Je, makampuni ya teknolojia yanaweza kuendesha nchi vizuri kuliko serikali?

fdc

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Gabriel Gatehouse
    • Nafasi, BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Balaji Srinivasan ni mfanyabiashara na mwekezaji katika uwanja wa teknolojia ya sarafu ya mtandaoni, anaamini teknolojia inaweza kufanya karibu kazi zote ambazo serikali zinawajibika kuzifanya.

Firikia mazingira ambayo unaweza kuchagua uraia wako – hiyo ndio picha ya miji ijayo ambayo Balaji anawaza kichwani mwake. Anaamini kwa vile tunaweza kuunda kampuni kama Facebook na Google na pesa ya mtandaoni, pia tunaweza kuunda nchi.

Katika mkutano mkubwa wa teknolojia huoko Amsterdam, nilimuona Balaji akielezea mawazo yake hayo kwa hadhira.

Jinsi zinavyofanya kazi nchi hizi: Kwanza, unakuwa na jumuiya ya mtandaoni ambayo ina maslahi au maadili yanayofanana. Kisha wanapata ardhi na kuwa "nchi" na sheria zao wenyewe. Nchi hizi zitakuwepo pamoja na nchi zilizopo na hatimaye kuzibadilisha.

Vuguvugu la uwepo wa nchi za namna hii linazidi kupata nguvu. Watu hawa hawataki tu serikali zilizopo zibadilike ili makampuni yaendeshe mambo yao; wanataka kubadilisha serikali na mashirika.

Wengine wanaona wazo la nchi hizi ni kama mradi wa ukoloni mamboleo ambao utachukua nafasi ya viongozi waliochaguliwa. Lakini wengine wanaamini wazo hilo ni njia ya kuondokana na hali ya sasa ya demokrasia ya Magharibi, ambayo wanaona kuwa imejengwa kwa kanuni nyingi.

Baadhi ya Jumuiya Hizi

sd

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mjasiriamali wa teknolojia Balaji Srinivasan

Katika Mkutano wa Amsterdam wa Tech Entrepreneurs, baadhi ya hizi "jumuiya za wanaoanzisha" zilionyeshwa. Moja inaitwa "Cabin," "mji wa mtandaoni wenye matawi huko Marekani, Ureno, na kwingineko. Nyingine ni CoolDosk, jumuiya yenye makao yake Arizona iliyoundwa kwa ajili ya kufanya kazi mtandaoni.

CoolDosk na Cabin ni kama jumuiya za mtandaoni. Lakini jumuiya ya "Prospera" ni tofauti. Iko kwenye kisiwa karibu na pwani ya Honduras, kwenye "mji binafsi" unaohudumia wajasiriamali. Huko, kuna sayansi ya kuongeza maisha na tiba ya majaribio ya jeni ili kupunguza kasi ta kuzeeka.

Prospera inaendeshwa na kampuni iliyoko katika jimbo la Marekani la Delaware, na wakati wa serikali iliyopita Honduras, kampuni hiyo uliweza kupata nafasi kuunda sheria zake.

Lakini Xiomara Castro, rais wa sasa wa Honduras, anataka kusitisha shughuli za kampuni hiyo na ameanza kubatilisha baadhi ya ruhusa ambazo hapo awali ilipewa kampuni hiyo.

Lakini Prospera inaishtaki serikali ya Honduras ili kuzuia hilo.

Nchi ya Praxis

fdc

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wakati wa mkutano wa Amsterdam, mtaalamu mwingine aliyepanda jukwaani ni Dryden Brown, anasema anataka mji mpya kwenye mwambao wa Mediterania.

Mji huo hautaendeshwa na urasimu wa serikali, utaendeshwa kwa teknolojia ya sarafu za mtandaoni. Aliuwita mji huo "Praxis" neno kutoka Kigiriki lenye maana ya "pragmatism."

Brown anasema raia wa kwanza wa taifa hilo jipya wataanza kuhamia mapema 2026. Lakini maelezo ya mpango wake yalikuwa na maswali: Nani atajenga miundombinu? Nani ataiendesha?

Kwa sasa, "Jumuiya ya Praxis" inapatikana zaidi mtandaoni. Kuna tovuti ambapo unaweza kutuma maombi ya uraia. Lakini wananchi hawa ni akina nani hasa? Hilo haliko wazi.

Baada ya hotuba ya Brown katika ukumbi wa mikutano nje kidogo ya Amsterdam, nilikwend kumuona. Alikuwa na tabia ya kushuku, lakini alinipa nambari yake ya simu. Nilimtumia ujumbe na kujaribu kuzungumza naye, lakini sikufanikiwa.

Takriban miezi sita baadaye, niliona habari kwenye X. "Uzinduzi wa jarida la Praxis." Hakuna wakati au mahali pametangazwa itafanyika hafla hiyo ya uzinduzi. Kulikuwa na kiungo kimoja (linki) ambacho unaweza kutuma ombi la kushiriki.

Nilituma maombi, lakini sikupata jibu. Asubuhi iliyofuata nilimtumia tena ujumbe Dryden Brown. Na kinyume na matarajio yangu, alijibu: "Ella Fant, saa 04 usiku."

"Ella Fant" ni jina la baa na kilabu huko Manhattan. Mahali hapo hapo awali palijulikana kama Club 82 na palikuwa moja ya eneo maarufu kwa watu wa mapenzi ya jinsia moja.

Sasa hapa ndio kuna sherehe maalum kwa watu wanaotaka kuanzisha nchi mpya. Na kwa namna fulani nilipata mwaliko, lakini tatizo lilikuwa - niko umbali wa maili 2,000 huko Utah. Ikiwa nataka kufika kwa wakati, nalazimika kupanda ndege mara moja.

Kwa kweli, nilikuwa mmoja wa watu wa kwanza kufika. Wafanyakazi wachache wa Praxis walikuwa wakileta nakala za jarida hilo katika baa. Nilichukua nakala na kupekua. Lina karatasi ya gharama, nzito yenye matangazo mengi ya bidhaa mbalimbali, kama vile manukato, bunduki.

Jarida hilo linawahimiza wasomaji kutoa nakala nyingine na kuzieneza katika jiji. Mashine ya kunakili iliwekwa hapo mahsusi utekelezaji wa hilo.

Niliingia baa na kujipatia kinywaji. Kisha nilianza kuzungumza na wanawake wawili vijana ambao hawakuonekana kuwa sehemu ya jumuiya hiyo.

Ezra ni meneja wa klabu na rafiki yake Dylan ambaye ni mwanafunzi. Nao kumbe walikuwa na maswali yao. Dylan aliuliza, “itakuwaje kama hakuna wafanyakazi wa kutosha shuleni au hospitalini katika nchi hiyo?

Na Ezra akasema, wazo hili linaonekana kama la ajabu. “Lakini tulitaka kuona kile kinachotokea katika mkutano mwenyewe wa jumuiya hii," alitania.

Kisha nilikutana na Dryden Brown, mwanzilishi wa Praxis. Alikuwa anakwenda nje kuvuta sigara, nami nikamfuata. Jarida la Praxis, aliniambia, ni njia ya kuonyesha utamaduni mpya anaotarajia kuunda.

Nilitaka kumuuliza maswali kuhusu mradi wa nchi yake: Ni nani watakuwa raia wa nchi hii mpya? Nani ataiendesha? Na swali la nani atafanya kufanya katika hospitali?

Lakini kuwasili kwa wageni wapya kulikatisha mazungumzo yetu. Dryden Brown alinialika kutembelea Ubalozi wa Praxis kesho. Tukaagana na kurudi ndani ya baa. Kisha nilichukua nakala ya gazeti na kuondoka.

Niliketi kwenye chumba kidogo nilichokodi juu ya duka kubwa la Wachina na kupekua gazeti. Pamoja na matangazo kulikuwa na kodi ya QR.

Ni kiungo cha filamu fupi, ilani ya dakika 20 dhidi ya upuuzi wa maisha ya kisasa, na ubora wa ulimwengu mwingine wa vyeo na ushujaa.

Msimulizi anasema: “Vyombo vya habari vya kisasa vinadai kuwa na maadili yoyote ni ufashisti. Kitu chochote kinachotokana na imani kali ni ufashisti."

Harakati hii inaonekana kutafuta ufahamu juu ya utamaduni wa Magharibi; Ulimwengu wa Nietzschean ambapo watu imara husalia baada ya machafuko na vurugu.

Ubalozi wa Praxis

Siku iliyofuata nilitembelea Ubalozi wa Praxis, huko Broadway. Kwa kweli kuna nakala nyingi za vitabu vya Nietzsche, wasifu wa Napoleon, na kitabu chenye kichwa cha habari "The Dictator's Manual." Nilitumia muda mwingi huko, lakini hakukuwa na dalili ya Dryden Brown kutokea.

Niliondoka nikiwa bado sina uhakika ni nini hasa nilichoshuhudia jana usiku; ni maono ya siku za usoni ambapo nchi kama Amerika na Uingereza zitaanguka?

Au Dryden Brown na marafiki zake ni kikundi cha "marafiki wa teknolojia" wakijifanya wanamapinduzi wa siasa kali za mrengo wa kulia ili kudhihaki wengine na kufurahia tafrija?

Je, Dryden Brown siku moja atakuwa CEO au mfalme wa utawala wa mrengo wa kulia katika Bahari ya Mediterania?

Nina mashaka juu ya hilo. Lakini juhudi zinaendelea kuanzisha maeneo yanayojitegemea, bandari huria na miji ya kukodisha. Na ikiwa demokrasia iko hatarini, inaonekana harakati za nchi za aina hiyo, zinasubiria kuchukua nafasi.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Seif Abdalla