Enatha Cyuzuzo, msichana mhandisi ujenzi ,mfano kwa vijana

Iliyochapishwa

Yves Bucyana

BBC Swahili

Wanawake wanaongezeka katika kazi ya ujenzi nchini Rwanda, lakini ni wachache sana kati yao wanaopatikana wakifanya kazi kama wahandisi katika maeneo ya ujenzi, Enatha ni miongoni mwao.

Kujenga nyumba ni taaluma aliyosomea chuo kikuu, lakini pia ni jambo ambalo alipenda tangu akiwa mdogo, kwa msaada wa wazazi na kaka zake, kama alivyoiambia  BBC.

Katika ofisi ya kampuni yake ya Ela Poder Construction Company, na katika moja ya nyumba anazojenga katika mji wa  Nyagatare, Cyuzuzo huajiri wanaume na wanawake ambao wanamzidi kwa rika.

 Moja ya nyumba anayojenga inakaribia kukamilika. “Tunapojenga nyumba tunakwenda hatua kwa hatu, kuna hatua ya kwanza ya kupanga -hiyo hasa ndiyo kazi kubwa, yaliyobaki  yako kwenye karatasi nayafikiria tu kichwani na kuyatekeleza nikiwa kiwanjani-‘’

Alisema: "Hapa unahitaji kuwa makini sana kwa sababu Wilaya itaangalia ikiwa  ramani ya nyumba inakwenda sambamba na ramani ya mji’’

Katika kazi yake ,msichana huyo mwenye umri wa miaka 26  hufunga  mikataba ya ujenzi na kuwapa ajira wanawake na wanaume ambao pia wanafwata maagizo yake kuhusu nini cha kufanya,kisha kuwalipa.

Mmoja wa wafanyakazi wake, Tuyishime Fidela, alisema: "Ninajisikia furaha sana kuwa mtu anayesimamia eneo la ujenzi  ni msichana mwenzangu , na ninahisi kwamba nitafika hapo alipo."

Nyirubwite Martine, mwenye umri wa miaka 39, pia ameajiriwa na Enatha aliambia BBC kwamba wakati fulani mmoja wa Watoto  wake alisema kwamba yeye pia atapigania kuwa Mhandisi kama ‘muajiri wa mama’ yaani Enatha-

Alisema: "Wakati tunajenga, anatuambia 'ukiona kitu kibaya, nishauri kama mtu mzima',lakini hatujaona  chochote kisichokwenda sawa’’

'Siwezi kushindwa'

Cyuzuzo akiwa mhandisi wa ujenzi amejenga nyumba Kigali anakotoka na Nyagatare ambapo aliamua kufanyia kazi kwa kuona ni jiji ambalo litaendelea kutoa kazi nyingi za ujenzi hapo baadae.

Gatete Athanase, ambaye alimpa kazi ya kumjengea nyumba katika jiji la Nyagatare, anasema kuwa alimpa kandarasi  hiyo  kwa sababu aliona kuwa ana uwezo.

“Anajua kujenga, na ujenzi si kitu cha kuficha.Nyumba ni kitu ambacho unaweza  kuona   na kusema ‘nyumba hii imejengwa vizuri’, kwa hiyo vitendo vyake  [hapo awali]  vinadhihirika - ana uwezo na ubunifu’’.Alisema Gatete

 Hata kama  hana uzoefu wa miaka mingi katika kazi hii, Cyuzuzo anasema kwamba sasa anajiamini, lakini hajasahau  alivyoanza- Nyumba ya kwanza  aliyosimamia kujenga.

Kwa sababu ya  sehemu mbaya  ambako ilikuwa  , haikuwa rahisi, alisema: "Yaani nyumba hii ilikuwa ngumu kwangu! Nilifika mahali ambapo hata usingizi nikakosa’’.

"Lakini baada ya kumalizika kwa nyumba hiyo ikanifanya nijichunguze mwenyewe  , nikawa mtu tofauti  kabisa na nilihisi kuwa nimekuwa mtu mzima.Ujenzi wa nyumba hiyo ulinitatiza  sana kuliko ujenzi wa gorofa –lakini nilipoikamilisha nikasema ‘hakuna kitu kinachoweza kunishinda‘’

Miongoni mwa nyumba kadhaa  alizojenga Nyagatare, kuna jengo la biashara mjini hapo, ambalo ni moja ya nyumba anazozipenda zaidi.

"Inanifanya nijivunie kuingia ndani ya jengo hilo na kushuhudia  wateja wakiegesha magari na kuingia ndani japo siyo jengo langu  lakini najisikia furaha moyoni na kusema 'waww! nilichofanya kinaonekana’, alisema Cyuzuzo.

Anasema Kuchora ramani  ni moja ya talanta ambayo aligundua kuwa alikuwa nayo tangu utotoni. 

Ugumu wa kufanya kazi na baadhi ya wanaume

 Anafanya kazi zaidi na wanaume na anasema kuwa hii husababisha baadhi ya matatizo ambayo anakumbana nayo  yatokanayo na  mitazamo ya baadhi yao.

 Anasema : "kuna baadhi  wanaofikiria kwamba msichana huwezi kupanga naye mambo ya kazi tu.

 “Yaani kufanya kazi na mwanaume unahitaji  kujifananisha naye-wengi wakikuona kuwa wewe ni msichana wanataka kukutongoza hata kama wewe ni Bosi!lakini ukimuonyesha mwanaume   kuwa wewe pia uko kama yeye –una uwezo na ukimuonyesha kuwa  wewe ni msichana ‘mwenye akili’, utakuwa umemweza na hapo ndipo mwanaume anaishiwa  na kukosa la kufanya.’’

 Enatha Cyuzuzo ana mpenzi wake ambaye  wanatarajia kufunga ndoa  ‘’hivi karibuni’’.Mpenzi wake huyo  anasema anapenda ‘kazi yangu’ na "ni moja ya sababu inayonifanya kuwa na nguvu ya kufanya kazi".