Mauaji ya Kimbari : Protais Mpiranya afariki dunia baada ya kujificha kwa muda mrefu

Chanzo cha picha, AFP
Kifo hiki kimethibitisha meja wa mwisho wa Rwanda aliyeshtakiwa na mahakama ya uhalifu wa kivita kwa jukumu lake katika mauaji ya kimbari ya 1994.
Protais Mpiranya alikuwa mkuu wa walinzi wa rais na alituhumiwa kuamuru mauaji ya Waziri Mkuu wa wakati huo, Agathe Uwilingiyimana.
Maafisa wake pia waliwaua walinda amani 10 wa Umoja wa Mataifa wa Ubelgiji waliokuwa wakimlinda.
Wachunguzi walimtafuta hadi Zimbabwe, ambako kaburi lililofukuliwa hivi karibuni lilithibitisha kuwa alifariki mwaka 2006.
Waligundua kuwa Mpiranya alitumia washirika mbalimbali wakati akikimbia kukwepa kukamatwa kwa zaidi ya miaka 12.
Mara tu baada ya mauaji ya kimbari - ambapo Watutsi wapatao 800,000 wa kabila la Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa na Wahutu wenye msimamo mkali katika siku 100 - alihamia Cameroon.
Wengine wanaotuhumiwa kushiriki katika mauaji ya kimbari walikuwa wametoroka mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuunda kundi la waasi linalojulikana kama FDLR.
Mpiranya alijiunga nao mwaka wa 1998, akiongoza kikosi kilichopigana pamoja na jeshi la Zimbabwe, ambalo lilikuwa limeingia katika mzozo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaohusisha mataifa kadhaa ambayo mara nyingi yanaitwa "vita vya dunia vya Afrika".

Chanzo cha picha, AFP
Alijiasili jina la Alain Hirwa na kujulikana kama "Kamanda Alain" - na aliheshimiwa sana na maafisa wakuu wa Zimbabwe, uchunguzi uligundua.
Ni washirika wake wa Zimbabwe ambao walipanga kumuhifadhi katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, baada ya kushtakiwa kwake kuwekwa hadharani mwaka 2002 na mahakama ya kimataifa iliyoundwa ili kuwafikisha mahakamani wale waliohusika na mauaji ya Kimbari.
Alishtakiwa kwa makosa manane, yakiwemo mauaji ya kimbari na ubakaji, kwa "kutoa amri, kusimamia, kuhimiza, na kusaidia uhalifu" uliotekelezwa na walinzi wa rais.
Uchunguzi "ulio na changamoto kubwa" ya kumtafuta ulifanywa na chombo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita za Rwanda na Yugoslavia.
"Kwa waathirka wa uhalifu wake, Mpiranya alikuwa mkimbizi wa kuogopwa na maarufu, kiongozi wa walinzi wa rais wakati wa mauaji ya kimbari na baadaye kamanda mkuu wa FDLR," mwendesha mashtaka wa International Residual Mechanism for Criminal Tribunals (IRMCT), Serge alisema. Brammertz.
"Kuthibitisha kifo chake kunatoa faraja ya kujua kwamba hawezi kusababisha madhara zaidi."
Kulingana na IRMCT, katika miaka yake minne nchini Zimbabwe, Mpiranya alifanya biashara na shemeji yake na bado alikuwa na uhusiano na washirika wa FLDR - na alikuwa na pasipoti ya Uganda chini ya jina la James Kakule.
Mkewe na binti zake walienda kuishi Uingereza, lakini walimtembelea Harare.
Alipougua sana mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 50, akiwa na kifua kikuu alikuwa akitumia jina Ndume Sambao - na hili lilikuwa jina kwenye kaburi lake alipozikwa kwenye makaburi nje ya Harare.
"Tangu Oktoba 2006, familia ya Mpiranya na washirika wake wamejitahidi sana kuficha kifo chake na mahali alipozikwa," IRMCT ilisema.
"Wamerudia mara kwa mara kutoa taarifa za uongo kwa wachunguzi, na kuwafundisha wale waliojua uwepo na kifo cha Mpiranya huko Harare kusema uwongo wakiulizwa.
Jiwe katika kaburi lake liliwekwa kwa makusudi kuzuia ugunduzi wake."

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalifanyikaje?
Tarehe 6 Aprili 1994, ndege iliyokuwa imembeba Rais wa wakati huo Juvenal Habyarimana - Mhutu - ilidunguliwa na kuwaua wote waliokuwa ndani.
Wahutu wenye itikadi kali walilaumu kundi la waasi la Kitutsi, Rwandan Patriotic Front (RPF), ambalo lilikanusha shutuma hizo.
Katika kampeni iliyoandaliwa kwa umakini ya kuchinja, wanamgambo walipewa orodha ya waanga wa Kitutsi. Wengi waliuawa kwa mapanga katika vitendo vya ukatili wa kutisha. Jitihada kidogo sana ilifanywa kimataifa kukomesha mauaji.
Hatimaye RPF, ikiungwa mkono na Uganda, iliandamana hadi mji mkuu Kigali. Baadhi ya Wahutu milioni mbili walikimbia, haswa kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Makumi ya Wahutu walitiwa hatiani kwa kuhusika katika mauaji na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya Rwanda, yenye makao yake nchini Tanzania, na mamia ya maelfu ya wengine walikabiliwa na kesi katika mahakama za jamii nchini Rwanda.

Zaidi kuhusu Kimbari:












