Mpango wa matumizi ya dawa za VVU unakiuka uhuru wa kidini, hakimu asema

Dawa ya dharura ya (PrEP) inaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa VVU kwa 99% inapotumiwa kama ilivyoagizwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dawa ya dharura ya (PrEP) inaweza kupunguza hatari ya kuambukizwa VVU kwa 99% inapotumiwa kama ilivyoagizwa
Iliyochapishwa

Mipango ya afya ya Marekani ambayo inajumuisha dawa ya kuzuia virusi vya ukimwi (VVU) inayojulikana kama (PrEP)  katika bima inakiuka haki ya uhuru wa kidini, jaji ameamua.

Waajiri wanatakiwa kulipia huduma fulani za kinga na dawa katika bima zao chini ya sheria za Marekani.  

Lakini kundi la Wakristo wa Texas lilishtaki mwaka wa 2020 juu ya dawa za kuzuia kuambukizwa VVU (PrEP).

Walisema kuwa dawa hiyo inaweza ‘’kuchochea tabia ya mapenzi ya jinsia moja’’.

PrEP inapendekezwa kwa watu wazima walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU.

Inaweza kupunguza hatari ya kupata maambukizi kwa hadi 99% inapotumiwa kama ilivyoagizwa, kulingana na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.

Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa (CDC) kimetaja kuongezeka kwa matumizi ya dawa hiyo kama sababu muhimu katika kupunguza maambukizi ya VVU.

Dawa hiyo inayotumiwa kwa kunywa imetumiwa na zaidi ya watu 600,000 katika nchi 76, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Walalamishi huko Texas walisema kuwa mfumo ambao serikali kuu huamua ni huduma zipi za uzuiaji zinazopaswa kulipwa na mwajiri  katika mipango ya bima ni kinyume cha sheria.

Kesi iliyowasilishwa na wakili Jonathan Mitchell anayeishi Austin - ambaye anasifiwa kwa kupanga utekelezaji wa marufuku ya utoaji mimba ya wiki sita nchini humo - inawaleta pamoja wafanyabiashara na waajiri wanaojiita Wakristo.

Mshitaki mmoja katika kesi hiyo, Dk Steven Hotze, alidai kuwa kulipia dawa za PrEP katika bima ya wafanyakazi wake itakuwa kinyume na ‘’imani zake za kweli za kidini’’.

Daktari huyo, ambaye ni mfadhili mkubwa wa chama cha Republican alidai dawa za kawaida ambazo zinanunuliwa dukani zinaweza ‘’kuchochea tabia ya mapenzi ya jinsia moja’’.

Waliowasilisha malalamishi pia waliandika kwamba ‘’hawahitaji au kutaka’’ kugharamia dawa hiyo katika mipango ya bima ‘’kwa sababu wako katika uhusiano wa mke mmoja na wenzi wao’’ na ‘’kwa sababu wao au wanafamilia wao hawashiriki katika tabia inayoendeleza maambukiza ya VVU’’.

Takwimu za CDC zinaonyesha kuwa karibu kesi moja kati ya watano wapya wa VVU nchini Marekani sasa ni miongoni mwa wanawake, huku wengi wao wakiwa na mahusiano na watu wa jinsia tofauti.

Lakini Jaji wa Wilaya ya Reed O'Connor alitoa uamuzi Jumatano kwamba, serikali haiwezi kuhitaji ‘’mashirika ya kibinafsi, ya kidini’’ kugharamia dawa hiyo ‘’bila kugawana gharama na bila kusamehewa sheria fulani kwa misingi ya kidini’’.

Aliandika kuwa PrEP inakiuka haswa haki za kikatiba za walalamikaji chini ya Sheria ya Marejesho ya Uhuru wa Kidini.

RFRA hutumiwa mara kwa mara katika kesi za upatikanaji huduma za uavyaji mimba na huduma ya kuthibitisha jinsia kwa watu waliobadili jinsia.

Wataalamu wa matibabu hapo awali walikuwa wamekashifu kesi hiyo kama tishio kwa mfumo mzima wa utoaji huduma za kinga.

Jumuiya ya Madaktari ya Marekani na muungano wa mashirika 60 ya matibabu waliandika mnamo Julai kwamba uamuzi mmoja mbaya unaweza kumaanisha ‘’wagonjwa watapoteza uwezo wa ufikiaji wa huduma muhimu za afya ya kinga, kama vile uchunguzi wa saratani ya matiti, saratani ya utumbo mpana, saratani ya shingo ya kizazi, ugonjwa wa moyo, unene na kisukari’’.

Serikali kuu inatarajiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Jumatano.