Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafui: 'Fungu la mchanga bahari Tanzania linaloonwa kwa ratiba kama mwali'
Na Leonard Mubali, BBC Swahili
Je umewahi kusikia fungu la mchanga bahari?ikifahamika kitaalam kama SandBar. Ni tabaka la ardhi linalopatikana katika kina kirefu cha maji.
Fungu la mchanga bahari kubwa zaidi duniani, liko Australia lijulikanalo kama Fraiser ambalo ni kivutio kikubwa cha utalii.
Nchini Tanzania pia ambako zaidi ya asilimia 20 ya fedha za kigeni zinatokana na utalii, lipo fungu la mchanga linaloitwa Mafui ambalo linavutia maelfu ya watu kwenda kulitembelea, kutokana na upekee na mvuto wake.
Kutokana na ukubwa wa rundo hili la mchanga kwenye kina cha bahari wapo ambao hudhani ni kisiwa lakini si kisiwa, hiyo ni dhana tu, uhalisia ni kwamba ni tabaka la mchanga tu uliojirundika katikati ya kina kirefu cha bahari, ambalo huonekana pale tu maji yanapokupwa.
Mchanga wa Mafui ni mwali anayeonekana kwa ratiba
Katika baadhi ya maeneo Afrika, ikiwemo mikoa ya kusini na Pwani ya Tanzania, neno la kitamaduni na kimila la mwali ama mwanamwali si geni. Ni binti aliyekomaa ambaye hajaolewa.
Utamaduni huu ujumuisha wasichana kuwekwa ndani kwa muda wa miezi kadhaa kwa ajili ya ya kufundwa na watu wazima kujianda kwa ajili ya maisha ya utu uzima ikiwemo ndoa.
Wakati mwanamwali akiwa ndani kumuona ni kazi sana, ni ngumu. Wakati mwingine hata kama binti huyo una unasaba naye, bado itakuwia vigumu kumuona. Lazima utaratibu maalumu wa kimila ufanywe.
Hivyo hivyo kwa Fungu la mchanga la Mafue, hauwezi kwenda tu na ukaliona lazima ufuate taratibu na ratiba maalumu. Na pengine kwa muktadha huu, leo fungu la mchanga la Mafui ni maarufu kwa jina la Mwali.
'Lina uwezo wa kuonekana kwa muda wa saa mbili hadi tatu na baadae kufunikwa na bahari na kupotea kabisa', anasema Ephraim Mwangomo, Kamishna msaidizi uhifadhi kutoka hifadhi ya taifa ya Saadani.
Mwangomo anasisitiza hapa 'ili uweze kuliona (fungu la mchanga) ni lazima uje muda muafaka ambapo maji yatakuwa yameondoka'. Vinginevyo unaweza kwenda na usilione. Lakini pia hautapaswa kutumia muda mrefu kwenye mchanga huo, kwa kuwa maji yakirejea unafunikwa na kupotea kabisa.
Fungu hili la mchanga linapatikana wapi na lina sifa gani za kipekee?
Yapo mafungu mengi ya mchanga bahari duniani. Lakini mengi si sehemu ya hifadhi za taifa. Fungu la mchanga Mafui ni sehemu ya hifadhi ya taifa ya Saadani, iliyopo Bagamoyo, mkoani Pwani, umbali wa saa mbili na nusu kutoka Jijini Dar es Salaam kwa gari.
Linapatikana katika hifadhi ya taifa ya Saadani, ambayo ni hifadhi pekee katika ukanda wa afrika ambayo kwa wakati mmoja eneo la nchi kavu na bahari ni vivutio vya utalii.
Ni fungu la mchanga la kipekee katika ukanda wa bahari ya hindi. Ni eneo kubwa la rundo la mchanga ambalo huonekana pale tu maji yanapo kupwa lakini hupotea na kufunikwa maji yanapojaa.
Moja ya sifa kubwa ya fungu hili la mchanga ni kuwa na mchanga wa rangi nyekundu ambao ni laini na unaovutia kuutazama na hata kutembea juu yake.
Linazungukwa na viumbe hai kama vile Kasa, kuna mawe aina ya Matumbawe yenye rangi tofauti na maumbo tofauti ambayo hutumika kama ni mazalia ya Samaki.
Mamia ya watu wanaofika hapo, wanaonekana kufurahia muundo wake, ulaini wa mchanga wake, unaozungukwa. Ukiacha kufurahia muonekano wake, wapo wanaolitumia kuvishana pete, kwa wanandoa watarajiwa.