Ongezeko la ugonjwa wa kaswende ya kuzaliwa nayo lilivyo changamoto

Iliyochapishwa

Kaswende ni mojawapo ya magonjwa ya kale zaidi yanayojulikana ya zinaa.

Kuna kipindi ilifikiriwa kuwa umepungua, lakini sasa unarudi kwa kasi ya kutisha.

Ugonjwa kaswende umeitwa majina mengi tangu rekodi yake ya kwanza katika miaka ya 1490, lakini moja wapo ambalo limeendelea kusikika ni: "mwigaji mkuu".

Kaswende ni ugonjwa hodari wa kuiga maambukizi mengine na dalili za awali ni rahisi kukosa kujulikana.

Ikiwa hautatibiwa, matokeo yanaweza kuwa mabaya.

Tushar, afisa wa mradi, 33, huko Amsterdam, amekuwa na kaswende mara mbili.

Anakumbuka kwanza alipopokea habari hizo kupitia WhatsApp kutoka kwa mpenzi wake aliyekuwa wanashiriki naye ngono wakati huo.

"Walikuwa wamekasirika sana," anasema. "Walinilaumu jambo ambalo halikuwa kweli hasa ukizingatia kipindi ambapo maambukizi ya kwanza yalibainika na muda ambao vipimo vilifanywa kubaini ugonjwa huo. Nilihisi vibaya kushtumiwa na ilichukua muda kuondoka akilini mwangu."

Tushar alipimwa na kutibiwa wiki hiyo.

"Watu wanafikiria visivyo kuwa kaswende ni ugonjwa ambao hauwezi kutibika. Watu hawaelewi maana ya kuwa na kingamwili za kaswende na kutokuwa na maambukizi."

Mnamo Aprili, Marekani ilitoa data yake ya hivi punde kuhusu magonjwa ya zinaa (STI).

Maambukizi ya ugonjwa wa kaswende yameongezeko pakubwa, huku yakiongezeka kwa 32% kati ya 2020 na 2021 kufikia idadi kubwa zaidi ya maambukizi yaliyoripotiwa katika kipindi cha miaka 70.

Ugonjwa huo pia hauonyeshi dalili za kupungua, Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) vimeonya.

Na imeashiria mwelekeo mpya "wa kutisha" unaoendesha ongezeko hili la ghafla.

Kaswende ya kuzaliwa nayo - ambapo mama hupitisha maambukizo kwa mtoto wake wakati wa ujauzito, mara nyingi baada ya kuambukizwa na mwenzi wake - imeongezeka sana.

Ugonjwa huo unaweza kusababisha mtoto kufa akiwa bado tumboni, vifo vya watoto wachanga na matatizo ya afya kwa kipindi kirefu cha maisha.

Hali hiyo imewaacha wataalam wengi wa afya wakihangaika kutafuta ufumbuzi.

"Miaka kumi na tano au 20 iliyopita tulifikiri kwamba tulikuwa karibu kumaliza kabisa ugonjwa wa kaswende," anasema Leandro Mena, mkurugenzi wa kitengo cha kuzuia magonjwa ya zinaa kutoka CDC.

"Bila shaka tunachokiona ni kuongezeka kwa viwango vya ugonjwa wa kaswende, ambavyo hatujavishuhudia katika kipindi cha miaka 20 hivi."

Na si kitu kinachotokea tu nchini Marekani.

Kulikuwa na visa vipya milioni 7.1 vya kaswende ulimwenguni mnamo 2020 kulingana na data ya Shirika la Afya Ulimwenguni.

Mnamo mwaka 2022, Uingereza ilishuhudia maambukizi ya kaswende yakifikia kiwango cha juu zaidi tangu 1948.

Kuongezeka kwa maambukizi ni jambo ambalo wahudumu wa afya ya ngono wamezoea kulishuhudia.

"Nilipoanza uuguzi wa afya ya ngono mnamo mwaka 2005, ilikuwa nadra sana kupata mtu na ugonjwa wa kaswende, hata katika kliniki ya katikati mwa jiji," anasema Jodie Crossman, mwenyekiti wa taasisi ya STI nchini Uingereza, ambapo viwango vya kaswende viliongezeka kwa 8.4% kati ya 2020 na 2021. "Sasa kliniki nyingi za mjini zina angalau wagonjwa wawili au watatu kwa siku wanaopata matibabu."

Maambukizi husababishwa na bakteria aitwaye Treponema pallidum na dalili zimegawanywa katika hatua nne.

Dalili za awali kabisa ni pamoja na kidonda kisicho na uchungu kwenye eneo la ugonjwa au upele.

Dozi inayodungwa ndani ya misuli ya penicillin inachukuliwa kuwa njia bora zaidi ya kutibu maambukizi.

Hata hivyo, isipotibiwa, kaswende inaweza kusababisha magonjwa ya muda mrefu ya neva na mishipa ya damu.

Anayetazama janga hilo likitokea Marekani kutoka mpakani mwa Canada ni Isaac Bogoch, daktari wa magonjwa ya kuambukiza na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Toronto.

"Huu ndio mtindo ambao unaonekana katika nchi nyingi ulimwenguni," anasema.

"Inatia wasiwasi sana kwa sababu kwa ujumla, kaswende ni rahisi sana kutibika, na matibabu yanapatikana kwa wingi. Kwa hivyo, mengi ya haya yanaakisi matatizo kwa mfumo wa huduma ya afya ya umma."

Canada ilishuhudia maambukizi ya ongezeko la 389% ya ugonjwa wa kaswende, ikiwa ongezeko la juu zaidi kuliko magonjwa mengine ya zinaa, kati ya 2011 na 2019.

Katika miongo ya hivi karibuni, maambukizi mengi ya kaswende ni kati ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, watu wa jinsia mbili na wanaume wengine wanaofanya ngono na wanaume wenzao.

Baadhi ya sehemu za dunia, hata hivyo, zinashuhudia kupungua kwa maambukizi ya kaswende miongoni mwa wanaume.

Kwa mfano, viwango vya maambukizi ya kaswende nchini Canada vilipungua miongoni mwa wanaume.

Lakini wakati huo huo kumekuwa na ongezeko la viwango vya maambukizi ya ugonjwa huo miongoni mwa wanawake sio tu nchini Canada bali kimataifa, jambo ambalo limesababisha viwango vya juu vya kaswende ya kuzaliwa katika sehemu nyingi za dunia.

Kote katika bara la Amerika kwa ujumla kulikuwa na maambukizi 30,000 ya ugonjwa wa kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto mnamo 2021, takwimu ambayo maafisa wa afya wanaelezea kuwa "kiwango cha juu kisichokubalika".

Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito kwa mtoto aliye tumboni yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuharibika kwa mimba, kujifungua mtoto ambaye tayari ameshafariki, mtoto kuzaliwa kabla ya wakati, kuwa na uzito mdogo na kifo cha mtoto muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Nchini Marekani, viwango vya kaswende ya kuzaliwa vinaongezeka. Vilikuwa mara 3.5 zaidi mwaka wa 2020 ikilinganishwa na 2016 na imeongezeka tena mwaka 2021, na kusababisha vifo vya watoto kabla na baada ya kuzaliwa 220.

Na takwimu za kitaifa zinaonekana kuficha ongezeko kubwa la ugonjwa huu katika baadhi ya maeneo ya nchi - madaktari huko Mississippi wameripoti visa vya watoto kuzaliwa na ugonjwa wa kaswende kuongezeka kwa 900% katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Idadi kubwa zaidi inaonekana kati ya wanawake wa Marekani Weusi na Wahispania.

"Hiyo inaonyesha ukosefu wa usawa na ubaguzi wa rangi ambao bado tunao katika vituo vya afya vya umma na miundombinu ya matibabu," anasema Maria Sundaram, mwanasayansi mtafiti katika Taasisi ya Utafiti ya Kliniki ya Marshfield huko Wisconsin.

Kundi lililo hatarini zaidi la wanawake, kama vile wale ambao wamepoteza makazi yao au wanapambana na matumizi ya dawa za kulevya, pia wameathiriwa zaidi na ugonjwa huo.

Na kiwango kikubwa cha ukosefu huu wa usawa kulizidishwa na janga la Covid-19 kote ulimwenguni.

"Makubaliano katika jumuiya ya afya ya umma ni kwamba kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na kaswende kunawezekana kuhusiana na kukatizwa kwa rasilimali za kuzuia magonjwa ya zinaa wakati wa janga hili," anasema Sundaram.

Miongoni mwa sababu zinazoweza kusababisha tatizo hili ni pamoja na upatikanaji wa maeneo ya kupima magonjwa ya zinaa, unyanyapaa unaoendelea kuhusu kaswende na vizuizi vinavyowezekana vya lugha.

Utafiti mmoja nchini Brazil uligundua uhusiano kati ya wanawake weusi ambao walikuwa na viwango vya chini vya masomo na viwango vya juu vya kaswende ya kuzaliwa.

Katika maambukizi mengi wanawake wanatatizika kupata huduma ya kabla ya kuzaa inayofaa ambayo inaweza kutoa uchunguzi wa kaswende.

Utafiti mwingine katika Kaunti ya Kern, California - ambayo mwaka wa 2018 ilijumuisha 17% ya visa vya kaswende vya kuzaliwa licha ya kuwakilisha 2.3% tu ya wakazi wa jimbo hilo - ulibainisha jukumu la hali ya uhamiaji, hali ya bima ya matibabu na unyanyasaji wa kijinsia au unyanyasaji wa nyumbani kwa wanawake wajawazito wanaotafuta huduma wakati wa ujaouzito.

Nusu ya wanawake wajawazito au baada ya kuzaa waliohojiwa walitambuliwa kuwa wa asili ya Kilatino au Kihispania.

Lakini ingawa matatizo ya kupanda kwa gharama ya maisha na janga la corona kumeathiri rasilimali za afya ya umma, pia kumekuwa na mabadiliko katika tabia na mitazamo ya wanadamu dhidi ya magonjwa ya zinaa.

Mabadiliko katika tabia ya ngono ni eneo ambalo watafiti nchini Japani wamekuwa wakitafiti kwa kuangalia uhusiano kati ya programu za uchumba na visa vya kaswende.

Walihitimisha kuwa matumizi ya programu za kuchumbiana "yalihusishwa kwa kiasi kikubwa na matukio ya kaswende," wakiunganisha matumizi ya programu na matukio makubwa ya ngono ya kawaida bila kinga.

Picha:

Hili ni jambo ambalo Sasaki Chiwawa, ambaye anaandika kuhusu utamaduni wa vijana wa Kijapani na biashara ya ngono, pia alibaini katika mazungumzo yake na wafanyabiashara ya ngono.

Chiwawa anasema wafanyabiashara ya ngono zaidi na zaidi hawatumii kondomu na hakuna wajibu kwa wateja kupima magonjwa ya zinaa.

Iwapo wafanyabiashara ya ngono watapata maambukizi, huwa wanasema ni "bahati mbaya," anasema Chiwawa.

"Wengi wao hutanguliza kutafuta pesa kuliko hatari iliyopo."

Kwa maafisa wengi wa afya, njia ya kukabiliana na kaswende iko wazi - tayari tuna dawa za kukabiliana nayo kwani penicillin bado inasalia kuwa tiba bora licha ya kuongezeka kwa matukio ya ukinzani wa viuavijasumu.

Upimaji na uhamasishaji zaidi ili kukabiliana na unyanyapaa unaohusishwa na ugonjwa huo pamoja na uhamasishaji mkubwa wa umma kuhimiza tabia salama ya ngono zote zina jukumu kubwa zaidi la kutekeleza.