Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamume wa Marekani aliyeibwa akiwa mtoto na kumpata mama yake mzazi nchini Chile miaka 42 baadaye
- Author, Leire Ventas
- Nafasi, BBC World Service
- Iliyochapishwa
Ilikuwa hadi tarehe 22 Agosti mwaka huu ambapo Jimmy Lippert Thyden, wakili kutoka Ashburn katika jimbo la Virginia la Marekani, hatimaye aliweza kumkumbatia mama yake mzazi Maria Angelica Gonzalez, huko Valdivia kusini mwa Chile.
Ingawa ni mama na mwana, hii ilikuwa mara ya kwanza kuonana ana kwa ana, waliweza kukumbatiana, na kusema "nakupenda".
Miongo minne mapema, mnamo Oktoba 1980, wakati Gonzalez alipojifungua mtoto wake wa kiume katika Hospitali ya Salvador huko Santiago, mji mkuu wa Chile, walikuwa wamemwambia kwamba angelazimika kukaa kwenye kifaa maalum chga watoto wachanga ambao wahawajafikisha muda wa kuzaliwa yaani incubator kwani alikuwa amezaliwa kabla ya wakati wake.
Aliporudi kumchukua, walimweleza kuwa amefariki, na alipoomba kuuona mwili huo, walimwambia kuwa “wameutupa mwili huo”.
Lakini kwa kweli, alikuwa ametolewa kwa ajili ya kuasiliwa na wanandoa kutoka Marekani.
Alikuwa "mtoto aliyeibwa", kama wengine wengi wakati wa utawala wa Jenerali Augusto Pinochet (1973-1990).
Kidokezo
"Nililelewa nikijua kuwa nimeasiliwa. Wazazi wangu hawakuwahi kuninyima hilo na nilikulia katika nyumba iliyo wazi na yenye upendo,” Lippert-Thyden aliambia BBC kupitia Zoom kutoka Chile jioni kabla ya kurejea Marekani.
“Kile ambacho sikujua, wala wazazi wangu walezi hawakujua ni kwamba ulikuwa ulezi wa uwongo na bandia,” aliongeza kusema “Niliamini kwamba mama yangu ameniacha kwa sababu alitaka nipate fursa nyingi zaidi na maisha bora. Ndiyo maana niliifikiria kama hadithi ya kuasili yenye mwisho mwema."
Ingawa anakiri kwamba kulikuwa na kitu ambacho hakikufaa kabisa.
Wakati fulani, mama yake mlezi - ambaye bado anamwita "mama", huku akimtaja mama yake mzazi kama "mama" - alikuwa amemuonyesha karatasi za kuasili.
"Na kulikuwa na matoleo matatu: moja ilisema kwamba hakurudi hospitalini, nyingine kwamba alinipa kwa hiari miaka miwili baada ya kujifungua, na ya tatu, kwamba alikufa wakati wa kujifungua."
Huku mbegu ya mashaka ikiwa tayari imepandwa akilini mwake, aliendelea na maisha yake huku akidhani ili kulitatua ni lazima ajiwekee akiba na kwenda katika nchi yake ya asili, hadi Aprili mwaka huu aliposoma kwenye magazeti kuhusu kesi hiyo ya Mmarekani ambaye alikuwa ameasiliwa kinyume cha sheria nchini Chile.
“Nilielewa kwamba huo ndio ukweli pekee ambao ungeweza kueleza uwongo huo,” anakumbuka. "Na pia niligundua kuwa kulikuwa na shirika lililo tayari ambalo linaweza kunisaidia katika uchunguzi wa nyanjani.
Msako
Jambo lililofuata lilikuwa kuwasiliana na taasisi hiyo, Nos Buscamos, ambayo katika miaka ya hivi karibuni imeratibu zaidi ya mikutano 450 kati ya wale ambao walikuwa wahasiriwa wa kuasiliwa haramu na familia zao za kibaolojia za Chile.
Lakini jumla ya idadi ya watoto ambao walichukuliwa kutoka kwa wazazi wao nchini Chile katika miaka ya 1970 na 1980 inakadiriwa kufikia makumi kwa maelfu.
Ilikuwa ni sehemu ya ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu ambao ulifanyika wakati wa miaka 17 ya utawala wa Jenerali Augusto Pinochet, ambaye tarehe 11 Septemba 1973 aliongoza mapinduzi ya kupindua serikali ya kidemokrasia ya Salvador Allende.
"Vurugu zilianza na ukandamizaji na kutoweka kwa watu upande wa upande wa mrengo wa kushoto na upinzani, na kisha ukachukua aina tofauti," Danny Monsalvez, profesa wa Historia na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Concepción, aliiambia BBC mnamo 2021.
Katika muktadha huo, wizi wa watoto wachanga ulikuwa "sehemu ya sera", mtaalamu wa serikali ya kijeshi ya Pinochet alisema wakati huo.
"Hazikuwa kesi za pekee na mchakato wa kuasili ulihusisha taasisi za serikali, kama vile Sajili ya Kiraia."
Watoto waliishia katika nchi kote Uropa, au Marekani, kama Lippert-Thyden.
"Walichukuliwa kutoka kwa familia maskini, kutoka kwa wanawake maskini ambao hawakujua na hawakuwa na njia ya kujitetea," mwanzilishi na mkurugenzi wa Nos Somos, Constanza Del Río, anaiambia BBC.
"Na kwa upande wa Jimmy, kidokezo pekee tulichokuwa nacho (kujaribu kuwatafuta jamaa zake wa kumzaa) ni jina ambalo lilionekana kwenye nyaraka zake, Maria Gonzalez, na haikuwa ya kutia moyo sana, kwa sababu ni jina la wanawake wengi nchini Chile.”
Kwa hivyo, wakati walipata vyeti halisi vya kuzaliwa vya Lippert-Thyden, yeye, kwa kufuata itifaki za shirika, alifanyiwa kipimo cha DNA.
Nos Buscamos imehusishwa na jukwaa la nasaba la MyHeritage kwa miaka miwili, ambalo hutoa vifaa vya bure vya kusambaza kwa watoto wa Chile na wahasiriwa wanaodaiwa wa ulanguzi wa watoto nchini.
Vipimo vya nyumbani vilithibitisha kwamba alikuwa raia wa Chile 100% na vilimhusisha na binamu ambaye pia anatumia jukwaa hilo
Pia aliibuka kuwa na jamaa anayeitwa Maria Angelica Gonzalez na kuwasaidia kupata mawasiliano.
'Mama, ni mimi, mtoto wako'
Njia ya kwanza ilitolewa na Del Rio. Kisha akaiacha mikononi mwa Lippert-Thyden.
“Kwa hiyo nilimtumia tu ujumbe [kwa Kihispania] na kutuma picha yangu: ‘Mama, ni mimi, mtoto wako,’” asema. Kisha akaambatanisha picha zingine - "Huyu ni mke wangu, wajukuu zako wawili."
Akamwambia asiwe na haraka ya kujibu. "Chukua wakati wote unaohitaji," aliongeza, tena kwa Kihispania.
Hiyo ilifuatiwa na masaa na masaa ya kubadilishana ujumbe, kulingana na Lippert Thyden, na kukiri kwake kwamba alimlilia usiku mzima, ingawa hakuwahi kumwambia mtu yeyote kwamba alikuwa naye.
Wiki chache baadaye ulikuwa wakati wa kuonana kupitia mkutano wa video. Kufikia wakati huo, uchunguzi wa DNA uliofanywa kwa Gonzalez ulikuwa tayari umethibitisha uhusiano kati ya wawili hao.
"Nilikuwa nimeenda nyumbani kwa mama yangu kuona jinsi walivyokuwa wakihisi, kwa sababu walikuwa wakifuata utaratibu pamoja nami na ilikuwa vigumu kwa kila mtu," Lippert Thyden anakumbuka, simu hiyo ya video ilipowasili kupitia WhatsApp.
"Tulipoonana, hakukuwa na shaka. Niliwatambulisha na ilikuwa wakati wa neema kama hiyo…,” anasema. “Nakushukuru kwa kumlea, kumtunza, na kumpenda,” mama yake mzazi alimwambia mama yake mlezi, naye mama yake mlezi akajibu hivi: “Asante kwa kushiriki naye pamoja nasi.”
BBC ilijaribu kuzungumza na akina mama wote wawili, lakini jibu lilikuwa kwamba bado hawajawa tayari.
Kulingana na Lippert Thyden, wazazi wake waliomlea pia walikuwa wahasiriwa wa mtandao huu.
"Wazazi wangu walitaka familia, lakini hawakutaka iwe hivyo," aliambia BBC. "Si kwa unyang'anyi, kwa wizi."
Uasili haramu nchini Chile
- Mapema mwaka wa 2018, uchunguzi ulianza katika karibu kesi 500 za kuasili watoto kinyume cha sheria ambazo zilifanyika kati ya 1970 na 1990.
- Kufikia mwisho wa mwaka huo, Mahakama ya Rufaa ya Chile ilikuwa tayari imekadiria kwamba karibu watoto 7,500 walioasiliwa wakati huo huenda walikuwa kinyume cha sheria.
- Mnamo Septemba 2018, baada ya shinikizo kutoka kwa vikundi mbali mbali, baraza la chini la Bunge la Chile liliunda tume ya kuchunguza tuhuma nyingi.
- Mnamo Julai 2019, tume hiyo maalum ilichapisha ripoti ya kurasa 144 ambayo inazungumza juu ya kesi 20,000 za watoto wa Chile ambao waliasiliwa na wanandoa wa kigeni wakati wa serikali ya Augusto Pinochet.
- Kwa kawaida akina mama walidanganywa na kuambiwa kwamba watoto wao wamekufa.
- Katika baadhi ya matukio, kulikuwa na uungwaji mkono kutoka kwa majaji, mamlaka ya uhamiaji, notary, watu wa dini na taasisi za serikali, kulingana na ripoti hiyo hiyo.
- Wengi wa watoto waliishia Sweden, Italia, Marekani, Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani.
'Hilo si jina langu'
"Ni kweli, Jimmy alifika Marekani akiwa amemkubali, lakini aliondoka Chile akiibiwa, akiwa na pasipoti na jina ambalo wafanyabiashara hao walikuwa wamempa," Del Río anasisitiza.
Bado ana hati hiyo yenye kifuniko chekundu na herufi za dhahabu.
Inajumuisha picha ya mvulana, amevaa shati .
Tarehe ya kuzaliwa: 31 Oktoba 1980. Jina: Carlos Dionne Burbach.
"Nataka kuweka wazi kuwa hilo si jina langu," anasema Lippert Thyden.
“Mimi ni Jimmy Lippert Thyden. Nililelewa katika nyumba yenye upendo, katika familia, na walinipa jina hilo,” anabainisha.
"Ingawa mimi pia ni mtoto wa Maria Angelica Gonzalez, na hadhi pekee ninayoweza kumpa katika maisha haya ni kujumuisha jina lake la mwisho karibu na langu," anaendelea.
Ndiyo maana anataka kubadilisha jina lake kuwa Jimmy Lippert Thyden Gonzalez. "Na nikishapata, ninapanga kufanya kazi na wanasheria nchini Chile kuunda utambulisho huo, ili utambulike kama utambulisho wangu wa Chile."
Itakuwa njia ya kusuluhisha swali: "mimi ni nani?", Ambayo imekuwa ikimsumbua kwa miongo kadhaa.
"Ingawa nilikuwa na maisha ya utotoni yenye furaha, nikiwa mtoto wa kuletwa kulikuwa na awamu ngumu, na maisha yangu yote nilikuwa kahawia sana kuwa mweupe, mweupe sana kuwa kahawia. Sikuhisi kwamba nilifaa mahali popote na sikuzote nilijua kwamba kuna kitu kilikosekana,” aeleza.
"Sikuwahi kuhisi kuwa Mmarekani kabisa, hata baada ya kutumikia kwa miaka 19 katika Jeshi la Wanamaji," anaendelea kusema. "Sikuzote nilihisi kuwa Mmarekani wa Chile.
Ziara ya Chile
Ili kuendelea kuchunguza upande wake wa Chile, wiki iliyopita alisafiri na mkewe Johanna na binti zao wawili, Ebba Joy, 8, na Betty Grace, 5, hadi nchi alikozaliwa.
Huko alianza kugundua tabia alizo nazo na mama yake mzazi, kama vile msisimko usioisha na njia ya kuzungumza "kana kwamba anatazama maneno".
Wanawasiliana kwa Kihispania, lugha ambayo alisoma katika shule ya upili.
"Katika siku nzuri ninaelewa 90%, kwa siku za kawaida 60 - lazima uzingatie jinsi Wachile wanazungumza haraka". Wakati mwingine hutumia tafsiri za mtandaoni.
Pia alitambua kwamba wanashiriki upendo wa kupika.
"Nina mikono yangu katika unga sawa na mama yangu," alisema kwa mshangao huku akitengeneza empanada pamoja.
Alikuwa amerejea tu kutoka kutembelea mbuga ya wanyama ya Santiago, mahali pa kwanza ambapo wazazi wake Waamerika walimpeleka baada ya kuasiliwa. Dada yake wa kibaolojia ndiye alikuwa kiongozi wake wakati huu.
Kuona maeneo, kutembea mitaani, kujaribu chakula, kuzungumza, kugawana ... Hivyo ndivyo siku zake zilivyopita.
Ingawa pia alichukua fursa hiyo kukutana na wachunguzi, wanasheria na wawakilishi wa serikali.
"Njia pekee ya kuboresha hii ni kwa kuunganishwa tena na kujumuishwa," anasema.
Lakini leo hakuna utaratibu - wa kifedha au vinginevyo - kusaidia watoto wa Chile katika juhudi zao za kutembelea nchi yao ya asili.
"Mimi na mke wangu tuliuza lori letu ili tuweze kuja, lakini si kila mtu ana chaguo hilo."
Lakini pia anatafuta kutambuliwa zaidi, jambo ambalo Del Rio pia anasisitiza.
"Hatutaki pesa," mwanzilishi na mkurugenzi wa Nos Buscamos aliambia BBC.
"Tunachoomba ni kwamba Serikali inatambua kisheria wizi huu kama ukweli wa kihistoria."