Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jengo la bunge Afrika Kusini lawaka tena moto
Moto mkubwa ambao uliwaka katika jengo la bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town ulizuka tena saa chache baada ya kusemekana kudhibitiwa.
Moto ulionekana kwanza ukitokea kwenye paa la jengo hilo siku ya Jumatatu, huku wazima moto wakijaribu kuuzima moto huo.
Moto huo ulizuka kwa mara ya kwanza Jumapili na kuharibu kabisa chumba cha chini cha bunge hilo.
Polisi wamemkamata mshukiwa ambaye atafikishwa mahakamani siku ya Jumanne kwa tuhuma za uchomaji moto, uvunjaji wa nyumba na wizi.
Mamlaka ilionya kuwa moto ungeweza kuongezeka kwasababu ya mazulia na sakafu ya mbao katika jengo hilo, huku msemaji wa bunge Moloto Mathapo aliiambia TimesLive ya Afrika Kusini kuwa baadhi ya wazima moto "walifanya kazi usiku kucha" kujaribu kuzuia moto zaidi.
Lakini wazima moto 12 pekee ndio walikuwa kwenye eneo hilo wakati upepo ulipopamba moto juu ya Bunge la Kitaifa siku ya Jumatatu, kulingana na shirika la habari la AFP. Licha ya uimarishwaji huo moto bado ulionekana kuibuka kutoka kwa jengo hilo usiku ulipoingia.
Taarifa kutoka kwa baraza la jiji iliyotoka saa nne za nchini humo ilisema kwamba ghorofa ya nne na ya tano ya jengo hilo ilikuwa imeharibiwa kabisa. Haikuweza kufahamika mara moja iwapo moto huo ulikuwa umezimwa.
Siku ya Jumapili, Rais Cyril Ramaphosa - ambaye alikiri mfumo wa kunyunyizia maji wa jengo hilo haukufanya kazi ipasavyo - aliwasifu wazima moto kwa kujibu "tukio baya la uharibifu" kwa dakika chache.
Waziri wa serikali Patricia de Lille alikiri kwamba kamera za CCTV hazikuwa zikifuatiliwa wakati moto wa kwanza ulipoanza.
Bi de Lille alisema moto wa Jumapili ulisababisha "kuteketezwa kabisa" kwa bunge la Kitaifa. Maeneo mengine ya jengo la bunge - sehemu ambayo ni ya 1884 - pia yaliharibiwa vibaya.
Kwa sasa hakuna shughuli zinazoendelea katika jengo la bunge sababu wapo likizo, na hakuna aliyejeruhiwa.
Jengo hilo ni hifadhi kwa maelfu ya hazina vikiwemo vitabu vya kihistoria, picha na kazi muhimu za sanaa, ambazo maafisa walisema zimehifadhiwa.
Kumekuwa na wasiwasi fulani kwamba Keiskamma Tapestry ya thamani, ambayo ina urefu wa 120m (394ft) na inaandika historia ya Afrika Kusini, inaweza kuwa imeharibiwa au kuharibiwa.