Katiba mpya Tanzania: Maswali 4 mepesi yenye majibu magumu

Iliyochapishwa

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Mchakato wa Katiba mpya Tanzania ni kama umeanza rasmi hasa baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro kutangaza kuanza mchakato wa Katiba Mpya uliokwama na jana Rais Samia Suluhu Hassan kukutana Ikulu ya Chamwino Dodoma na watendaji muhimu wa mchakato huo.

Mbali na watendaji wengine Rais alikutana na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Ndumbaro na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Na katika kikao hicho akamuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi kuitisha kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu mbalimbali kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Pamoja na mambo mengine Kikosi kazi hicho kilichokuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala kilipendekeza kuwa mchakato wa Katiba ambao ulikwama tangu mwaka 2014 kufufuliwa tena.

Hivyo ni wazi Rais Samia na serikali yake wameonyesha nia njema ya kuibua mchakato huu. Lakini yapo maswali manne mepesi kuhusu hasa wapi uanzie, lakini ukiuliza wengi hasa watawala huwezi kupata jibu la moja kwa moja.

1: Uanzie kwenye rasimu ya Warioba?

Mchakato wa Katiba mpya Tanzania ulianza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.

Kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ikaanzishwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikuwa chini Uenyekiti wa Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Tume hii ndiyo iliratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba.

Rasimu hii ya pili ambayo ni maarufu kama Rasimu ya Warioba ikawasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba (BMK) ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa na wajumbe wengi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi -Zanzibar.

Wapo wanaotaka mchakato uanzie kwenye rasimu hii kwa sababu ndiyo ilikuwa na maoni halisi ya wananchi kabla baadhi kuondolewa kwenye hatua zilizofuata. Moja ya maoni yaliyotolewa ilikuwa ni kuundwa kwa Serikali tatu. Je ni hatua itakayobebwa? Swali jepesi, si rahisi kupata jibu la moja kwa moja.

2: Uanzie kwenye Bunge Maalumu la Katiba?

Bunge maalumu la Katiba (BMK), ambalo Makamu Mweyekiti wake alikua Samia Suluhu kabla hajawa rais, chini ya Uenyekiti wa marehemu Samuel Sitta (spika wa zamani wa bunge), ndiko kulikoibua mivutano mikali kuhusu masuala kadhaa yaliyomo kwenye rasimu ya pili ya katiba ya Warioba.

Jukumu kubwa la Bunge ilikuwa kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa kabla ya kwenda kupigiwa kura ya maoni.

Kutokana na mvutano mikali na kuonekana baadhi ya maoni ya wananchi yakichujwa, baadhi ya wajumbe wa bunge hilo hasa kutoka upinzani waliamua kujitoa na kususia mchakato.

Hata hivyo waliobaki ambao wengi walikuwa kutoka chama tawala (CCM) waliendela na mchakato na ikapatikana Katiba pendekezwa ambayo ilipaswa kupigiwa kura ya maoni.

Mchakato ukaishia hapo, hakukuwa na kura ya maoni mpaka leo. Wengi walikosoa mantiki ya kuwaaambia wananchi watoe maoni yao, halafu maoni hayo yanaondolewa na kundi la watu wachache. Waliiona Katiba pendekezwa ni kama imekosa muafaka na maridhiano amba unatajwa kuwa msingi wa kupata Katiba bora ya kitaifa yenye kukubalika na wengi. Je mchakato urudishwe kwenye bunge la Katiba na uanzie hapa?

Kwenye ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) waliyoitoa mwaka 2018 yenye kichwa cha habari 'Mchakato wa Katiba mpya nini mwisho wake?' ilisema ikianzia kwenye hatua hii basi 'Liwe Bunge linalotokana na watu wasio wanasiasa wengi kama ilivyokua Bunge lililotunga Katiba Inayopendekezwa'.

3: Uanzie kwenye kura ya maoni?

Kura ya maoni ni mchakato ambao wananchi wanapiga kura ama kuikubali ama kuikataa Katiba inayopendekezwa ambayo imetoka kwenye Bunge la Katiba.

Ni mchakato ambao uko chini ya Sheria ya Kura ya Maoni Na. 11/2013. Hata hivyo Mchakato huo ulikwama na Aprili 2, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30 mwaka huo hadi itakapotangazwa tena. Mpaka leo haijatangazwa.

Na alipoingia madarakani Rais wea awamu ya tano, Hayati John Magufuli aliweka wazi mchakato huo haukuwa kipaumbele chake. Je mchakato huu unaofufuliwa uanzie kwenye hatua hii?

4: Au mchakato uanze upya kabisa?

Hatua hii haionekani kama muafaka sana, lakini ni hatua inayoweza kufuatwa. Ingawa kwa mwaka ujao wa fedha serikali imeongeza shilingi bilioni 9 zaidi kuwezesha kukwamuliwa kwa mchakato wa Katiba mpya, kuanzia upya kabisa kunatajwa ni kama kupuuza rasilimali iliyotumika toka hatua ya kwanza ya mchakato huu ulioanza mwaka 2010/2011.

Lakini ipo bajeti ya kutosha kukidhi mahitaji ya mchakato mpya?

Maoni ya wadau wengi na mkutano wa kitaifa

Pamoja na maswali hayo manne ya wapi pa kuanzia kuufufua mchakato huu wa Katiba mpya, wadau mbalimbali tangu Rais Samia aonyeshe nia ya kuufua wamekuwa wakitoa maoni yao ya namna gani ya kuufufua na wapi pa kuanzia.

Wengi wanataka kwanza kuwe na mkutano mkubwa kitaifa kuchukua maoni ya wapi na namna gani ya kwenda. Rais sasa ametaka Baraza la Vyama vya Siasa kukutana pengine ni katika namna ya kuendelea kutafuta maoni ya namna gani ya kwenda.

Zitto Zuberi Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo mara kadhaa aliwahi kueleza kwamba unahitajika kufanyika kwa mkutano wa kitaifa ili kupata mwafaka wa masuala yaliyokwamisha mchakato wa awali.

Alitaka pia uanze kwa kuiboresha sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ili kuweka taratibu mpya za kisheria za kupata Katiba mpya.

Analolisema Zitto kuhusu sheria hii linaonekana pia kwenye ripoti ya LHRC ya 'Mchakato wa Katiba mpya nini Mwisho wake?'. Ripoti hii yenye inataja sheria ya kura ya maoni ikisema ' Kutokana na kupita kwa muda kisheria, maboresho ya Sheria ya Kura ya Maoni hayaepukiki ili kuruhusu mwendelezo mzima wa mchakato wa kupata katiba mpya'.

Zitto pia alitaka kuundwa kwa timu ya wataalamu 'kuwianisha rasimu za Katiba zilizopo, yaani ya Warioba na katiba pendekezwa'.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lisu alipohutubia wanachama wa chama hicho kanda ya Kaskazini kupitia mtandao wa zoom katika ukumbi wa Shaaban Robert jijini Tanga, Juni 2022 alisema mchakato huo uanzia pale ulipoishia mchakato wa Katiba ya tume ya Warioba.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria alisema pamoja na hilo kuna haja ya kufanya marekebisho kwa kuwa kisheria Katiba iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Warioba muda wake uliisha na kuna vipengele ambavyo vinahitaji kurekebishwa, ili viweze kuendana na matakwa ya Watanzania ya sasa.

Hili la mabadiliko ya sheria lilisemwa pia Juni 2022 na Taasisi ya Jukwaa la Katiba Tanzan ia (JUKATA) kupitia kwa mwenyekiti wake wa bodi, Ananilea Nkya.

"Tunapendekeza sheria ya mabadiliko ya Katiba na sheria ya kura ya maoni zitungwe upya ili ziendane na hali halisi ya maisha ya Tanzania leo hii', alisema Nkya na kuongeza ' Tunaamini kwamba Katiba tunayohitaji leo ni katiba iliyo bora kwa kila Mtanzania, siyo ili mradi Katiba, hapana'.