Charles Njonjo :Mwanasheria mkuu wa kwanza Mkenya afariki

Chanzo cha picha, Ikulu-Kenya
Mwanasheria mkuu wa kwanza wa raia wa Kenya bwana Charles Njonjo amefariki dunia akiwa na miaka 101.
Rais Uhuru Kenyatta ametangaza leo Jumapili, Januari 2, taarifa ya kifo cha mwanasiasa huyo mkongwe Charles Mugane Njonjo.
"Ni kwa masikitiko makubwa kwamba asubuhi ya leo, Jumapili tarehe 2 Januari 2022, nimepokea taarifa za kuhuzunisha na za kufariki kwa Charles Mugane Njonjo," Rais Kenyatta amenukuliwa na magazeti ya Kenya.
Njonjo, alikuwa mjumbe pekee aliyebaki katika Baraza la Mawaziri la uhuru wa Kenya.
Kufariki kwa Mhe. Njonjo ni pigo kubwa sio tu kwa familia yake bali kwa Wakenya wote na kwa hakika, bara zima la Afrika kwa sababu ya jukumu lake kuu katika kuanzishwa kwa taifa la Kenya wakati wa uhuru," Rais alisema.

Chanzo cha picha, Kenya state
Taarifa kutoka kwa familia zinasema, maiti ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo tayari imechomwa katika mji wa Kariokor jijini Nairobi.
Charles Njonjo ni nani?
Charles Mugane Njonjo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzaliwa wa Kenya kati ya 1963 na 1979.
Alistaafu kama mwanasheria mkuu akiwa na umri wa miaka 60.
Baadaye Njonjo alichaguliwa bila kupingwa katika Bunge la Kitaifa Aprili 1980 kama Mbunge wa Jimbo la Kikuyu.
Aliyekuwa rais Hayati Daniel Moi alimteua katika Baraza la Mawaziri mnamo Juni 1980 kuhudumu kama Waziri wa masuala ya ndani na Kikatiba.








