'Elimu ya Tanzania inachangia ukosefu wa ajira'

M
Iliyochapishwa

'Nitawezaje kupata kazi wakati kila tangazo linaandika ujuzi miaka mitatu , ujuzi miaka mitano...' huyo ni kijana wa Kitanzania ambaye anaonekana kukata tamaa kusambaza bahasha za rangi ya kaki katika maofisi mbalimbali.

Na sasa anasema ili aweze kutuma barua za maombi ya kazi lazima awe na intaneti ya kutosha, hiyo ni gharama nyingine tena.

Yeye amemaliza chuo kikuu tangu mwaka 2019, na mpaka leo hajapata ajira.

Anasema alikuwa anafanya vizuri sana darasani na hata vyeti vyake vinathibitisha hilo lakini bado upatikanaji wa ajira ni suala ambalo hajui kesho yake.

Huyo ni mmoja kati ya vijana wengi ambao wamehitimu viwango mbalimbali vya elimu nchini Tanzania na hawajapata ajira.

Kwa mujibu wa Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni mbunge wa jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam amezua gumzo nchini Tanzania baada ya kuja na hoja kuwa tatizo la ajira nchini humo linatokana na mfumo wa elimu kupitwa na wakati.

Prof.Mkumbo anasema ni wakati sasa kwa rais kuchukua hatua na kufanya mabadiliko katika mfumo wa elimu ili kuwawezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa.

Anasema mfumo uliopo hauwafundishi wahitimu ujuzi wala stadi zozote za kujitegemea kimaisha, badala yake umelenga kumwezesha mwanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi inayofuata.

Mfano mwanafunzi akimaliza darasa la saba akiwa na miaka 13, mfumo utakuwa umemfanya amalize akiwa na maarifa ya historia au jiografia nini na akimaliza sekondari mambo ni yale yale pia.

Mwanafunzi anamaliza shule bila ya kuwa na maarifa, ujuzi wala stadi za maisha, hivyo akikwama katika ngazi moja ni ngumu kusimama katika hatua nyingine ya maisha ya kuweza kiujitegemea au kujiajiri.

Mfumo uliopo sasa nchini Tanzania unaanza kutoa ujuzi mpaka mtu afike chuo kikuu au vyuo vya ufundi. Na hivyo kupelekea wengi kumaliza chuo bila ajira wala uwezo wa kujiajiri.

vijana

Wakati , mwenyekiti wa taasisi ya Haki Elimu Dkt. Wilberforce Meena anasema ukiangalia mfumo wa elimu kwa sasa haswa upande wa mtaala ambao unaongoza elimu inayotolewa katika nchi mbalimbali.

Nchini Tanzania kumekuwa na jitihada mbalimbali za kuboresha mitaala ya ellimu , ili mitaala inayotolewa iendane na mahitaji ya wakati huu.

Huko nyuma kulikuwa na jitihada mbalimbali kwa mfano Tanzania ilianzisha elimu ya kujitegemea katika miaka ya 60 kwa lengo la kuwa na elimu inayoendana na mila na destori na maisha halisi ya Tanzania.

Kuna wakati kulikuwa na azimio la musoma ambapo walikuja na kuwa na elimu iendane na soko la ajira.

Miaka ya 2000, katika shule za msingi kulikuwa na mabadiliko ya mtaala kutoka mtaala wa maudhui au maarifa kwenda kwenye mtaala wa kulenga umahiri.

Ni kawaida kwa nchi kufanya mabadiliko ya mifumo yake ya elimu ili iendane na nadharia inayotumika pia katika nchi za Magharibi, mfano mtaala wa magharibi unashuhudiwa kuwa unatekelezwa katika kuwa na maandiko mazuri lakini hakuna vitendo au utekelezaji, shuleni na vyuoni hakuna uhalisia.

Hata hivyo Dkt. Meena anaona ni vyema kufanya mabadiliko lakini jambo muhimu ni kuwa na maandalizi ya kutosha.

Kwa uzoefu wake Dkt.Meena anasema "Kumekuwa na mipango mizuri sana lakini tunapata maandiko bila utekelezaji.

Wadau hawajaandaliwa vya kutosha na hakuna vifaa vya kutosha."

Dkt.Meena ameongeza kusema kuwa Mwaka 2015, darasa la kwanza na la pili kulikuwa na mabadiliko makubwa ya mtaala huku walimu wakiwa hawajaandaliwa , vitabu na matokeo yake walimu walirudi katika mfumo wake wa zamani.

Wakati hayo yanajiri nchi ya jirani ya Kenya , wao wamefanya mabadiliko makubwa ya mtaala na hali bado ni vute nikuvute.

Nchini Kenya mnamo Januari 2017 iliamua kusitisha mtaala wa zamani wa 8-4-4 (miaka 8 katika shule ya msingi, miaka 4 ya sekondari, miaka 4 katika elimu ya juu) na kupeleka kwenye 2-6-3-3. yaani miaka miwili shule ya awali, miaka sita shule ya msingi, miaka sita sita sekondari unaowiana na mpango wa Kenya wa Dira ya 2030 wa maendeleo. Majaribio yalianza Mei 2017 na mtaala mpya kuanzia darasa la awali hadi la 3 umetekelezwa kwa mipango ya kutekeleza kikamilifu huku mtaala ukiwa unabadilishwa kwa hatua mbalimbali.

Na malalamiko yakiwa yanatoka kwa wadau kuhusu maandalizi ya kutosha kuanzia walimu , wazazi , watengeneza vitabu na wadau wengine.

Swali la Dkt.Meena ni Je, mtaala mpya unaweza kufanya kile kitakachokusudia katika kuboresha elimu? Kwenye karatasi hakika inaonekana hivyo, lakini ukweli unasimulia hadithi tofauti.

Ni muhimu kujiandaa zaidi ili kupata mafanikio.

Wakati mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge, Stansilous Nyongo anasema wameweza kushauri serikali kuitisha mijadala ya kitaifa kwa kuangalia kule tulipotoka, tulipo na tunapoenda.

Na hii inatokana na hali halisi iliyopo ambapo vijana wengi hawana ajira , je nini kitafanyika baada ya kuona kilichopo na mjadala umeanza.