Putin adai mashambulizi ya Ukraine ya kujibu mapigo yameshindwa

Iliyochapishwa

Rais wa Urusi Vladimir Putin amedai mashambulizi ya kurudisha mapigo ya Ukraine yameshindwa, na vikosi vyake vimepata hasara kubwa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa vita, hasara iliyopata Kyvi inakaribia kufika kiwango cha janga. Madai hayo bado hayaja thibitishwa.

Rais wa Ukraine amekanusha mashambulizi yake kufeli. “Tunasonga mbele,” amesema katika hutuba yake ya usiku kupitia video.

Amevishukuru vikosi vya Ukraine kwa kila hatua na kila mita ya ardhi ya Ukraine wanayoikomboa kutoka katika uovu wa Urusi.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Kamanda Mkuu wa vikosi vya Ukraine, Valery Zaluzhny, aliandika kupitia mtandao wa Telegram, “kuna mafanikio, tunatekeleza mipango yetu na kusonga mbele.”

Mashambulizi ya Kyiv yako katika hatua za awali, yamekomboa eneo dogo la ardhi mashariki mwa Donetsk and kusini-mashariki mwa mikoa ya Zaporizhzhia. Bwana Zelensky pia amedai wamesonga mbele huko Bakhmut.

Lakini mambo hayako wazi kuhusu madai ya Kyvi ya kukomboa maeneo mwanzoni mwa wiki hii.

Siku ya Jumanne, BBC ilipewa ruhusa ya kufika katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Donetsk ambako bendera ya Ukraine inapepea kwa sasa. Maeneo mengi yamehamwa, na katika baadhi ya maeneo vikosi vya Urusi vinajibu mapigo.

Mkuu wa Nato, Jens Stoltenberg alisema, bado ni mapema ila hatua imepigwa kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi.

“Kile ambacho tunakijua, kadiri Ukraine inavyoweza kukomboa ardhi ndivyo inavyozidi kuwa na nafasi nzuri katika meza ya mazungumzo,” alimwambia rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano wa Ikulu.

Bila ya kutoa ushahidi, bwana Putin alisema, Ukraine imepoteza vifaru 160 na Urusi vifaru 54. Pia, alidai hasara ya Ukraine ni mara kumi zaidi ya ile ya Urusi. Na kusisitiza Kyiv haijafanikiwa kwa lolote.

Kauli yake imepingwa na afisa wa Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa, ameliambia shirika la habari la AP, anatahadharisha dhidi ya kuipa uzito tathmini ya Moscow kwani sio sahihi.

Ingawa kauli nyingi za Rais Putin katika mkutano wake na waandishi wa habari wa vita, zilikuwa zinajikanganya. Amekiri Moscow ingeweza kutabiri vizuri zaidi mashambulizi ya hivi karibuni yaliyovuka mpaka kuingia Urusi kutoka Ukraine.

Ukraine imekuwa na wasiwasi wa muda mrefu juu ya uwezo wa Urusi kutengeneza silaha.

Siku ya Jumanne, bwana Zelensky alitoa wito wa vikwazo vikali zaidi kwa Urusi ili kuzuia vifaa vya kutengenezea silaha, ambavyo baadhi vinatengenezwa na nchi washirika wa Ukraine.

Alisema, Urusi imekuwa ikitumia vifaa hivyo kutengeneza makombora ambayo siku ya Jumanne yalipiga makazi ya raia na ghala huko Kryvyi Rih, na kuuwa watu 11 na kujeruhi makumi.

Siku hiyo hiyo, Marekani ilitangaza itatuma msaada mpya wa kijeshi wa thamani ya dola milioni 325.

Kwa upande mwingine, kiongozi wa Belarusi, Alexander Lukashenko amesema nchi yake itapokea silaha za nyuklia kutoka Urusi ambazo zina nguvu mara tatu ya bomu la atomiki ya Hiroshima na Nagasaki.

Hakusema ikiwa wameshapokea silaha hizo au bado, lakini alidai kuletwa kwake ni muhimu kwa Minsk ili kuzuia uwezekano wa uchokozi.

Mwanzo wa mwezi huu, Urusi ilisema itapeleka silaha za kimkakati za nyuklia katika ardhi ya Belarusi kuanzia mwezi Julai, hilo likionekana ni onyo kwa Magharibi, ambayo imeongeza uungaji mkono wa kijeshi kwa Ukraine.