Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa Ukraine: Jenerali mwingine wa Urusi auawa Ukraine
Vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimethibitisha kifo cha mmoja wa majenerali wakuu wa Moscow wakati wa mapigano makali katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.
Meja Jenerali Roman Kutuzov aliuawa akiongoza shambulio kwenye makazi ya watu katika eneo hilo, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa shirika la serikali la Rossiya 1.
Alexander Sladkov alisema Jenerali Kutuzov amekuwa akiongoza wanajeshi kutoka Jamhuri ya Watu wa Donetsk iliyojitangaza kuwa huru.
Wizara ya ulinzi ya Urusi haijazungumzia ripoti hizo.
Jeshi la Ukraine pia lilithibitisha kuuawa kwa Jenerali Kutuzov, bila kutoa maelezo zaidi kuhusu hali hiyo.
Kifo chake kinakuja huku uvumi ukienezwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba afisa mkuu wa pili, Luteni Jenerali Roman Berdnikov, kamanda wa Jeshi la 29, pia aliuawa katika mapigano mwishoni mwa juma. BBC haiwezi kuthibitisha madai hayo.
Makamanda wa Urusi wamezidi kulazimishwa kuwa mstari wa mbele vitani katika jaribio la kuendeleza uvamizi huo na Moscow imethibitisha vifo vya majenerali watatu wakuu.
Kyiv inadai kuwaua majenerali 12 na maafisa wa ujasusi wa nchi za Magharibi wanasema takriban makamanda saba wakuu wameuawa.
Lakini kumekuwa na utata juu ya ripoti za vifo vya maafisa wengine kadhaa wa Urusi. Majenerali watatu ambao vikosi vya Ukraine vilidai kuwaua wameripotiwa kuwa hai.
Mwezi Machi, vikosi vya Ukraine vilisema Meja Jenerali Vitaly Gerasimov aliuawa nje ya mji wa pili wa Kharkiv nchini humo. Hata hivyo, tarehe 23 Mei vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilisema alikuwa ametunukiwa heshima ya serikali na kutupilia mbali ripoti za kifo chake.
Mnamo mwezi Machi, afisa katika kundi la ndani la Rais Volodymyr Zelensky aliliambia jarida la Wall Street kwamba timu ya maafisa wa ujasusi wa kijeshi wa Ukraine walikuwa wamepewa jukumu la kutafuta na kulenga maafisa wa jeshi wa vyeo vya juu wa Urusi.
"Wanatafuta majenerali wa hadhi ya juu, marubani, makamanda wa silaha," afisa huyo alisema. Waliongeza kuwa maafisa hao walilengwa aidha kwakutumia walenga shabaha au mizinga.
Majenerali wa Urusi waliouawa
Luteni Jenerali Yakov Rezantsev aliripotiwa kuuawa na shambulizi la Ukraine kwenye uwanja wa ndege wa Chornobaivka karibu na mji wa Kherson.
Alipandishwa cheo na kuwa Luteni jenerali mwaka jana, na alikuwa kamanda wa kikosi cha 49 cha wilaya ya kijeshi ya kusini mwa Urusi.
Inasemekana alishiriki katika operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Syria.
Meja Jenerali Oleg Mityaev aliripotiwa kufariki mahali fulani karibu na jiji la Mariupol, jiji lililo kusini-mashariki mwa Ukraine ambalo lilikuwa eneo la kuzingirwa kwa muda mrefu na Urusi.
Kikosi cha Azov kilidai kumuua.
Alikuwa kamanda wa kitengo cha 150 cha bunduki za magari cha jeshi la Urusi, kitengo kipya kilichoundwa mnamo 2016, na kilichowekwa katika mkoa wa Rostov karibu na mpaka wa Ukrain.
Ukraine inadai kuwa kitengo hicho kiliundwa ili kushiriki katika mzozo katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi mashariki mwa Ukraine, ingawa Urusi inakanusha kuwa jeshi lake lilihusika katika mapigano huko.
Meja Jenerali Andrei Kolesnikov, wa jeshi la pamoja la 29, aliuawa katika mapigano tarehe 11 Machi, kulingana na vyanzo rasmi vya Ukrain.
Mazingira ya kifo chake hayakutolewa.
Baada ya Kolesnikov kuwa jenerali wa tatu wa Urusi kuripotiwa kuuawa nchini Ukraine, afisa mmoja wa nchi za magharibi aliwaambia waandishi wa Habari kwamba jeshi la Urusi linaweza kuwa na ari ya chini, na ndiyo maana maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi wanasonga kwenye mstari wa mbele.
Meja Jenerali Andrey Sukhovetsky, naibu kamanda katika kitengo sawa na Gerasimov, aliripotiwa kuuawa na mlenga shabaha mnamo tarehe 3 Machi.
Kama Gerasimov, Sukhovetsky alikuwa sehemu ya operesheni za kijeshi za Urusi huko Crimea na Syria.
Tofauti na majenerali wengine, kifo cha Sukhovetsky kiliripotiwa kwenye vyombo vya habari vya Urusi na Rais wa Urusi Vladimir Putin alithibitisha katika hotuba yake kwamba jenerali mmoja alikufa huko Ukraine.