Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Warusi wanaowachunguza na kuwaripoti raia wenzao na wageni kwa mamlaka
Kuwapeleleza, au kuripoti majirani, wenzako na hata raia wa kigeni kwa mamlaka, lilikuwa ni jambo la kawaida katika zama za Urusi chini ya Mujungano wa Usovieti.
Lakini sasa wakati serikali ya Urusi inakabiliana na wakosoaji wa vita vya Ukraine, watu wenye chuki za binafsi na misimamo yao ya kisiasa wanawaripoti wenzao na wageni kwa mamlaka.
"Nilifundishwa jinsi ya kuwapeleleza na kuwaripoti watu wengine na babu yangu ambaye yeye mwenyewe alikuwa akiwapeleleza na kuwaripoti watu kwa mamlaka ," anadai mwanamke anafahamika kwa jina la Anna Korobkova. Anasema anaishi katika mji mkubwa wa Urusi lakini anakataa kusema ni nani.
Lakini anasema babu yake alikuwa mpelelezi asiyejulikana kwa polisi wa siri wa Usovieti wakati wa utawala wa Stalin, wakati kutoa taarifa kuwahusu watu ilikuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku, na anafuata nyayo zake. Sasa, anaripoti mtu yeyote anayedhani ni mkosoaji wa vita nchini Ukraine.
Mpelelezi sugu anayekiri kufanya kazi hiyo
Korobkova anadai kuwa aliandika ripoti kuwahusu watu 1,397 tangu ulipoanza uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Anasema watu wamepigwa faini, kufukuzwa kazi na kutajwa kama mawakala wa kigeni kwa sababu amekuwa akiwaripoti kwa mamlaka.
"Sijihisi kuwahurumia ," anafichua. "Najisikia furaha wanapoadhibiwa kwa sababu ya kuwaripoti kwangu."
Sheria mpya za udhibiti zilianzishwa muda mfupi baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022. Tangu wakati huo, Korobkova ametumia muda wake mwingi mtandaoni, mara nyingi akiwaripoti watu kwa "kudharau jeshi la Urusi" - kosa ambalo ukipatikana nalo unalipa faini ya hadi roubles (pesa za Urus) 50,000 ($ 560; £ 450) au hadi kifungo cha miaka mitano ikiwa umelitenda zaidi ya mara mbili.
Korobkova huwa na makini na mwenye tahadhari sana anapozungumza na mimi na huzungumza nami kupitia barua pepe. Hataki kuonyesha uso wake na hakubali kutoa ushahidi wa utambulisho wake. Anasema hii ni kwa sababu mara nyingi anapokea vitisho vya kuuawa na anahofia taarifa zake zinaweza kudukuliwa au kuibiwa.
Anaonekana kuchochewa na sababu mbili za kuwaripoti raia wenzake. Kwanza, ananiambia anaamini anaisaidia Urusi kuishinda Ukraine na, pili, anafikiri itasaidia kumpatia fedha za kudumu.
Anaishi peke yake na anafanya kazi kwa muda kama profesa wa masuala ya kibinadamu, akitegemea sana akiba yake. Lakini Korobkova anahofia kuwa Urusi inaweza kuishia kulipa fidia ikiwa Ukraine itazishinda katika mzozo huo na hilo linaweza kuathiri fedha za nchi nzima na kila mtu anayeishi huko.
"Wale wote wanaopinga operesheni maalum ya kijeshi ni wapinzani wa ustawi wangu mwenyewe," anaelezea, akitabiri ushindi kwa Ukraine utakuwa hasara kwake. "Ningeweza kupoteza akiba yangu yote na ningehitaji kupata kazi ya wakati wote."
Tangu sheria mpya za udhibiti zianzishwe, zaidi ya kesi 8,000 zimefunguliwa dhidi ya watu kwa kulidhalilisha jeshi, kwa mujibu wa shirika huru la haki za binadamu la Urusi OVD-Info.
Malengo
Korobkova anaripoti zaidi watu wanaozungumza na vyombo vya habari, hasa wale wanaoonekana kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, kama vile BBC. Moja ya malengo ya Korobkova ni daktari wa mifupa Aleksandra Arkhipova.
"Ameniripoti mara saba," Arkhipova anasema. "Kuandika kuhusu jinsi ya kumripoti mtu ni njia yake ya kuwasiliana na mamlaka. Anaiona kuwa ni kazi yake.
"Amepata ajira yake. Kuwaripoti wataalamu kkumeweza kuwanyamazisha kabisa," anaongeza Arkhipova, ambaye sasa yuko uhamishoni na anadhani vitendo vya Korobkova vinaweza kumsababishia kuitwa wakala wa kigeni na serikali ya Urusi mwezi Mei.
"Marafiki zangu, ambao aliwashutumu, sasa wanakataa kutoa maoni yoyote kwa vyombo vya habari. Kwa hiyo, unaweza kusema kuwa amefanikiwa. Ujumbe umekamilika."
Mlengwa mwingine alikuwa mwalimu wa Moscow aitwaye Tatiana Chervenko.
Wakati Urusi ilipoanzisha madarasa ya uzalendo mnamo Septemba 2022, Chervenko aliamua kufundisha hesabu badala yake, aliiambia TV Rain, kituo cha mwisho cha kujitegemea cha Urusi, ambacho kilifungwa na serikali na sasa kiko Uholanzi.
Matokeo yake, Korobkova, ambaye aliona mahojiano yake ya televisheni, alianza kutoa shutuma dhidi ya Chervenko, akilalamika kwa mwajiri wake, wizara ya elimu ya Moscow na kamishna wa haki za watoto wa Urusi.
Chervenko baadaye alifutwa kazi mnamo Desemba 2022.
Korobkova haonekani kujutia matendo yake, badala yake anajivunia kuweka hifadhidata ya watu aliowaripoti, pamoja na matokeo.
Anadai kuwa baada ya kuachishwa kazi watu sita walifukuzwa kazi na wengine 15 walitoa mashtaka ya kiutawala na kutozwa faini.
Ingawa Korobkova anasisitiza kuwa anawalenga watu anaowaamini ni maadui wa serikali, watu wengine wameiambia BBC kuwa denunciations pia zinatumiwa nchini Urusi kutatua uhasama wa kibinafsi.
Kufungwa jela na kutamani uhuru
Mvuvi Yaroslav Levchenko kutoka Peninsula ya Kamchatka, katika mashariki ya mbali ya Urusi, inayojulikana sio tu kwa mandhari yake ya volkano na wanyamapori wa ajabu lakini pia kwa uwepo wake mkubwa wa kijeshi. Watu wengi katika eneo hili ni wanaomuunga mkono -Putin ikiwa ni pamoja na wenzake Levchenko.
Mnamo Februari 2023, meli ya Levchenko ilitia nanga katika bandari ya Kamchatka baada ya safari ya uvuvi ya mwezi mmoja. Anasema mvuvi mwenzake alimpa kinywaji cha pombe, ambacho alikataa. Anaamini mtu mwingine tayari alikuwa na chuki dhidi yake na waliishia katika hoja. Levchenko anaeleza kuwa alipigwa kichwani kwa chupa na baadaye akaamka akiwa hospitalini.
Levchenko anasema alipoachiliwa na kwenda kituo cha polisi kutoa ripoti, alishangaa kujua kuwa yeye ndiye aliyeripotiwa - sio kwa ajili ya kushambuliwa bali kwa kuwa na maoni ya kupinga vita. Alidai polisi walimwambia kuwa hakuna ushahidi wa kutosha wa kumfungulia mashtaka ya jinai mwenzake.
Levchenko alikamatwa tarehe 13 mwezi Julai. Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizoshuhudiwa na BBC, anatuhumiwa kuhalalisha ugaidi, mashtaka anayoyakanusha, na anazuiliwa gerezani wakati akisubiri kesi.
Njia pekee ambayo anaweza kuielezea BBC ni kupitia barua, alizopitia wakili wake.
Marafiki wa Levchenko wananiambia wanafikiri kitendo chake cha kuwaripoti watu kililenga kugeuza umakini wa polisi mbali na kushambuliwa na ukweli kwamba pombe ilikuwa ikitumiwa kwenye meli, jambo ambalo lilikuwa ni marufuku.
"Nataka kurudi nyumbani," Levchenko alisema. "Naweza kuona tu anga kutoka kwenye mahabusu yangu ya jela, kupitia safu kadhaa za baa, na haiwezi kuvumilika," anaandika katika barua kwa rafiki yake ilisambazwa na BBC.
'Mashitaka yasiyo na mwisho'
Polisi wa Urusi wamekiri kuwa wamekumbwa na shutuma tangu vita hivyo vilipoanza. Maafisa ambao hawakutambuliwa wameiambia BBC kuwa wanatumia muda mwingi kuchunguza na kurekebisha "mashitaka yasiyo na mwisho juu ya kudharau jeshi".
"Watu daima wanatafuta kisingizio cha kumshutumu mtu kuhusiana na 'operesheni maalum ya kijeshi'," afisa wa polisi mstaafu hivi karibuni aliiambia BBC, na kuongeza kuwa: "Kila kitu halisi kinapojitokeza, hakuna mtu wa kuchunguza''.
Huku miito ya mara kwa mara ya Rais Putin ya "kuwaadhibu wasaliti" na mwisho wa vita nchini Ukraine bila kuonekana, wapelelezi wanaofanya kazi hiyo kila wakati kama Korobkova hawaonyeshi dalili za kuacha yabia ya kuwaripoti kwa mamlaka raia wenzao.
"Nitaendelea kuwapeleleza na kuwaripoti watu ," anaandika katika barua pepe kwa BBC, akiongeza: "Nina kazi nyingi za kufanya."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi