Mapigano ya Sudan: Mvutano wa kijeshi ndio chanzo cha mapigano huko Khartoum

Iliyochapishwa

Mapigano ambayo yamezuka katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na kwingineko nchini humo ni matokeo ya moja kwa moja ya mvutano mkali wa madaraka ndani ya uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.

Kuna mapigano katika maeneo muhimu ya kimkakati katika mji mkuu huku wanachama wa kikosi cha kijeshi - Rapid Support Forces (RSF) - na wanajeshi wa kawaida wakipigana.

Balozi wa Marekani nchini Sudan - John Godfrey

Awali, balozi wa Marekani nchini Sudan, John Godfrey, amesema katika ujumbe wa Twitter kwamba kuongezeka kwa mivutano "ndani ya kitengo cha kijeshi" ni "hatari sana" na kutoa wito kwa uongozi wa juu wa pande hizo mbili kusitisha mapigano hayo haraka.

Ujumbe wa Nukuu: " Niliwasili mjini Khartoum usiku wa kuamkia jana na kusikia milio ya risasi na mapigano ya kutisha," amesema kwa John Godfrey balozi wa Marekani nchini Sudan

Aliongeza kuwa yeye na wafanyakazi wa ubalozi walikuwa wanajihifadhi mahali.

Hali ilivyo Khartoum ni tete - Anthony Blinken

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken, amesema hali huko Khartoum ni "tete", kulingana na ripoti za shirika la habari la Reuters.

Blinken, ambaye kwa sasa yuko katika safari yake ya kwanza rasmi nchini Vietnam, amesema kunaweza kuwa na wengine wanaopinga maendeleo ambayo yamepatikana nchini Sudan katika kuunda serikali ya kiraia.

Lakini kipi tunachokijua kufikia sasa?

  • Mapigano yanayoendelea inasemekana ni mzozo wa pande mbili wenye kuhusisha nani atakayechukua udhibiti wa maeneo muhimu ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
  • Kikosi cha Rapid Support Forces paramilitary (RFS) kinasema kimechukua udhibiti wa Ikulu ya rais na uwanja wa ndege wa kimataifa, lakini madai hayo hayajathibitishwa.
  • RSF pia inadai kuwa imekamata wanajeshi wa jeshi la Sudan na kuteka baadhi ya maeneo katika majimbo mengine nchini humo.
  • Kwa upande wake, jeshi linasema bado linadhibiti vituo vyote na viwanja vya ndege.
  • Limeongeza kuwa jeshi la anga linaendesha operesheni ili kukabiliana na kikosi cha RSF.
  • Picha kutoka kwa watangazaji wa ndani zimeonyesha ndege ya kijeshi katika anga ya Khartoum, lakini hii pia haijathibitishwa.
  • Pande hizo mbili pia hazikubaliani juu ya nani aliyeanzisha mzozo huo.
  • Hapo awali, RSF ilishutumu jeshi kwa kuanzisha mapigano hayo kwa kushambulia makao yake makuu mjini Khartoum na kuzingira wanajeshi wa RSF waliokuwa hapo.
  • Lakini jeshi la Sudan lilisema RSF ilianza mapigano kwa kushambulia

Vyama vya kiraia vya Sudan ambavyo vimetia saini makubaliano ya awali ya kugawana madaraka na jeshi na RSF hapo awali vilitoa wito kwa pande zote mbili kusitisha uhasama, Reuters inaripoti.

Pia walitoa wito kimataifa na kikanda kuingia kati na kusaidia haraka kukomesha umwagaji damu.

Historia ya mapigano hayo ni ipi?

Tangu mapinduzi ya Oktoba 2021, Sudan imekuwa ikiendeshwa na baraza la majenerali na kuna wanajeshi wawili katikati mwa mzozo huo.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa majeshi na rais wa nchi hiyo kwa sasa.

Na naibu wake na kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti.

Hawakubaliani na mwelekeo ambao nchi inaenda na hatua inayopendekezwa kuelekea utawala wa kiraia.

Mojawapo ya mambo muhimu ya kuzingatia ni juu ya mipango ya kujumuisha askari 100,000 wa RSF katika jeshi na ambao wangeongoza kikosi kipya.

Kwa nini yote haya yalianza Jumamosi?

Ghasia hizo zinafuatia siku za mvutano huku kikosi cha RSF wakisambazwa tena nchini kote katika hatua ambayo jeshi liliona kama tishio.

Kumekuwa na matumaini kwamba mazungumzo yanaweza kutatua hali hiyo lakini hili halijatokea.

Haijabainika ni nani alifyatua risasi ya kwanza Jumamosi asubuhi lakini kuna hofu kwamba hali hii itazidi kuwa mbaya.

Wanadiplomasia wamezitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano.

Kwa nini jeshi ndio linasimamia nchi?

Mapigano haya ni kipindi cha hivi punde zaidi katika mivutano iliyofuatia kuondolewa madarakani kwa Rais Omar al-Bashir aliyehudumu kwa muda mrefu mwaka wa 2019.

Kulikuwa na maandamano makubwa ya kutaka kusitishwa kwa utawala wake wa karibu miongo mitatu na jeshi lilianzisha mapinduzi ili kumuondoa.

Lakini raia waliendelea kudai nafasi katika mpango wa kuelekea utawala wa kidemokrasia.

Mpango mkakati wa kurejesha mamlaka mikononi mwa raia ulikubaliwa Desemba mwaka jana lakini mazungumzo ya kukamilisha hatua hiyo yameshindwa.

Serikali ya pamoja ya kijeshi na ya kiraia ilianzishwa wakati huo lakini hiyo ilipinduliwa katika mapinduzi mengine mnamo Oktoba 2021.

Na tangu wakati huo ushindani kati ya Jenerali Burhan na Jenerali Dagalo umeongezeka.

Kikosi cha Rapid Support Forces ni kina nani?

Kikosi cha wanajeshi wa Rapid Support Forces (RSF) kimejitokeza kwa kujulikana na sifa mbaya kikiwa katikati ya mzozo huu, ambao ni juu ya kuelekea utawala wa kiraia.

Kikiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo - naibu kiongozi wa nchi - kimekuwa kikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Hii ikiwa ni pamoja na mauaji ya Juni 2019 ya waandamanaji wasiopungua 120 kwenye maandamano ya kukaa ndani katika makao makuu ya Jeshi.

RSF kiliundwa mwaka wa 2013 ikiwa na wapiganaji wengi kutoka kwa wanamgambo wa Janjaweed ambao walipigana kikatili na waasi huko Darfur.

Mnamo mwaka wa 2015, wanachama wake 40,000 walijiunga na muungano wa kijeshi ulioongozwa na Saudi katika vita huko Yemen.

Wapiganaji wa RSF pia wametumwa Libya.

Ili kuwezesha pendekezo la mpito kwa utawala wa kiraia, kulikuwa na mpango wa kuanza kuunganisha RSF katika jeshi.

Lakini mzozo kati ya Jenerali Dagolo na mkuu wa Jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, kuhusu ratiba ya mabadiliko hayo na nani angeongoza kikosi kipya ndio suala ambalo limejitokeza kuwa chanzo cha mzozo.

Mvutano huo ulienea katika mapigano yaliyozuka asubuhi ya leo.

Mzozo huu umefikaje hapa?

Majenerali wamekuwa wakiendesha nchi ya kaskazini-mashariki mwa Afrika ya Sudan kupitia kile kiitwacho Sovereign Council tangu mapinduzi ya Oktoba 2021.

Kikosi cha kijeshi cha Rapid Support Forces (RSF) kiko chini ya uongozi wa makamu wa rais wa baraza hilo, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo. Jeshi, wakati huo huo, linaongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa Baraza Kuu.

Pendekezo la kuhamia serikali inayoongozwa na raia limekiuka ratiba ya kuunganisha RSF katika jeshi la taifa.

Hata hivyo, RSF ilitaka kuchelewesha kwa hatua hiyo kwa miaka 10, lakini jeshi lilisema inapaswa kutokea mara mbili.

Nini kinaweza kutokea sasa?

Ikiwa mapigano yataendelea basi yanaweza kusambaratisha zaidi nchi na kuzidisha machafuko ya kisiasa.

Wanadiplomasia, ambao wamekuwa na jukumu muhimu katika kujaribu kuhimiza kurejea kwa utawala wa kiraia, watakuwa na hamu ya kutafuta njia ya kupata majenerali hao wawili kuzungumza.

Wakati huo huo, watakuwa Wasudan wa kawaida ambao watalazimika kuishi katika kipindi kingine cha kutokuwa na uhakika.