Vita Sudan: Kwanini nchi za Afrika zinajikongoja kuondoa raia wake?

Chanzo cha picha, EPA
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Mshike-mshike wa kuwaondoa raia nchini Sudan unaendelea, nchi za Ulaya zinatuma ndege za kijeshi na helikopta kuondoa raia wake na kuwapeleka maeneo salama. Maelfu ya watu wamesha ondoshwa hadi sasa.
Ila hali ya raia wa mataifa ya Afrika, bado ina suasua, kuna idadi ndogo hasa wale wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wameondolewa. Wengi bado wamekwama wakisubiria hatima ya ahadi wanazo pewa na serikali zao.
Hii kwa wengi inakumbusha mwaka mmoja nyuma wakati Urusi inaivamia Ukraine. Raia wa mataifa ya Afrika walipitia changamoto nyingi kuondoka Ukraine, kiasi cha kukumbana na ubaguzi walipokuwa wakifanya juhudi za kuingia Poland.
Kwa uhakika nguvu ndogo zinazotumiwa na mataifa ya Afrika kuwashughulikia raia wake wakati wa migogoro, ni moja ya chanzo cha kutokea changamoto kama ile iliyotokea katika mpaka wa Ukraine na Poland.
Mgogoro wa Sudan upo ndani ya bara la Afrika. Pengine hilo lingesaidia kurahisisha Waafrika kuondolewa mapema zaidi, kuliko raia wa mabara na mataifa mengine, lakini hali haionekani kuwa hivyo.
Juhudi za kuwaondoa Waafrika bado ni za mwendo wa jongoo. ‘Usalama’ ikiwa ndio kauli ya kujitoa kimasomaso. Usalama ni jambo la kulizingatia kweli. Raia wa mataifa mengine wamesha ondoshwa kwa mamia, na nchi za Afrika hazijaondoa raia wake kwa wingi kama nchi za Ulaya, hapo kuna tatizo la kimipango pia, sio usalama pekee.


Afrika imesimama wapi hadi sasa?
Hadi siku ya Jumatatu Aprili 24, orodha ya nchi zilizokwisha ondoa raia wake, iliyochapishwa na shirika la habari la AP, inaonesha kuna nchi mbili pekee za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kenya na Afrika Kusini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Nchi nyingi katika orodha hiyo ni zile za Ulaya na mabara mengine. Na idadi ya walioondolewa na nchi hizo mbili, bado ni ndogo ukilinganisha na mamia ya watu waliokwisha ondolewa na nchi za Ulaya.
Serikali ya Afrika Kusini imeeleza raia wake 77 wakijumuisha wafanyakazi wa ubalozi, wako njia kuondoa Khartoum. Wakati wanafunzi wa Kenya 29 ndio ambao wamevuka kuingia Ethiopia, na wengine 18 wakiwa njiani kupitia mpaka wa Sudan Kusini.
Awali Kenya ilieleza juu ya uwepo wa takribani raia wake 3000 waliokwama Sudan, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nje wa taifa hilo, Dkt. Alfred Mutua. Kwa kuzingatia idadi hiyo na namna uokoaji ulivyo, bado kuna kusuasua kukubwa.
Wakati huo huo kuna kundi kubwa la Waafrika wanaopambana kujiokoa wenyewe, wakisafiri kuelekea mpaka wa Sudan Kusini. Zaidi ya watu elfu kumi, kwa mujibu wa serikali ya Sudan Kusini wameingia nchini humo, wengi wao wakiwa ni Wasudan, Wasomali, Waeritrea na Wakenya.
Kwa mujibu wa serikali ya Nigeria, kuna raia 5,000 wa nchi hiyo nchini Sudan. Hadi siku ya Jumatatu Nigeria ilikuwa bado haijaondoa raia wake, matarajio ni kuwa shughuli ya uokoaji ianze siku ya leo kwa usafiri wa mabasi hadi Cairo kabla ya kupaa kurudi Nigeria.
Gazeti la Daily Monitor la Uganda, liliripoti siku ya jana liki mnukuu Balozi wa nchi hiyo nchini Sudan, Dkt. Rashid Ssemuddu juu ya uwepo wa Waganda zaidi ya mia mbili wanaosafiri kuondoka Khartoum. Ingawa bado raia hao hawajawasili Uganda.
Kuna nchi nyingi katika bara la Afrika bado hazijaeleza hata mipango yao ya kuondoa raia. Yumkini zipo ambazo zinasubiri huruma za nchi nyingine au raia wake wapambane wenyewe namna ya kujinasua katika uwanja wa vita.
Ukiangalia nchi za awali kuondoa rai wake, sio za Afrika, zilikuwa ni nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, kisha zikafuatiwa na Marekani, Uingereza, Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya na yale ya Asia. Kuna kujikongoja kukubwa kwa nchi za Afrika kuondoa raia wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ushirikiano usiokuwepo Afrika

Kuna ushirikiano mkubwa umefanyika kufanikisha idadi kubwa ya raia wa mataifa ya Ulaya kuondolewa Sudan. Ushirikiano ambao unaonekana kuwa mdogo au kutokuwepo kabisa miongoni mwa mataifa ya Afrika.
“Zaidi ya raia 1000 wa umoja wa Ulaya wameweza kuondoka Sudan kutokana na juhudi za pamoja za nchi nyingi ambazo zimewa okoa raia wengine wa Umoja wa Ulaya pamoja na raia wa nchi zao,” Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya Josep Borrell alieleza Jumatatu.
Hadi siku ya Jumatatu Italy, ilikuwa imesha ondosha watu takribani 200 na kuwapeleka Djibouti, Waziri wa Mambo ya Nje, Antonio Tajani alielza. Wakiwemo Waitalia 140, raia wengine wa mataifa ya Ulaya na wafanyakazi wa ubalozi wa Vatican.
Uhispania imeondoa takribani watu 172 kutoka Khartoum na kuwapeleka Djibouti. Kati ya hao wamo raia 32 wa taifa hilo, wengine ni raia wa Argentina, Colombia, Ireland, Italy, Mexico, Portugal na Poland.
Hali ni hiyo hiyo kwa mataifa mengine ya Ulaya yaliyohusika kuondoa watu; mfano Ufaransa, Ujerumani, Norway, Finland, Netherlands, Bulgaria, Sweden, Denmark, yamekusika pakubwa kuokoa raia wao na wa mataifa mengine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Upi wajibu taasisi za Afrika?

Wakati nchi za Ulaya zinaondoa raia wao kwa ushirikiano, wapo wanaohoji nafasi za taasisi kubwa za Afrika katika kusaidia dharura kama hii. Taasisi zenye majina makubwa, mfano Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) au ile Jumuiya ya Kiuchumi cha nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS).
Umoja wa Afrika (AU) unaonekana kujikita zaidi kwenye kutafuta suluhu ya mgororo huu kwa njia za mazungumzo. Na suala la kuwaondoa raia limeachwa kwa nchi zenyewe za Afrika, hii ni tofauti kidogo na namna Umoja wa Ulaya ulivyoamua kufanya.
Kwa hakika Umoja wa Afrika unao uwezo wa kuyafanya yote mawili kwa wakati mmoja, kuisimamia juhudi za kusitisha mapigano, na vilevile kuwa mstari wa mbele kuhakikisha Waafrika wanaondoka Sudan salama.
Kuna ukweli kwamba nchi nyingi za Afrika ni masikini, na hazina uwezo kama ule wa Marekani na nchi za Ulaya wa kupaisha madege makubwa ya kijeshi, katika hali kama hii ushirikiano unabaki kuwa njia bora zaidi ili hata nchi zisizo na uwezo kuinuliwa.
Mgogoro mfano ule wa Ukraine na huu wa Sudan, yanapaswa kuwa waalimu kwa mataifa ya Afrika kujifunza kuwa wa kwanza kuondoa raia wao kila penye hatari. Bila shaka Waafrika wataondoshwa Sudan, ila swali ni kwanini wawe wa mwisho mwisho?
Ni matumaini ya wengi kwamba makubaliano ya masaa 72 ya kusitisha mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), yaliyoanza Jumatatu usiku, (ikiwa yatadumu) yatatoa mwanya kwa nchi za Afrika kuondoa raia wake kwa wingi.















