Kigimbi: Kwa nini msuli huu unaoitwa 'moyo wa pili' ni muhimu sana?

Iliyochapishwa

Misuli iliyo katika sehemu ya kigimbi, ni mojawapo ya misuli muhimu katika mwili. Sio tu kuweka sawa mwili, lakini kuna mishipa muhimu ndani yake ambayo ina jukumu muhimu katika mzunguko wa damu.

‘Kile kinachoifanya sehemu hiyo kuwa muhimu ni muundo wake,’’ anasema Dk. Carles Pedret, mhadhiri katika idara ya Sports Medicine, Chuo Kikuu Barcelona.

''Kuna mishipa mingi, na imekusanya tishu ambazo zinaunganika na tishu za mishipa mengine. Na zote hufanya kazi kwa pamoja.’’

Kuzalisha Nguvu

"Misuli hii ni muhimu kwa shughuli yoyote inayohusisha kusimama au kutembea," anaeleza Dk. Marc Hamilton, kutoka Chuo Kikuu cha Houston, Texas.

Misuli hiyo imeundwa na aina tofauti za tishu kulingana na kazi zake.

Ni misuli inayodumisha mwonekano wa mwili wako. Ni misuli ambayo inaweza kukufanya ubaki umesimama muda mrefu au kutembea bila kuchoka.

"Kigimbi kina kiasi kikubwa cha tishu ambazo ni muhimu katika kuzalisha nguvu. Huzalisha kiasi kikubwa cha nishati," anaeleza Dk. Pedret.

Mkusanyiko huu wa tishu ambao hufanya misuli hii, ambayo inawakilisha 1% ya uzito wa mwili, ina uwezo mkubwa wa kuzalisha nguvu kuliko viungo vingine vingi vya mwili.

Kusukuma Damu

Kigimbi pia kina kazi maalumu sana, kinasaidia moyo katika kazi yake ya kusukuma damu kuzunguka mwili.

Dkt. Hámilton anaeleza jinsi mchakato huu unavyofanya kazi. Muundo wa misuli ya kigimbi ni tofauti na ile ya misuli mingine. Kimsingi, kwa kila hatua unayopiga unasukuma damu iliyo kwenye miguu yako kurudi kwenye moyo.''

Faida ya Misuli hii

Kama ilivyo kwa misuli yote ya mwili, kigimbi kinahitaji kufanya kazi ili kuwa na afya. Lakini kazi hiyo inatakiwa iwe ya polepole na ya kudumu.

Dkt. Pedret anasema, ‘kazi bora ni kutembea. Watu hufikiri kwa kufanya kazi nyingi misuli ndio inakuwa na afya. Lakini ukweli kinachohitaji ni kazi endelevu ya polepole.

"Maisha ya kukaa tu ni mabaya kwa misuli hii, lakini kuifanyisha kazi ya nguvu pia ni hatari."

Ni kanuni muhimu linapokuja suala la misuli yetu, ambayo wanasayansi wanazidi kuihusisha na utendaji jumla wa miili yetu.

"Ninachosema kila wakati ni kwamba watu kwa kawaida huhusisha ubora wa maisha katika uzee na kuwa na afya nzuri ya akili, ingawa hilo ni kweli, lakini ubora wa maisha hupatikana kwa kuwa na misuli imara," anasema Pedret.

"Kudumisha afya kwa misuli hufanya mfumo mzima wa mwili ufanye kazi vizuri zaidi. Inapunguza hatari ya magonjwa. Ubongo pia hufanya kazi vizuri na huboresha afya ya akili.

imetafsiriwa na Rashid Abdalla