Miaka mitatu ya Lissu kusotea stahiki zake za ubunge

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Kama angeshinda uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, leo angekua Ikulu Dodoma ama Dar es Salaam akizungukwa na wasaidizi makumi kwa makumi wanaomnyenyekea kwa heshima, na kumfanyia kila analotaka.

Angekuwa anapigiwa saluti na kupigiwa mizinga kwenye dhifa kubwa mbalimbali za kitaifa. Lakini kubwa zaidi angekuwa jicho la bajeti ya nchi na kuwa sehemu ya kuamua itumikaje. Bajeti ya shilingi trilioni 31 ya mwaka wa fedha 2021/2022 ingekuwa chini yake akiisimamia na kuitekeleza kwa namna yake.

Angewapangia wafanyakazi wa umma walipwaje mishahara hata ushawishi wake kwa hilo ungewagusa pia wabunge wanaopitisha bajeti za Serikali. Mishahara yao ingetokana na utashi wake licha ya mamlaka ya kikatiba ya bunge iliyonayo katika kuisimamia serikali.

Pengine trilioni 9.7 ya mishahara iliyopangwa kutumika kwa mwaka ujao wa fedha wa serikali unaoanza mwezi Julai,2022 angeweza kuifanya atakavyo. Angeamua hata kujilipa mshahara wa shilingi milioni 50 kwa mwezi na posho ya shilingi 100mil kwa mwezi, pamoja na kujipangia safari za posho kila siku kutengeneza masurufu asingefanywa lolote kisheria, sana sana kungeibuka manung'uniko na makelele ambayo angeyapuuza na kuendelea na hamsini zake.

Lakini imekuwa tofauti, kwa Tundu Lissu, mwanasiasa mahiri wa upinzani mahiri, aliyekuwa mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni na mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha CHADEMA katika uchaguzi wa 2020. Kwa karibu miaka mitatu, amekua akisotea stahiki zake kibunge kutokana na kuvuliwa ubunge.

'Kutokulipwa stahiki hizi kuliniletea usumbufu mkubwa sana. Nilishtakiwa na benki kwa kushindwa kulipa deni lao, kwa sababu deni hilo lilikuwa linalipwa kwa makato ya mshahara wangu wa ubunge. Na ni wazi nilishindwa kulipia matumizi yangu mengine binafsi kwa sababu ya kunyimwa stahiki hizo', Lissu ameiambia BBC.

Nini Kilitokea?

Safari ya maslahi ya Tundu Lissu, ambaye ni makamu mwenyekiti wa CHADEMA, ilianzia Dodoma Septemba, 2017 alipopigwa risasi zaidi ya 10 na watu wasiojulikana. Alijeruhiwa vibaya na alikimbizwa Nairobi kwa matibabu kisha Brussels Ubelgiji toka mwezi Januari mwaka 2018. Na tangu wakati huo hajarejea rasmi Tanzania, licha ya kuja kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kurudi tena Ubelgiji.

Kutoonekana kwake bungeni kwa miaka karibu miwili, kukamfanya aliyekuwa spika wa bunge hilo Job ndugai, kulitangazia bunge la nchi hiyo, Ijumaa Juni 28, 2019 kuwa ameiandikia tume ya uchaguzi ya nchi hiyo, NEC kuileleza kuwa jimbo la Singida Mashariki, lililokuwa likishikiliwa na Lissu kupitia chama kikuu cha upinzani Chadema lipo wazi.

Hatua hii ilikuja baada ya Mbunge wa Geita vijijini Joseph Msukuma kutoa hoja bungeni kuhoji uhalali wa Tundu Lissu kuendelea kupata mshara huku akiwa hahudhurii vikao kwa sababu ambazo hazijulikani.

Spika Ndugai alitaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi barua hiyo, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.

Lakini Lissu alizipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.

"Mimi si mtoro bungeni na sijawahi kuwa mtoro. Kilichonikuta kinajulikana, nilipigwa risasi 16 nikiwa natoka bungeni Septemba 7, nikaletwa nje kwa matibabu. Tangu hapo nipo nje natibiwa," amesema Lissu na kuongeza, "Kwanza walionishambulia mpaka sasa hawajulikani, hakuna aliyekamatwa. Leo inasemwa sijulikani nilipo navuliwa ubunge... kinachoendelea si ajabu, kuna watu hawana maarifa tena, walichobaki nacho ni mabavu tu."

Kabla ya kutangaza hatua hiyo ya kuvuliwa ubunge, Mwezi Februari, 2019, Spika Ndugai alikubali kufanyia kazi hoja ya kuzuia stahiki za Lissu ikiwemo mshahara kwa madai hayo, na kusema kuwa hana taarifa rasmi juu ya alipo Lissu na hali yake ya kiafya, na amekuwa akimuona kwenye vyombo vya habari.

Lissu alikuwa akionekana katika vyombo vya habari vya Ujerumani, Marekani na Uingereza likaibua mjadala kwa wakosoaji wake, wakimuona ni kama amepona na angepaswa kuwa bungeni.

Je msimamo wake ulikoleza majibizano ya stahiki zake?

Lissu ni mwanasheria, anayeendesha siasa za kiharakati zenye msimamo wa anachokiamini, hakuogopa kuukosoa utawala wa Rais John Magufuli wala utawala wa bunge chini ya Spika Ndugai. Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliopendelea kumuita Magufuli kuwa 'Dikteta Uchwara' ama kwa lugha ya kingereza 'Petty Dictator'.

Wakati anashambuliwa kwa risasi, Lissu hakuwa tu mnadhimu wa kambi rasmi bungeni Tanzania bali pia raisi wa chama cha wanasheria nchini humo. Pengine msimamo wake ulimfanya kukosana na mamlaka. Hata Hivyo uamuzi wa kuzuia stahiki zake, kwa mujibu wa Ndugai ulizingatia sheria.

"Hawa watu wana hofu juu yangu, wana hofu juu ya Septemba 7 siku nitakayorudi Tanzania. Hakuna cha kunizuia kurudi," alisisitiza Lissu wakati huo.

Kwenye waraka wake kwa njia ya video alioutoa mwezi Machi, 2019 Lissu alisema uamuzi wa kumfutia mshahara na posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa, awe anaumwa au mzima, awe amehudhuria vikao vya Bunge au hajahudhuria, ni uthibitisho mwingine wa ukiukaji wa Katiba, Sheria na taratibu.

''Nje ya Katiba na Sheria ya Uendeshaji wa Bunge, namna pekee ambayo mshahara na posho za kibunge unaweza kuathiriwa kihalali ni kwa Mbunge kusimamishwa na Bunge kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kukiuka maadili ya Bunge'', Alieleza Lissu na kuongeza kuwa mshahara na posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa kila mwezi sio fadhila bali ni haki ya kikatiba na kisheria ya kila mbunge wa Tanzania. Maoni ya wengi kuhusu stahiki za Lisuu ikiwemo gharama za matibabu ni kama bunge lilimtelekeza Lissu.

Kauli hii ikamuibua tena Spika Ndugai, aliyewaambia waandishi wa habari 'Naomba mumuulize Lissu swali hili, kama muajiri hajakupa mshahara unaoudai je, unakimbilia kwenye mitandao ya kijami au utazungumza na muajiri wako kwa taratibu zilizowekwa'. Spika Ndugai aliliambia bunge pia kuwa si kweli kuwa chombo hicho kimtelekeza Lissu.

Tangu wakati huyo wa majibizano hayo ya kistaha kuhusu stahiki zake, Lissu aliendelea kusimamia msimamo wake kwamba anastahili kulipwa stahiki hizo kwa kulituikia bunge la 11 kuanzia mwaka 2015. Februari, 2022 hatimaye alikutana na Rais Samia Suluhu na kumfikishia suala hilo kati ya masuala matano makubwa alipokutana naye rais Samia alipkwenda Ubegiji kwa ziara ya kikazi.

'rais ameonyesha ukomavu wa kisiasa, ameonyesha utu, Tundu alipigwa risasi dunia nzima inajua, alikuwa mbunge dunia nzima inajua, stahiki hizi alipaswa kutozililia, alipaswa kulipwa tu, alisema Zainabu Nassib, mkazi wa Dar es Salaam.

Lakini kwa nini Lissu asotee stahiki zake kwa kiwango hiki?

Kwa muktadha wa kisheria, hakuna aliye juu ya sheria, na utawala wa sheria unataka sheria kusimamia utendaji wa masuala na shughuli bila kujali aliyepewa mamlaka ya kuitekeleza na kuisimamia sheria. Wapo wanaojiuliza kama Mgombe urais, mbunge, mwanasiasa na mwanasheria mbobezi, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni anasotea maslahi na stahiki zake kwa namna hii, vipi kuhusu mwalimu wa shule ya msingi Ilonga, Kilosa au afisa kilimo wa Tunduru?

Wadadisi na wachambuzi, wanaona ukakasi wa utekelezaji wa utawala wa sheria kwa baadhi ya watendaji kwenye mamlaka mbalimbali kutokana na muelekeo wa siasa uliokuwepo.

'wakati huo siasa zilikuwa na muelekeo mwingine, lile usiloliwaza kutokea liliweza kutokea hata kama lilikuwa lina mashaka, sheria zilikuwa na nguvu za wastani kuliko utashi wa mtu,' anasema Beatrice Kimaro, mchambuzi wa siasa Tanzania.

Kuhusu fedha matibabu Lissu alisema ameambiwa aandike barua na mamlaka za ulipaji ili alipwe, "nimeshaiandaa kukamilika kwa kiasi kikubwa, ingawa bado natafuta nyaraka kwa sababu nimetibiwa Kenya na Ubelgiji."

"Kwa hiyo naweza nikasema hadharani kwamba (kuhusu stahiki zake) limefanyiwa kazi na ni jambo jema kwa kweli. Sina madeni ya benki na usumbufu niliokuwa nikiupata," alisema Lissu kupitia mtandao wa Club House.

Kiasi gani alicholipwa Tundu Lissu na tafsiri yake ni nini?

Tangazo la Spika Ndugai la Mwezi Februari,2019 lilimaanisha stahiki zote za Lissu, ukiwemo mshahara wake umesitishwa kulipwa kuanzia wakati huo.

Ndugai alidai kuwa hadi mwishoni mwa Desemba 2018, Lissu alikuwa amelipwa Sh207.8 milioni pamoja na Sh43 milioni zilizotolewa kama mchango wa matibabu yake na wabunge wenziwe na kufanya jumla kuu ya fedha alizolipwa kuwa Sh250milioni.

Hata hivyo, Lissu alimjibu Ndugai wakati huo na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema bunge la Tanzania halijawahi kutoa hata senti moja kugharamia matibabu yake ingawa alikiri kupokea Sh43 milioni zilizotolewa na wabunge wenzake kama mchango wao na kwamba kiasi kingine alicholipwa kinachofanya jumla ya fedha hizo kufikia Sh250 ni mishahara na stahiki zake, lakini siyo gharama za matibabu.

Msoto huu ulimfanya Lissu kufikishwa mahakamani na benki inayomdai na kupata usumbufu mwingine wa mahitaji wa maisha, lakini sasa anakiri hadharani kulipwa stahiki zote kama mbunge na kilichosalia sasa ni gharama za matibabu.

BBC imemuuliza Lissu kuhusu swali hili 'sijaambiwa kiasi kamili isipokuwa nimeambiwa ni takriban shilingi milioni 79. Sehemu kubwa imelipwa benki ambako nilikuwa nadaiwa mkopo wa gari', alisema Lissu na kuongeza 'nimeambiwa kuna 'balance' ya takriban shilingi milioni 9 ambayo wananisubiri nifufue akaunti yangu ya NMB ili wazitume huko', alisema Lissu.

Kuhusu tafsiri ya malipo haya Lissu, alisema 'tafsiri ya malipo haya ni kwamba Rais Samia ameanza kurekebisha dhuluma niliyofanyiwa na mtangulizi wake. Ameahidi pia kunilipa na gharama za matibabu ambayo nilinyimwa na Magufuli'.

Lissu anasema 'haya yote ni mambo mema kwangu binafsi na kwa umma pia. Yanaonyesha kwamba Rais Samia anatambua dhuluma za nyuma na yuko tayari kuzirekebisha'.

Kulipwa kwa stahiki za Lissu sasa baada ya karibu miaka mitatu kunaibua mjadala mpya, Je usikivu wa Rais Samia aliyemuomba kushughulikia hilo au mamlaka zilizopita hazikutii sheria ya kumpa stahiki zake?

Taarifa zaidi kumhusu Tundu Lissu: