Nini maana ya kufunguliwa kwa magazeti yaliyofungiwa Tanzania?

Chanzo cha picha, Tanzania Daima
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Pengine kuliko waziri mwingine yeyote katika Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ilisadifu kwamba hatua ya kufungulia magazeti manne yaliyofungiwa wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, imetangazwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.
Katika baraza lote la Rais Samia, hakuna waziri mwenye mahusiano ya karibu na wanahabari wengi wa vyombo vikubwa vya Tanzania kumzidi Nape.
Uhusiano wake huo umejengwa taratibu kwa takribani miaka 15 sasa - kuanzia akiwa kiongozi kwenye Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Katibu Mwenezi wa CCM na baadaye akiwa waziri wa wizara hiyohiyo wakati wa utawala wa Rais John Magufuli.
Wakati Magufuli akianza sera za kuvibana vyombo vya habari vilivyokuwa vikimkosoa, Nape alikuwa ndiye 'bakora' yake. Kati ya magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa, mawili yalifungwa kwa Saini ya Nape mwenyewe -Mawio na Mseto yaliyofungiwa Januari na Agosti 2016 mtawalia.
Gazeti la Tanzania Daima lilifungiwa Juni mwaka 2020 wakati Waziri wa Habari akiwa Dk. Harrisson Mwakyembe. Gazeti lingine ambalo limenufaika na kufunguliwa kwa magazeti kulikotangazwa na Nape wiki hii ni MwanaHalisi ambalo kimsingi lilianza kufungiwa mwaka 2012 wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na suala likawa linapigwa danadana kuanzia mwaka 2015 wakati adhabu yake ya kifungo cha miaka mitatu ilipomalizika hadi sasa.

Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, Nape alitamka kwamba zama zimebadilika na kwamba yaliyotokea huko nyuma yamepita.
Faida pekee aliyonayo Nape ni kwamba inajulikana kwamba maamuzi ya kuyafungia magazeti yalikuwa nje ya uwezo wake na kama ukweli utasemwa kama ulivyo - naye alikuwa mmoja wa waathirika wa utawala wa Magufuli; akiondolewa kwenye uwaziri na kutishiwa maisha hadharani.
Jambo moja ambalo linaonekana wazi katika hatua hii mpya ya serikali ni kwamba zama zimebadilika. Ingawa Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Magufuli ukweli ni kuwa wawili hao ni wanasiasa wa aina mbili tofauti.
Katika siku zake za mwanzo kwenye urais, Samia alizungumzia gharama kubwa ambazo yeye na ndugu zake walikuwa wanachangishana kuendesha kituo cha televisheni cha mitandaoni walichoanzisha.

Huu ni ushahidi kwamba yeye binafsi - walau katika ngazi ya watu wake wa karibu, alikuwa akisikia vilio na masimulizi ya wanahabari moja kwa moja. Uamuzi wa kufungulia magazeti aliutangaza yeye mwenyewe Januari mwaka huu ingawa wasaidizi wake serikalini walitoa kauli kuonyesha kwamba kufungulia magazeti yaliyofungiwa ni jambo la kiutaratibu linalohitaji kuondolewa pia kwa kufuata kiutaratibu.
Wakati Magufuli anamteua Nape kwenye sekta ya habari, ilitarajiwa kuwa lengo lilikuwa ni kufungua mahusiano mapya na wadau wa sekta hiyo ingawa hali ilikuja kuwa tofauti baadaye.
Hatua ya Samia kumrejesha mbunge huyo wa Jimbo la Mtama kwenye wadhifa huo - ingawa jina la wizara limebadilika, inaonekana ina lengo lile lililodhaniwa wakati wa mtangulizi wake.
Matarajio ya wengi ni kwamba kitendo cha kufungulia magazeti ni hatua ya kwanza tu katika hatua nyingi zinazotakiwa kufuatwa ili kurejesha hadhi, heshima na wajibu wa vyombo vya habari katika nchi inayoendeshwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.
Kama kufungulia magazeti manne ni hatua ya kwanza, zipi ni hatua nyingine zinazotakiwa kufuatwa kurejesha hali katika mstari unaotakiwa?
Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016

Chanzo cha picha, Hisani
Jambo kubwa lililo katika vinywa vya wadau wa sekta ya habari nchini Tanzania linahusu maudhui ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016. Hii ni sheria iliyotungwa katika sura na haiba ya utawala wa Rais Magufuli. Si kila kitu kwenye sheria hiyo kina matatizo lakini vile vyenye matatizo vimeibua mjadala mkubwa.
Ni sheria hiyo ndiyo iliyoweka masharti ya mtu anayetaka kuwa mwandishi wa habari awe na angalau diploma ya uandishi wa habari ili aruhusiwe kufanya kazi hiyo. Kwenye mkutano wake na wahariri, Nape alizungumzia uwezekano wa kuongezwa kwa muda wa kutumika kwa sheria hiyo iliyopangwa kuanza kutumika mwaka huu.
Inafahamika kwamba serikali ina mapendekezo ya makundi matatu tofauti yanayohusika na masuala ya kisheria na habari - Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), CORI na Jukwaa la Wahariri (TEF) yaliyotaka kufanyiwa kwa marekebisho kwa sheria hiyo ya mwaka 2016.
Kuna mambo kadhaa ambayo yanajirudiarudia kupitia ripoti za taasisi hizo tatu. Kwanza ni suala la elimu kwa waandishi, suala la kufanya kesi za kashfa au upotoshaji magazetini kuwa jinai, kuhusu baraza la habari na suala zima la utoaji wa matangazo kwa vyombo vya habari visivyo vya umma.
Sharti la waandishi kuwa na walau diploma ya uandishi lina utata kwa sababu litawanyima sifa mamia ya waandishi wa habari waandamizi ambao baadhi yao wana elimu zaidi ya diploma lakini katika fani nyingine na walisomea uandishi kwa ngazi ya cheti na kupitia mafunzo kazini.
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ni mmoja wa wanahabari ambao wamezungumza kwa uwazi kuhusu umuhimu wa kuwa na Baraza la Habari Tanzania lenye uwakilishi mpana wa waandishi, serikali na sekta binafsi litakalokuwa linashughulika na masuala ya tasnia kama ilivyo katika nchi kama Kenya na Ghana. Hilo ni baraza tofauti na lililo katika sheria hiyo ya mwaka 2016 lenye ushawishi mkubwa wa serikali.
Mkutano wa Nape na wahariri umefanyika katika pengine kipindi kigumu zaidi kwa vyombo vya habari Tanzania katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Ingawa utawala wa Samia unaonekana salama kuliko wa Magufuli, tatizo ni kwamba vyombo vya habari vingi vimekufa na vingine viko hoi; kama alivyonukuliwa akisema aliyekuwa mmiliki na Mhariri Mtendaji wa MwanaHalisi, Saed Kubenea.
Makumi ya wanahabari wenye vipaji, uzoefu na uzeefu mkubwa katika fani hiyo sasa hawana kazi kwa sababu kuna vyombo vichache vyenye uwezo wa kuajiri watu. Na, nikimnukuu Kubenea, hata kama magazeti hayo yamefunguliwa, uwezekano wa kuanza kuonekana mitaani katika siku za karibuni ni mdogo.
Na vitisho vya utawala uliopita kwa waandishi na vyombo vyao umepunguza kwa kiasi kikubwa aina ya kada ya waandishi waliokuwa wakijulikana kwa kuhoji masuala magumu na wale wa habari za uchunguzi. Ingawa kwenye nchi nyingine biashara ya magazeti na televisheni imepunguzwa kwa kiasi kikubwa na mitandao ya kijamii - kwa Tanzania hali ni mbaya zaidi kwa sababu ya kupungua hata kwa ubora wa vyombo hivyo kulinganisha na walau miaka 15 iliyopita.
Kufungulia magazeti pekee ni hatua ya kwanza, lakini kuna hatua nyingine mahususi inabidi zifanywe na wadau kuhakikisha waandishi bora wanarudi kazini, vyuo vya uandishi vinazalisha wahitimu wanaoendana na soko, vyombo vinafanya kazi kwa uhuru na uchumi na sekta binafsi vinakua kwa kasi ili kutoa uwezekano wa mapato mbadala ya matangazo kwa vyombo husika hapa nchini.
Hata hivyo, walau waandishi wanaweza kuanza kuota kuhusu Tanzania mpya yenye vyombo vya habari imara na vinavyotimiza wajibu wake kwa umma.













