Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi kukojoa kitandani kulivyompa hofu mwanamke huyu
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Hali ya mtu kukosa uwezo wa kudhibiti haja ndogo (Mkojo) hasa katika umri wa utu uzima ni kitu ambacho hakijadiliwi waziwazi katika jamii nyingi za Afrika, ila wanaopitia hali hiyo wanaishi na unyanyapaa mwingi, kulingana na mwanaharakati wa masuala hayo Bi. Lucy Wambui ambaye ni mkaazi wa mji wa Nairobi nchini Kenya.
Mwanamke huyu anakiri kuwa katika maisha yake ya utotoni hadi alipotimiza umri wa miaka 15 alikuwa anaishi na hali ya kwenda haja ndogo mara kwa mara kila usiku .
”Ni kitu ambacho kilikuwa kinanihangaisha sana , hasa nilipoingia kwenye miaka ya kujifahamu mimi ni nani ”anakumbuka Lucy
Aidha Lucy anasema kuwa hofu yake kuu hasa alipoanza kubaleghe ilikuwa ni kupata usingizi kwani kilichofuatia kila usiku ilikuwa ni kujipata katika kitanda kilichojaa mikojo .
”Wakati mwengine mama alikuwa ananiadhibu kwa kitendo hicho, hasa siku ambayo angehisi harufu ya mikojo, ila nilikuwa na matatizo ya udhibiti na hakuna aliyekuwa anajua ni jinsi gani ya kunisaidia, mama alikua ni mlezi wetu na ndugu zangu kwani baba alikuwa ameaga dunia ”anasema Lucy
Kero nyengine katika miaka ambayo Lucy alikuwa na mahangaiko ya kukojoa kitandani akiwa usingizini ni ile ya kupigwa marufuku kutembelea marafiki na shangazi wake, kutokana na hofu iliyokuwepo kwamba angeleta aibu .
Anakumbuka siku nyingi za wasiwasi kutokana na kejeli aliyopata kutoka kwa kaka zake kuhusiana na hali yake . Na kwa hivyo hakukua kama mtoto wa kawaida anayecheza na wenzake .
Lucy anasema kuwa alikosa kupitia viwango vyote vya utotoni hasa kutangamana kupitia michezo na shughuli nyengine kwani alilazimika kujitenga na watu ili wasihisi harufu ya mkojo.
Hadi wakati Lucy anajiunga na shule ya sekondari alikuwa bado ana matatizo hayo , ikiwa ni mojawapo ya sababu ambazo zilimfanya asijiunge na shule ya bweni.
Kwa mujibu wa mwanamke huyu ambaye ni binti wa pekee katika familia, pia hali yake iliilazimu familia yake kumkinga dhidi ya aibu ambayo angeleta kutoka kwa jamii.
Hata hivyo anasema kuwa kitu ambacho sio cha kawaida kilifanyika wakati alipotimiza umri wa miaka 15 ambapo akiwa katika kidato cha tatu, aliamka na kugundua alikuwa amekojolea matandiko yake.
Na hadi wakati huo hali yake ilibadilika kabisa .
Kuwa mwanaharakati
Baada ya Lucy kukamilisha shule na kuwa huru na mahangaiko ya kujikojolea akiwa usingizini, alitumia fursa ya tatizo lake kuwahudumia watu wazima na vijana ambao walikuwa wakikabiliwa na tatizo kama hilo.
Aliamua kuanzisha shirika lisilo la kiserikali nchini Kenya linalojulikana kama Enuresis Innitiative , lengo lake likiwa kuangazia swala hili waziwazi, kwani anasema kuwa watu wengi hasa vijana na watu wazima huwa hawana ukakamavu wa kuzungumiza changamoto kutokana na unyanyapaa uliopo miongoni mwa jamii.
”Kupitia Simulizi la mahangaiko yangu na hali niliyokuwa naishi nayo , nilianza kuwa na moyo wa kusaidia watu wengine. Katika pitapita zangu niligundua kuna wengi wanaoumia hasa wanawake ambao wanaogopa kuingia kwenye ndoa kwa kuhofu shida ya kujiendea haja ndogo wakat iwa usingizi . na kwa kweli nimeweza kuwasikia wengi na kupata mikakati ya jinsi mtu anawezajitoa kwenye hali hiyo ”anasema Lucy
Kifaa cha kudhibiti mkojo
Mojawapo ya pendekezo ambayo Lucy anatoa kwa jamii ni kifaa kinachofahamika kama (bedwet alarm) anaeleza kuwa kifaa hiki kinatumika kote ulimwenguni, na watu ambao wanakabiliwa na tatizo hili.
Kifaa hiki ambacho kina kingo’ra kimetengenezwa hali ya kwamba hutoa sauti na kumuamsha mwathiriwa pindi anapoanza kujikojolea.
Pindi siku zinavyozidi kusonga mbele kifaa hiki kinaendelea kupiga kelele na kumuarifu mwathiriwa kila anapoanza kujikojolea akiwa usingizini.
Lakini je wataalamu wanasema nini kuhusu hali hii?
Hali hii inafahamika kama Enuresis kwa jina la kimatibabu , ni hali ya mtu kukojoa bila kupenda kwake wakati anapolala. Vilevile inaweza kuwa dalili ya matatizo ya udhibiti wa kibofu cha mkojo kama vile kukosa uwezo wa kujizuia au uwezo wake wa kuhimili maji mwilini ni mdogo . Hali hii pia inaweza kusababishwa na tezi dume au saratani ya kibofu
Ushauri kwa waathiriwa
Pendekezo la wataalamu kwa watu wenye changamoto hii ni kwanza mtu adhibiti unywaji wa maji hasa nyakati za jioni , pia wanashauri matumizi ya Kengele au King’ora cha kudhibiti mkojo unaotoka bila mtu kupenda.