UEFA yaandaa mashtaka ya jinai dhidi ya Infantino

Chanzo cha picha, Getty Images
Shirikisho la Soka barani Ulaya, UEFA, linaandaa mashtaka ya jinai dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kufuatia mpango uliokwama wa kuuza hisa katika Kombe la Dunia na mashindano mengine ya FIFA kwa wawekezaji binafsi.
Nyaraka ambazo BBC Sport imeziona, zinaonyesha kuwa UEFA imeomba kupata ushahidi na nyaraka zitakazotumika katika kesi nchini Uswisi dhidi ya Rais huyo, ambaye UEFA imemtuhumu kwa "utawala mbaya".
UEFA pia imesema inazingatia kuchukua hatua za kisheria za jinai dhidi ya maafisa wengine wa FIFA.
Muda mfupi baada ya Kombe la Dunia la mwaka huu, Infantino alipendekeza kuanzishwa kwa kampuni mpya iliyoitwa FIFA Forward Enterprise (FFE), ambayo ingehamisha hisa katika mashindano ya soka ya FIFA kwa wawekezaji binafsi. Mpango huo ulisitishwa baada ya kukabiliwa na upinzani mkubwa.
Katika ombi lake la kupata ushahidi, UEFA ilisema: "Kiuhalisia, ulikuwa mpango ambao Infantino na kundi lake dogo walilenga kujimilikisha moja kwa moja sehemu ya mali zenye thamani kubwa zaidi za FIFA, na kunufaika nazo kwa manufaa yao wenyewe, lakini yenye kuleta madhara kwa FIFA, wanachama wake na jumuiya nzima ya soka."
Infantino aliupitisha mpango huo katika mchakato wa ndani wa kuidhinishwa na FIFA siku chache zilizopita, katika kikao kilichoandaliwa kwa haraka, ambapo kundi dogo la maafisa wa FIFA na baadhi ya wafanyakazi ambao hawakuwa wamewahi kuusikia mpango huo, walipewa saa chache kuutekeleza mradi huo ambao haujawahi kufanyika na uliokuwa na thamani ya mamilioni ya dola.
Maafisa wakuu kutoka UEFA na viongozi wa soka barani Ulaya walikutana Monaco, muda mfupi kabla ya droo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku suala la Infantino likiwa miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa.
BBC Sport imewasiliana na Infantino na FIFA kutafuta majibu.
UEFA ilisema nini katika ombi lake la kisheria?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
UEFA ilisema thamani ya hisa zilizokuwa zikitarajiwa kuuzwa haikuthibitishwa kwa njia huru na kwamba zingetolewa kwa bei ya chini sana. UEFA iliuelezea mpango huo kama "bei ya ulaghai iliyowekwa chini ya thamani ya soko na kusukumwa na Infantino kwa ajili ya kujinufaisha binafsi".
Katika ombi hilo pia ilisema:
"Chini ya masharti yaliyotolewa na Infantino, wawekezaji hawa wangenunua hisa za kudumu katika kitengo cha biashara cha FIFA kwa dola bilioni 4.2, sawa na thamani ya kampuni ya dola bilioni 20 pekee, ambayo haikupatikana kupitia ushindani wa wazi wa soko wala kufanyiwa tathmini huru."
Katika ombi hilo, UEFA inaiomba mahakama huko Florida, Marekani, kukamata data inayoshikiliwa na kampuni mbili zinazomilikiwa na FIFA, FIFA Americas na FWC2026, kwa ajili ya kutumiwa baadaye katika kesi ya jinai nchini Uswisi.
Kampuni hizo mbili zina makao makuu Florida.
UEFA ilisema wanachama wake 55 wanaweza kuathiriwa na mpango huo wa uuzaji, na kwamba inaweza kufungua mashtaka ya jinai dhidi ya maafisa wengine wa FIFA pamoja na Infantino.
"UEFA na wahusika wengine wanaohusika wanaandaa kufungua mashtaka ya jinai nchini Uswisi dhidi ya Infantino na huenda maafisa wengine wa FIFA pamoja na washauri, kwa tuhuma za usimamizi mbaya wa mali," ombi hilo lilisema.
"Muundo wa siri, tathmini ya thamani, ufadhili na uuzaji wa mpango huo umesababisha madhara ya moja kwa moja na makubwa kwa sifa, utawala na mahusiano ya kibiashara ya FIFA, na hivyo kuidhuru FIFA pamoja na wanachama wake 211, wakiwemo vyama 55 vya wanachama wa UEFA."
UEFA inasisitiza kuwa mpango huo uliandaliwa bila wao kujua, wala bila taarifa kwa wadau wengine muhimu wa soka, na kwamba ulikuwa umeandaliwa kwa muda mrefu.
Katika waraka huo, UEFA ilisema kulikuwa na "historia ndefu ya ufisadi miongoni mwa maafisa wa FIFA" na ikasema chombo hicho kinachosimamia soka duniani kingeweza kubadili mipango yake tu pale shinikizo lingetoka nje ya ulimwengu wa soka.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mamlaka makubwa ya FIFA kwenye soka duniani yameendeshwa kwa kiasi kikubwa bila mifumo ya maana ya ndani ya udhibiti na uwajibikaji, huku uwajibikaji ukitokana zaidi na nguvu za nje, ikiwa ni pamoja na shinikizo la kisiasa, uchunguzi wa umma na hatua za utekelezaji wa sheria za kimataifa za jinai," UEFA ilisema katika ombi hilo.
FIFA ina makao makuu yake Zurich, Uswisi, na UEFA imesema mpango wake wa hatimaye kufungua mashtaka ya jinai dhidi ya Infantino unaungwa mkono na sheria za Uswisi.
BBC Sport imeelezwa kuwa kesi nyingine tofauti imefunguliwa katika mahakama ya New York, ambapo UEFA inataka kupata nyaraka kutoka Thrive Capital, kampuni iliyopendekezwa kununua FFE, pamoja na mwanzilishi wake Josh Kushner, ambaye ni shemeji wa Rais wa Marekani Donald Trump.
Benki ya uwekezaji ya Marekani, JP Morgan, pia imetajwa katika ombi hilo.
Ombi la tatu limewasilishwa Colorado, likimhusu aliyekuwa mkuu wa Formula 1, Greg Maffei, ambaye katika nyaraka za mahakama ametajwa kuwa "mshauri muhimu wa kibiashara" katika mpango wa FFE, pamoja na kampuni yake ya Bann Ventures.
BBC Sport pia imewasiliana na UEFA kutafuta maoni yake.
UEFA iliongoza upinzani dhidi ya mpango huo, ikiweka wazi kuwa haina imani na Infantino, na wanachama wake walikubaliana kususia Kombe la Dunia iwapo mradi wa FFE usingeondolewa.
Infantino, ambaye anawania muhula wa nne wa uongozi wa FIFA mwezi Machi, ametuhumiwa "kuusaliti" uaminifu aliowekewa, kwa mujibu wa barua ya wazi iliyotolewa kwa pamoja na UEFA, Concacaf na Shirikisho la Soka la Asia.
Chama cha Soka cha Uingereza kimejiondoa katika kumuunga mkono Infantino, lakini bado anaungwa mkono na Shirikisho la Soka la Amerika Kusini, Conmebol, pamoja na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Baadhi ya nchi pia zimejiondoa katika mashirikisho yao ya bara ili kuonyesha kumuunga mkono Rais huyo wa FIFA.















