamoto kubwa katika kukidhi mahitaji ya kimsingi kama vile kodi ya nyumba na matumizi," KMPDU ilisema kwenye taarifa.
Serikali imekuwa katika mzozo wa muda mrefu na vyama vya wafanyikazi kuhusu malipo na mazingira ya kazi ya wafanyikazi.

Chanzo cha picha, AFP
Serikali imependekeza kupunguza mishahara ya kila mwezi ya wahitimu hadi $540 (£430).
Muungano huo unataka ibaki $1,600 kama ilivyokubaliwa na serikali mnamo 2017.
Lakini Rais William Ruto amesema kuwa serikali haiwezi kumudu kulipa kiasi hicho, na "lazima tuishi kulingana na uwezo wetu".
"Hatuwezi kuendelea kutumia pesa ambazo hatuna," Ruto alisema mapema Aprili.
Kufuatia shinikizo linazoongezeka na vitisho vya mgomo, serikali mwezi uliopita ilitoa $7.4m kulipa zaidi ya wanafunzi 1,200 ambao hawakupokea mishahara yao tangu Agosti.
Baadhi ya wahitimu wanasema wanalipwa "karanga".
"Baada ya miaka sita hadi saba ya masomo, ilitubidi kungoja kwa miezi kadhaa kupata mafunzo ya kazi. Na kisha kwa muda mrefu wa kufanya kazi, serikali iliamua kutulipa karanga. Tunateseka sana," Dk Abdi Adow, mwanafunzi katika hospitali ya Mbagathi jijini Nairobi, aliambia BBC.
Dkt Adow ni miongoni mwa mamia ya madaktari chipukizi ambao wapo njia panda kati ya kuondoka nchini kutafuta kazi ng'ambo au kuacha taaluma hiyo ili kusaka kazi zinazolipwa vizuri.
Mwanafunzi mwingine ambaye alizungumza na BBC kwa sharti la kutotajwa jina lake kwa kuhofia kulipizwa kisasi, alisema: "Nimeapa kuokoa maisha, angalau, na kurejesha afya, bora zaidi, lakini serikali inafanya kila kitu kuua maisha yangu,bidii na kudhoofisha kiapo changu cha utumishi."
Wataalamu wanataja kifo cha mwezi uliopita cha Dkt Timothy Riungu kama mfano wa jinsi hali za kazi zilivyo ngumu kwa madaktari.
Alikuwa daktari wa watoto katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi, ambaye alianguka na kufariki akiwa nyumbani baada ya kutoka zamu ya mchana; alikuwa amelalamika mara kwa mara juu ya uchovu kwa msimamizi wake siku hiyo, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Daktari huyo mwenye umri wa miaka 35 alikuwa na kisukari na hakuwa amechukua likizo kwa miaka miwili, kulingana na familia yake.
Uchunguzi wa kitaalamu wa mwili wake ulionyesha kuwa Dkt Riungu alifariki kutokana na hypoglycemia, iliyosababishwa na kiwango cha sukari kwenye damu kushuka chini ya kiwango cha kawaida.
Pia ilionyesha hakuwa amekula chochote kwa zaidi ya saa 48 kabla ya kifo chake.
Mwezi Mei, serikali ya Kenya ilifikia makubaliano na chama kimoja cha madaktari ili kusitisha mgomo wa siku 56, lakini suala kuu la mishahara ya wahitimu wa mafunzo lilibaki pasipo kutatuliwa.
Mgomo huo ulikuwa umesimamisha shughuli katika hospitali za umma, huku makumi ya wagonjwa wakiripotiwa kupoteza maisha.
Duru kadhaa za mazungumzo zimesambaratika kuhusu malipo na mazingira ya kazi ya wahitimu.
Wiki iliyopita, KMPDU iliwaamuru madaktari wote kusalia nyumbani huku ikitoa notisi mpya ya siku 21 ya mgomo wa kitaifa, ikishutumu serikali kwa kupuuza makubaliano yaliyoafikiwa Mei.

Chanzo cha picha, KMPDU
Mnamo Septemba, mwanafunzi wa utabibu aliyekuwa na umri wa miaka 27 katika Hospitali ya Gatundu mwaka wa 5 katikati mwa kaunti ya Kiambu alijiua.
Dkt Desree Moraa Obwogi alikuwa amemaliza zamu ya saa 36 ambayo ilikuwa imeathiri hali yake ya afya ya akili, kulingana na wafanyakazi wenzake.
Walisema pia alitatizika kulipa kodi yake na gharama nyingine za mahitaji.
Dkt Muinde Nthusi, mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano ya Ndani ya KMPDU, alilaumu mazingira magumu ya kazi na kukosa fedha vimesababisha kifo chake.
Wakati wa mazishi, familia ya Obwogi iliomba serikali kuwajibika kwa maisha yaliyopotea, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Visa vingine vya hivi karibuni vya kujitoa mhanga vilivyobainishwa na KMPDU ni pamoja na Vincent Bosire Nyambunde, mfanyakazi katika Hospitali ya mafunzo na Rufaa ya Kisii; Collins Kiprop Kosgei, mwanafunzi wa mwaka wa tano wa utabibu katika Chuo Kikuu cha Nairobi na Keith Makori, mtabibu mwenye umri wa miaka 30 kutoka katikati mwa kaunti ya Kiambu.
Madaktari chipukizi wamekuwa wakihamasishwa kwenye mtandao wa X chini ya kauli mbiu ya #PayMedicalInterns ili kushinikiza malipo bora na mazingira ya kazi.
Waliandamana hadi ofisi za Wizara ya Afya wiki iliyopita ili kuelezea masikitiko yao.
"Madaktari na wauguzi wetu wanabeba majukumu mazito ya mfumo wa afya uliodhoofu, ilhali kilio chao kimezidiwa na uroho wa walio mamlakani," Dkt Kipkoech Cheruiyot alichapisha kwenye jukwaa la X.
Maafisa wa afya hawakujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao.
Lakini akijibu ongezeko la visa vya watu kujiua mwezi Septemba, Waziri wa Afya Deborah Barasa alisema "ni ukumbusho wa mapambano ya kimyakimya ambayo wengi, wakiwemo wale walio katika sekta ya afya ambayo mara nyingi hupitia na kustahimili".
Waziri alitangaza mipango ya kuanzisha programu za "afya ya akili mahali pa kazi" kwa wafanyikazi wa afya kote nchini "kuhakikisha kuwa mifumo ya usaidizi inaimarishwa na kwamba wale wanaokabiliwa na changamoto hawajisikii kuachwa peke yao".
Wataalamu wa tiba walisema madaktari wengi chipukizi pia huathirika kisaikolojia hasa wanapohisi hatia kwa kutofanya vya kutosha kuwatibu wagonjwa, ingawa walijaribu wawezavyo katika mazingira magumu.
"Fikra kwamba ungeweza kufanya kitu kuokoa maisha ya mgonjwa lakini usingeweza, inaweza kusababisha hisia za hatia, aibu, na kutokuwa na uwezo, na hivyo kuchangia masuala ya afya ya akili," Dk Chibanzi Mwachonda, daktari wa magonjwa ya akili, aliambia gazeti la Standard la Kenya.
Madaktari walioko mafunzoni waliambia BBC kwamba shule nyingi za tiba hazizungumzi ipasavyo mada ya kujiua, na kuwaacha madaktari wapya na waliochoka wakiwa na vifaa duni vya kukabiliana na changamoto ya msongo,shauku,na hii inachangiwa na malipo duni.
"Daktari mwenye afya njema hujenga taifa lenye afya nzuri. Ninapofadhaika kama daktari, naweza hata kusahau jinsi ya kumsaidia mgonjwa, ambayo inaweza kusababisha kupoteza maisha," daktari mmoja alisema.
"Daktari aliyeshushwa daraja ni mtu hatari kukuhudumia. Inakuwa kazi isiyo na shukrani."
Takriban Wakenya 1,400 hufa kwa kujitoa uhai kila mwaka, kulingana na Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya. Lakini wachambuzi wengine wanaamini kuwa idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.
Kujiua bado ni kosa la jinai nchini Kenya, ambapo wale wanaopatikana na hatia ya kujaribu kujiua wanaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka miwili, faini, au vyote kwa pamoja.
Sheria hii imekuwa ikikosolewa vikali, huku baadhi ya mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitaka ifutiliwe mbali, yakisema kuwa inanyanyapaa zaidi masuala ya afya ya akili na kuwazuia watu kutafuta msaada.
"Tutazika madaktari wangapi ili serikali ichukue hatua?" aliuliza Dr Adow.
Imetafsiriwa na Martha Saranga












