Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ufalme wa Chola: Je, ni kwanini wanawake hawa walizikwa hai na mfalme aliyefariki?
- Author, Mayakrishnan Ka
- Nafasi, BBC Tamil
- Iliyochapishwa
Katika kipindi cha utawala wa Chola, huko Tamil Nadu, India tukio la kushangaza lilitokea ambapo mfalme alieaga dunia alizikwa na wanawake walio hai.
Hilo lilifanywa kwa matumaini kwamba wataishi wote hata baada ya kifo. Wanawake watatu walizikwa wakiwa hai pamoja na mfalme aliyekufa.
Tulikwenda katika kijiji cha Thamaraipakkam ili kujua kuhusu tukio hili la wakati wa utawala wa Koothatum Prithikangan katika eneo la Thiruvannamalai katika ufalme wa Kulothunga Chola.
Wanawake watatu walizikwa
Kabla ya kuingia hekaluni, Katibu wa Kituo cha Utafiti wa Historia cha Wilaya ya Balamurugan, Tiruvannamalai Vattakshiyar ambaye aliandamana na timu ya BBC, alitueleza kuhusu maandishi yaliyopo katika hekalu hilo.
Anasema kuna maandishi katika hekalu hili la Agneeswarar, ambayo yanaeleza habari juu ya waimbaji watatu wa kike waliozikwa wakiwa hai na Mfalme Prithigangan alipofariki. Ni maandishi ya mistari 14 kwenye ukuta wa mashariki wa hekalu la Agneeswarar. Katika ufalme wa Kulothungan III, Mfalme Prithikanga Somanathan aliandika maandishi hayo mwaka 1188.
Yanasomeka "natoa ardhi hii kama fidia kwa familia tatu, ambazo watu wao walizikwa wakiwa hai katika shimo na baba yao aliyekufa, Mfalme Koothatum Deva Prithikangan."
Balamurugan anaeleza kuwa familia za wanawake hao zilipewa shamba kubwa lenye uzio kama fidia ya kupoteza watoto wao.
Maandishi haya yamerekodi majina ya wanawake waliozikwa wakiwa hai. Wanawake hao watatu wa ukoo wa Devaradiyar, Aadum Alwar, Saturanadai Perumal na Niraitha Vanjethal.
Balamurugan anasema kupitia tukio hili tunaweza kujua hali za kijamii za wanawake wakati huo. Pia anasema ni uthibitisho kuwa wanawake wameteseka katika enzi hizo.
Falme Nyingine
Falme za Andhra na Karnataka nchini India, pia zilikuwa na desturi hiyo. Profesa Ramesh wa Idara ya Historia ya Chuo cha Sanaa cha Anna, Villupuram, anasema mila na desturi hizo za ajabu zimerekodiwa katika historia.
"Maandishi yanayohusiana na matukio kama haya yanapatikana sio tu Tamil Nadu, kuna maandishi kama hayo huko Andhra Pradesh na Karnataka."
Maandishi ya mistari 24 katika Bwawa la Kijiji cha Hoondi, Wilaya ya Mysore, yanataja ndoa ya mke na mume wake aliyekufa.
Vile vile, maandishi ya Kannada yenye mistari 25 yaliyochongwa kwenye ubao kusini mwa kijiji cha Kalukode, wilaya ya Bellary yanasema askari alizikwa pamoja na mfalme aliyekufa.“
Wakati huo wafalme waliheshimiwa kuwa sawa na Mungu. Na neno lao liliheshimiwa kama neno la Mungu. Kwa hivyo, yanaweza kuchukuliwa kuwa ni matendo ya ujinga au kielelezo cha nguvu," anasema Profesa Ramesh.
Kilele cha Ushirikina
Akizungumzia matukio ya ajabu kama haya na tabia za ajabu za watu wa wakati huo, Dk. Udaya Kumar anasema, "matukio kama kupanda daraja na kujiua yanaweza kusemwa ni upotovu wa akili. Ni kilele cha ushirikina. Inaumiza mtu akiacha maisha yake ya thamani."
"Sababu ni kwamba yawezekana waliamini baada ya kifo kuna ulimwengu mwingine ambapo anaweza kwenda kuishi na wapendwa wao.
"Kuna wakati walikuwa wakizika watu wawapendao kama walivyokuwa wakizika vitu wavipendavyo na maiti. Hii ni sawa na ushirikina," anasema daktari wa magonjwa ya akili Uday Kumar.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah