Nini maana ya hatua ya kutimuliwa kwa Wabunge 19 wa Viti Maalumu CHADEMA?

Wabunge 19 waliofukuzwa uanachama Chadema
    • Author, Beatrice Kimaro
    • Nafasi, Mchambuzi, Tanzania
  • Iliyochapishwa

Baraza kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, jana limethibitisha uamuzi wa kamati kuu ya chama hicho cha upinzani Tanzania na kuwavua uanachama wabunge 19 wa viti maalumu wanawake.

Wabunge hao wanawake walifukuzwa uanachama Novemba 27, 2020 baada ya kwenda kuapishwa bungeni kuchukua nafasi 19 za viti maalumu ambazo zilisusiwa na CHADEMA.

Ni nafasi zilitokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Sababu za kususa ilielezwa ni kupinga utaratibu na mchakato mzima wa uchaguzi huo uliomuweka madarakani aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli.

Mwezi mmoja baada ya kufukuzwa kwao walikata rufaa Baraza kuu la chama, kupinga uamuzi wa kamati kuu wa kuwafukuza. Sasa ikiwa ni miezi karibu 18 imepita, Baraza kuu linakubaliana na uamuzi wa kamati kuu na kubariki kufukuzwa kwao. Swali kubwa: uamuzi huu wa sasa wa Baraza Kuu unamaanisha nini?

Ubunge wao 'Rehani'

Ibara ya 71 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza yanayoweza kumfanya Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukoma kuwa mbunge.

Kipengele kidogo cha (e) cha Ibara hiyo kinaeleleza iwapo mbunge atakoma kuwa mwanachama wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge, basi atapoteza ubunge wake.

Kwa uamuzi huu wa Baraza Kuu, inamaanisha kuwa wabunge hao watapoteza nafasi zao za Ubunge, kama Chama hicho kitawasilisha taarifa rasmi kwa Spika wa Bunge kuhusu uamuzi wa Baraza hilo.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amethibitisha kuwa hatua inayofuata sasa ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuandika barua ya kumtaarifu Spika wa Bunge la Tanzania kuhusu uamuzi uliofanywa na baraza kuu kwa hatua zaidi.

Wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema

Hatua yenyewe anayoizungumza hapa Mrema ni kuvuliwa ubunge kwa wanachama hao kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Halima Mdee, akizungumza baada ya kutimuliwa kwao, alionyesha hajakubaliana na uamuzi wa Baraza kuu akiuita ni uamuzi uliojaa uhuni.

'Sikujua kama chadema kunaweza kufanyika uhuni wa kiwango hiki, mimi ni Chadema nitaendelea kuwa chadema vizuri, lakini kilichofanyika ni uhuni wa kiwango cha hatari'

Halima alisema ataongea wakati mwingine kuhusu hatma yao na uamuzi watakaouchukua baada ya uamuzi wa Baraza kuu la Chadema.

Wabunge hao wana nafasi nyingine ya kukata rufaa?

Mchakato wa kutimuliwa na kukata rufaa kwa wabunge hao umeigusa pia Ibara ya 5.4.3 ya Katiba ya Chadema inayoelezea mchakato wa kukoma uanachama na nafasi ya kukata rufaa. Kama ilivyo kwa katiba nyingi, Katiba ya chadema imetoa pia fursa ya mwanachama kukata rufaa kwa ngazi ya juu kama hakuridhika na adhabu za ngazi za chini. Je kwa hatua ya sasa wanayo nafasi ya kufanya hivyo?

'Kwa utaratibu wa kichama, sidhani kama wanayo nafasi tena, labda nje ya chama', anasema Salim Amin ambaye kwasasa yupo Ujerumani mmoja wa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, Baraza kuu ndicho chombo kikuu cha maamuzi cha chama. Rufaa ya wabunge hao kugonga mwamba kwenye baraza hilo, maana yake kwa mifumo ya chama, hawana tena nafasi ya kukata rufaa ya kuvuliwa uanachama wao.

'hawana tena nafasi ya kukata rufaa, kwa sababu mamlaka yao ya mwisho ya kukata rufaa ilikuwa ni Baraza kuu. Kwa hiyo hawana ngazi nyingine ya kwenda, kwa upande chama tumemalizana nalo kwa utaratibu huo', anasema Mrema, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Chadema.

Ipo fursa nje ya chama ambapo wanasheria na wachambuzi wa siasa na demokrasia Tanzania wanaona wabunge wao 19 wanaweza kuitumia kutafuta haki yao, kama wataona imeminywa katika ngazi ya Baraza kuu

Ingawa mkutano mkuu wa chama kwa mujibu wa katiba ya chama, unajukumu la kuzingatia na kutoa uamuzi juu ya masuala ya kinidhamu yanayowasilishwa na Baraza Kuu.

'kupitia mkutano Mkuu sioni kama unaweza kwenda tofauti na maamuzi ya baraza kuu, nafasi yao ni finyu sana, nadhani fursa kubwa ni ile ya kwenda mahakamani', anasema Amin na kuongeza 'japo watahitaji msingi mzuri wa hoja, ila Mahakama inaweza kuwapa haki ikiridhika kukiukwa kwa utaratibu wa kufukuzwa kwao, lakini hoja, hata kama watarejeshewa na mahakama uanachama wao, watawezaje kufanya kazi na wanachama wenzao ambao wamewapigia kura hawawataki?

Je nani kupata hasara kati ya Chadema na wabunge hawa 19 'waliotimuliwa?

Wabunge hawa wa viti maalumu waliotimuliwa ni kama 'Siagi' wanawake wa chama hicho. Wengi walikuwa na nafasi kubwa kubwa ndani ya chama, na ni vinara waliokuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama.

Kufukuzwa kwako ndani ya chama, kwa namna yoyote, kunakiondolea na kukipunguzia chama hicho wanawake wanasiasa wenye nguvu na ushawishi ndani ya chama na nje ya chama.

Mchambuzi wa siasa Tanzania Rashid Abdallah akizungumzia athari za kuwafukuza wanasiasa hawa ni 'namna ya kuonesha kwamba chama hakivumilii wale wanaohesabiwa kuwa wasaliti'.

Pamoja na hilo anaongeza kuwa 'upinzani hautokufa kwa kuondoshwa hao. Utaendelea kubaki ukiwa dhaifu katika ngome ya wanawake. Upande pekee utakaonufaika na hilo ni chama tawala; ngome ya wanawake iliyokuwa ikiwasumbua hatimae imedondoshwa, anasema kwenye moja ya makala zake.

Kwa mantiki hii, chama kinatakuwa na jukumu la kujenga upya ngome ya wanawake, kazi ambayo imeonekana kuanza kwa kuwa na uongozi mpya wa Baraza la wanawake Chadema (Chadema).

Kwa wabunge hawa, hasara kubwa kwao ni kupoteza ubunge kama Spika ataridhia taarifa ya kufukuzwa kwao, watapoteza mafao yao, lakini pia watakuwa na jukumu kubwa la kujijenga upya kisiasa kupitia chama kingine, ama kama wataweza kuomba msamaha na kusamehewa kurejea Chadema.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe

Je Spika wa sasa kuutafuna 'mfupa' uliomshinda Ndugai?

Tangu mwaka 2020, wabunge hawa waliotimuliwa 'walikingiwa' kifua na aliyekuwa spika wa wakati huo, Job Ndugai, kwa maelezo kwamba, Chadema haikufuata utaratibu katika kuwavua uanachama.

Waliendelea kukaa bungeni kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu, licha ya Chadema wenyewe kuwakana kutowatambua na kutojua nani aliyewateua na kupeleka majina yao bungeni.

Kama Spika wa sasa Tulia Ackson atapokea na kuifanyia kazi taarifa ya Katibu mkuu wa chadema, Mnyika, basi wabunge hao watavuliwa ubunge rasmi.

Chadema sasa italazimika kupeleka majina mengine kulingana na utaratibu wa chama kama Spika atawavua ubunge.

Alipoulizwa Mrema, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Chadema, endapo chama hicho kimejiandaa kuteua majina mengine 19 kuziba nafasi za wabunge hawa waliotimuliwa alisema, 'Suala la kuteua wabunge wengine au kutokuteua wabunge wengine ni uamuzi utakaokuja kulingana na hii michakato mingine'.

Kwa mujibu wa Katibu na utaratibu wa chama hicho Mchakato wa kuteua wabunge unafanywa na kamati kuu ya chama hicho.

Mapema mwezi Februari, Spika Tulia Ackson alieleza kusubiri maamuzi ya Baraza kuu la Chadema kabla ya kusema ama kuchukua hatua yoyote, lakini kwa wakati huo wabunge hao walikuwa halali, na suala wamefikaje bungeni lilikuwa suala ambalo walipaswa kuuliza tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).

Mrema anaendelea kusisitiza kuwa 'hawa wabunge tuliowafukuza leo, hawakuwahi kuteuliwa na chama chetu hawakuwahi kiuandikiwa barua na katibu mkuu wa chadema. Katibu mkuu wa chadema hakuwahi kujaza fomu namba 12 C akaipeleka tume ya taifa ya uchaguzi, wao wanajua fomu walijaziwa na nani, waliteuliwa na nani, ndo maana tumefanya huo uamuzi, alisema Mrema na kuongeza sasa suala hilo litakuwa mikononi mwa Spika.

Wengi sasa wanajiuliza Spika Tulia ataweza kuutafuna mfupa uliomshinda Ndugai na kuwavua ubunge wabunge hao wanawake wakuteuliwa? Ni jambo la kusubiri.