Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wazazi wanaovunja uhusiano na watoto wao
Watoto wengi hukata mawasiliano na wazazi wao kwa sababu ya migogoro.
Si kawaida kwa wazazi kukata uhusiano na watoto wao - lakini hutokea, na inaweza kuwa upweke sana.
Helen hajazungumza na mwanawe kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Mara ya mwisho aliposikia kumhusu, alikuwa gerezani.
Sasa ana umri wa miaka 31, amekuwa mraibu wa dawa za kulevya kwa zaidi ya muongo mmoja.
“Amejaribu kunipigia simu, labda ili kuniomba pesa, na sijakuwa nikipokea,” anaeleza Helen, anayeishi Uingereza.
"Hivi sasa, huo ni uamuzi sahihi kwa usalama na afya yangu."
Akiwa mlezi mkuu wa binti mdogo wa mwanawe, lengo la Helen ni kuandaa mazingira yenye upendo na salama kwa ajili yake na mjukuu wake anapoendelea kukua.
Helen anamkumbuka mwanawe kama mtoto mpotovu na mharibifu, lakini mwenye ucheshi mbaya na roho nzuri.
“Alichanganyikiwa wakati, akiwa kijana, "tabia yake iligeuka kuwa ya uadui na akaanza kujifungia ndani ya choo kwa saa nyingi wakati fulani", Helen anakumbuka.
“Nilipomkabili, aliniambia mimi ndiye mwenda wazimu, ninayetumia dawa za kulevya. Wakati fulani, nilitaka kucheka, ilikuwa tukio la dharau sana.”
Helen alipogundua kuwa anatumia dawa za kulevya za heroini, hakujua wapi kwa kuanzia.
Angetoweka kwa siku nyingi, akirudi akiwa na majeraha ya kila aina.
Alipokuwa nyumbani, alikuwa mtu mwenye tabia ngumu sana kuwa naye karibu.
"Hakuwahi kunipiga, lakini mara nyingi aliharibu gorofa kwa hasira - bado kuna shimo kwenye ushoroba ambapo alipiga kwa ngumi," anaelezea.
Kazini, alilipwa pesa taslimu, ambayo anasema mtoto wake alianza kuichukua kutoka kwa pochi yake.
Hakutaka kusema lolote alipoanza kuwa na hasira, na mama huyo alianza kuweka pesa kwenye mkanda kiunoni mwake.
"Nilisema mapato yangu yaingia moja kwa moja kwenye akaunti ili nipate ukadiriaji bora," anasema.
Hatimaye alijisikia kutokuwa salama kuishi na mtu aliyezama ndani ya uraibu wa dawa za kulevya, na kukata mawasiliano naye.
Uhusiano kati ya mzazi na mtoto unatarajiwa kuwa wa kudumu milele - wenye kuzaa matunda, upendo ambao unaweza kustahimili panda shuka zote za maisha.
Hata hivyo, kwa wazazi wengine, kudumisha uhusiano huu inaweza kuwa vigumu.
Hatimaye, mzazi anaweza kuhisi kuwa amefikia hatua ya kutorudi nyuma, na hivyo kuchagua kuacha kutekeleza jukumu lake kama mzazi.
Katika ulimwengu unaozidi kuwa na mgawanyiko, gumzo kuhusu watoto wanaoacha kuwasiliana na wazazi wao imekuwa kawaida tu.
Na bado pia hutokea kwa njia nyingine, hata kama mazungumzo hayo hutokea mara chache.
Hii inaweza kuwa kwa kiasi kwa sababu data inaonyesha kwamba wazazi kukata uhusiano na watoto wao ni nadra sana: utafiti wa 2015 uliofanywa na shirika la kutoa misaada la Uingereza la Stand Alone ulionyesha kuwa 5% ya wazazi waliokata uhusiano na watoto wao walikuwa ni maamuzi yao wenyewe.
Uamuzi tayari ni mgumu na wenye uchungu mwingi, na wale wanaopitia utengano huu, wanasema unadra wake unafanya kuwa sawa na kutengwa, na inaweza kuongeza unyanyapaa kwa wale wanaochagua kufuata njia hii.
Upendo usio na masharti unaweza kuwa tatizo.
"Katika utafiti na utamaduni maarufu, ni nadra sana kusikia kutoka kwa wazazi wanaojitenga na watoto wao kwa sababu ni mwiko, na kuna matukio machache sana kuzungumzia waziwazi kuhusu kile unachopitia," anaeleza Lucy Blake, mhadhiri mkuu wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Uingereza Magharibi, Bristol, ambaye ni mtaalamu wa matukio ya utengano.
Sababu zinazofanya wazazi kusitisha uhusiano na watoto wao ni sawa na sababu zinazofanya watoto kuwakatisha tamaa wazazi wao: kulingana na Blake, miongoni mwa mambo yanayotajwa sana ni migogoro ya kifamilia, tofauti za maadili ya kibinafsi (kama vile imani za kidini), matumizi mabaya ya dawa za kulevya na tabia nyingine mbaya sana.
Utafiti mmoja ulionyesha kuwa kwa kuvunjika kwa uhusiano na watoto wa kiume, masuala yanayohusiana na talaka, wakwe na ndoa ndiyo yaliyokuwa yakiripotiwa zaidi kuchangia; huku upande wa mabinti, matatizo ya kiakili na unyanyasaji wa kihisia yalikuwa yakichangia pakubwa.
Hata hivyo, uamuzi huu wa kuvunjika uhusiano na watoto huwa wa mwisho kabisa na mgumu zaidi.
Katika jamii, wazazi wanatarajiwa kutunza watoto bila ubaguzi.
"Tuna matarajio makubwa sana kama mzazi, ambapo tunataka wawe na upendo usio na masharti," anaeleza Blake.
"Hii inaweza kuwa shida sana, kwani inapendekeza wanapaswa kukubali aina yoyote ya vile watakavyochukuliwa, ikiwa ni pamoja na aina zote za unyanyasaji wa kisaikolojia na kifedha."
Labda hii ndiyo sababu, hata wakati watoto wao wanawaumiza, wazazi wanajitahidi kuondokana na kusahau hisia hizo.
Jennifer Storey, mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kent, Uingereza, ambaye ni mtaalamu wa unyanyasaji kati ya watu, anaona kwamba katika mahojiano yake mengi na waathiriwa wa unyanyasaji, wazazi bado wana wasiwasi na huzuni kwa watoto wao.
"Ninajaribu kukumbuka mzazi mmoja ambaye alitaka sana kukatisha uhusiano na mtoto wao - karibu kila mara walitaka uhusiano huo uendelee, lakini hasa unyanyasaji ukome," anaeleza.
Inaweza pia kuwa vigumu kwao na kwa watu walio karibu nao kukubali ukweli wa kile kinachotokea.
“Wazazi hufikiriwa kuwa na uwezo wote, lakini kadiri mtoto anavyokua, nguvu hizo hubadilika,” anasema Amanda Holt, mwandishi wa kitabu cha ‘Adolescent-to-Parent Abuse: Current Understandings in Research, Policy and Practice’.
“Kutokuwa na imani kwamba unyanyasaji wa mzazi na mtoto unaweza kutokea, au kwamba inaweza kuwa mbaya sana kiasi cha mzazi kuhitaji kujiondoa, ni sababu nyingine ambayo ni vigumu sana kuondokana nayo.”
Mahusiano mazuri zaidi na watoto yanahusishwa na ustawi wa mzazi ulioboreshwa, ubora zaidi wa maisha na dalili za kupungua kwa huzuni; mahusiano mazuri zaidi na mzazi hayahakikishii manufaa sawa.
Hii ina maana kwamba uchaguzi wa mzazi wa kukata mawasiliano na mtoto, iwe kwa ghafla au hatua kwa hatua, haulengi tu uzito wa kushindwa.
"Uzazi ni jukumu na utambulisho unaoheshimiwa na kupendwa - pia unabadilisha maisha milele," anaelezea Blake.
"Wakati mzazi hana uhusiano mzuri na mtoto wao, wanaweza kuhisi wameshindwa katika jukumu hili, na kuleta hisia za maumivu makali na aibu."
Kwa kuzingatia vipengele hivi, inaweza kuwa changamoto zaidi kwa wazazi kukata mahusiano kuliko ilivyo kwa watoto.
"Kwa hakika inaweza kuwa aina tofauti ya uchungu, kwa sababu kwa wazazi, kuna uwezekano kwamba maisha yao yanaonekana kuwa na pengo au yasiyo na maana," anasema Blake.
Wengi watapoteza urafiki na uhusiano na wanafamilia wengine kama matokeo.
"Hasara na uchungu unaoambatana na kutengwa hujitokeza ili kugusa nyanja nyingi tofauti za maisha ya watu," anasema Blake.
Katika baadhi ya matukio, kama ya Helen, uamuzi wa kukata mawasiliano unafanywa wazi na mtu mmoja.
Lakini chanzo cha ugomvi kati ya wazazi na watoto mara nyingi kinaweza kutatanishwa zaidi.
Jack, anayeishi Marekani, alikuwa ameoana na mke wake kwa karibu miongo miwili, wakati huo walikuwa na watoto wanne pamoja.
Wakati wa kutalakiana, binti yao mdogo alikuwa na umri wa mwaka mmoja.
Wakati mke wake wa zamani alipoolewa tena, anasema, mtoto wake mdogo alivutiwa zaidi na baba yake wa kambo kuliko yeye - na alipokua karibu, mtoto alionekana kutofurahia kutumia muda na Jack.
Jack anasema alifikia hatua ya kuvunja uhusiano na binti yake alipokuwa na umri wa miaka 14. Baada ya kutofautiana kuhusu amri ya kutotoka nje, alimwambia Jack kwamba alichukia wikendi alizokuwa pamoja naye, na akamwita mama yake kwa ajili ya safari kwenda kwenye tukio alilopanga kuhudhuria.
"Nilimtumia barua pepe mpenzi wangu wa zamani kusema ilionekana [binti yangu] hataki tena kuwa nami kila wikendi, na kama hilo lingebadilika katika siku zijazo, angekaribishwa kwa mikono miwili," anasema Jack.
Hamlaumu binti yake kwa kufanya hivyo, lakini hajamsikia wala kumuona tangu wakati huo.
Ingawa binti yake alikata mawasiliano mwanzoni, Jack hajahisi hitaji la kurejesha tena mawasiliano naye moja kwa moja.
"Kadiri muda unavyoendelea, imepunguza hitaji langu la kuanzisha tena uhusiano huu. Inahisi kama kifo kwangu, na nimesonga mbele, "anasema.
“Katika hatua hii ya maisha yangu, kwa kiwango cha faraja ninachofurahia katika mahusiano niliyonayo, bila shaka nisingependezwa na muda unaohitajika kuwekeza katika kujenga uhusiano wa maana na yeye, bila kusahau vituko ambavyo vingeambatana na hilo,” anaeleza.
Simulizi ya Jack inaonyesha ukweli wa utengano wa mzazi na mtoto.
Binti yake alionyesha kutopendezwa naye, lakini yeye ndiye aliyependekeza kuwacha kuonana naye.
Helen, kwa upande wake, amekatiza mawasiliano na mwanawe mara kadhaa – wamekuwa katika kipindi cha kukata uhusiano na kufanya maridhiano kwa miaka. Lakini kwa sasa, hajawasiliana naye - na hana uhakika ni nini kitakachofuata.
“Ikiwa angenionyesha kwamba amejitolea kubadilika na kutoka gerezani, labda ningemtaka arudi katika maisha yetu,” anaeleza.
"Lakini sijui jinsi ninavyoweza kumwamini tena."
'Maisha ya upweke'
Hata kwa wazazi ambao wako thabiti katika hoja yao ya kukatisha uhusiano na watoto wao, ukweli wa siku hadi siku wa uamuzi wao si rahisi.
"Kibayolojia, kisheria na kijamii, kuna uhusiano na mtoto ambao ni wa kina sana," anaelezea Holt. Kiasi kwamba wazazi wakiukatisha, uhusiano huo unaweza kuisha lakini kuna mshikamano fulani ambao unaweza ukaendelea. Inaweza kuwa vigumu sana kusahau kila kitu.”
Wazazi wengi ambao huanzisha kukatisha uhusiano na watoto wao hukutana na aibu na lawama zinazozunguka uamuzi wao na pia husababisha kutengwa kwa papo hapo hata na jamaa wenye uhusiano nao wa damu.
"Wazazi ambao wameamua kukatisha uhuasiano na watoto wao, wanaweza tu kuzungumza na wale ambao wataonyesha huruma na kuelewa msingi wa msimamo wao," aeleza Blake.
"Kunaweza kuwa na fursa ya kuzungumza juu ya hisia za huzuni na kupoteza, lakini ni kana kwamba hilo limeisha na watu wanatarajiwa ukubali matokeo na kusonga mbele na maisha."
Huruma na fursa ya kuzungumza inaweza kuwa muhimu hasa katika nyakati maalum katika kipindi cha mwaka mzima - na muda huu ni tofauti kwa kila mzazi.
Maumivu huwa mabaya zaidi wakati wa likizo: kulingana na utafiti wa Stand Alone, 90% ya watu waliokatisha uhusiano na mwanafamilia huwa na kipindi kigumu wakati wa likizo, wakati 85% hutatizika zaidi siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa mtoto na 81% hupata shida kuwa karibu na familia zingine.