Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Chadema yahoji uhalali wa wabunge 19 kusalia bungeni
Chama cha upinzani nchini Tanzania, kimehoji uhalali wa waliokuwa wanachama 19 wanawake wa chadema kusalia bungeni baada ya kuvuliwa uanachama.
Naibu Katibu wa chadema upande wa Tanzania Bara, Benson Kigaila ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu sakata la waliokuwa wanachama wa chama hicho. (Halima Mdee na wenzake 18).
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliamuru suala la ubunge wa waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) na wabunge wa Viti Maalum, waliovuliwa uanachama wa chama hicho, liendelee kubakia kama hali ilivyo kwa sasa mpaka hapo maombi yao ya zuio la kuvuliwa ubunge huo yatakaposikilizwa.
Kwa uamuzi huo kwa sasa wabunge hao, Halima Mdee na wenzake 18 watendelea kushiriki vikao vya Bunge kama kawaida hadi maombi yao hayo yatakaposikilizwa Juni 13.
Uamuzi huo ulitolewa Jumatatu na Jaji John Mgetta kutokana na maombi yao waliyoyawasilisha mahakamani hapo baada ya chama hicho kuwavua uanachama.
Wabunge hao walivuliwa rasmi uanachama wa chama hicho, usiku wa kuamkia Mei 12, 2020, baada ya Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao walizozikata wakipinga uamuzi wa Kati Kuu iliyowavua uanachama.
Baraza Kuu la Chadema, ambalo ndilo chombo cha juu kabisa cha maamuzi ya Chadema lenye uamuzi wa mwisho katika kikao chake hicho liliunga mkono, uamuzi wa Kamati Kuu.
Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uanachana Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum kinyume cha utaratibu wa chama.
''Kwa maana hiyo hatukutambua jimbo moja tulilotangazwa nalo kwamba tumeshinda, viti 19 ambavyo tulipewa kuwa viti maalumu wala hatukutambua ruzuku ya sh milioni 107 ambayo tulitangazwa kuwa tulistahili''. Alisema Bw. Kigaila.
Kwa mujibu wa Kigaila,msimamo huo chadema kupitia kamati kuu yake haikuwahi kuteua mtu yeyote kuwa mbunge wa viti maalumu.
''Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika hakuwahi kuandikia Tume ya Uchaguzi barua ya uteuzi wa wabunge wa viti maalumu.
Kamati kuu ilikaa kikao cha dharura ili kushughulikia suala hili la dharura na watu ambao wameamua kwenda kuapa bungeni kwa jina la chadema wakiwa hawajachaguliwa na chadema''
''Kikao kililenga kuwauliza imekuwaje, mamlaka mmetoa wapi na nani amewapeleka ili kufanya hivyo Katibu Mkuu aliwaandikia wote 19 barua za kuwaita ili waieleze Kamati Kuu lakini hawakwenda.
''Pamoja na kukata rufaa kwao dhidi ya uamuzi wa kuvuliwa uanachama haikua tiketi ya wao kubaki bungeni , kwani utaratibu unamtambua mtu kuwa mbunge pale anapokuwa mwanachama hai wa chama cha siasa''. Alisema Kigaila.