Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Teknolojia inayosaidia wanawake kuwa salama wakiwa mitaani.
Nusu ya wanawake wote duniani wamehisi kukosa usalama kwa kipindi fulani wakitembea peke yao gizani, kwa mujibu wa takwimu za ofisi ya kitaifa.
Wanaweza kumpigia rafiki simu au watume ramani ya walipo kwenye WhatsApp, au wawe na funguo zao mkononi - mikakati yote wanaweza kutumia kuwa salama.
Unyanyasaji wa kimapenzi dhidi ya wanawake umemulikwa kipindi kingi mwaka huu huku wanawake kote nchini Uingereza wakibuni mbinu zao za kuwafanya kuhisi salama nyakati za usiku.
Kwa hivyo teknolojia inaweza kuchangia wanawake kuhisi salama kweye mitaa yetu?
Tangu yatokee mauaji ya Sarah Everard na Sabina Nessa, programu ya WalkSafe imepata umaarufu na kwasasa ndio programu inayotumiwa sana nchini Uingereza kutoa usalama.
Muasisi Emma Kaye alikuja na wazo hilo baada ya kunyanyaswa.
WalkSafe itakuwa na sehemu mpya mwaka ujao, itakayojumuisha ramani ya moja kwa moaja ambapo jamaa na marafiki wanaweza kufuatilia safari yako na kuzungumza nawe kwa njia ya sms moja kwa moja.
Kwa sasa kile kimeipa umaarufu ni ramani inayoruhusu watu kupanga kupitia njia salama zaidi kwa kutazama data za uhalifu.
Bi Kaye alisema, "app yetu inasaida watu kuchukua tahadhari ili kujiepusha na uhalifu badala ya kupambana wakati wakiwa hali mbaya.
Katika chuo cha Bath, watafiti wanajaribu kupata suluhu ya vifaa vya usalama. Wanaunda programu ya saa ya mkononi ya wanawake inayoweza kutuma ujumbe ikiwa itahisi mtumiaji yuko kwenye matatizo kwa kupima mapigo ya moyo na kusonga kwa mwili.
Muasisi mwenza E-J Roodt, anasema wazo lilimjia alipokuwa anakimbia sehemu moja ambayo haikuwa na mwangaza wa kutosha na kuhofia kushambuliwa.
"Nilipoona saa zikitumiwa kutambua mshutuko wa moyo, nilifikiria kuwa teknolojia hiyo inaweza kutumiwa kwa usalama wa wanawake," alisema.
"Suala kuu hapa ni kwamba inaweza kufanyika moja kwa moja na mshambuliji hatakuwa na muda wa kuizuia.
Mashtaka
Muasisi wa programu ya bSafe inayotumiwa kwenye simu za mkononi, Rich Larsen, anaamini teknolojia yake itasaidia watu kushtakiwa,
Ina king'ora cha dharura kinachowashwa kwa sauti. Kisha inaanza kupeperusha picha za video za moja kwa moja na sauti kwenda kwa watu waliochaguliwa na kurekodi kila kitu kinachofanyika.
Bw Larsen anasema kile kinachorekodiwa kinaweza kutumiwa mahakamani kama ushahidi, mfano ubakaji ambao mara nyingi ni vigumu kutoa ushahidi.
Kipaumbele kutoka kwa serikali
Mwezi Julai wizara ya mambo ya ndani ilizindua mifuko ya paunia milioni 5 kusaidia kuboresha usalama wa wanawake katika maeneo ya umma. Baadhi ya mambo yanayoangaziwa ni matumizi ya teknolojia.
Kwa mfano polisi huko Bristol wanatumia vifaa vipya kutambua iwapo vinywaji vimewekwa dawa kwenye vilabu vya usiku.
Polisi huko Cheshire wanaboresha teknolojia ya simu kuhakikisha jibu la mara moja kwa mwanamke anayepiga simu kutafuta msaada.
Mamlaka za West Yorkshire zinakuja na mtandao kwa wanawake wanaotumia usafiri wa umma, kama vile kufuatilia mabasi ili kuzuia wanawake kusimama peke yao vituoni.
Teknolojia pia inaweza kutumiwa kwa njia mbaya kwa watu wanaotaka kukudhuru au kukutisha. Kwa mfano teknolojia ile ile inayokuruhusu kuipata simu yako ilipotea inaweza kutumiwa na mtu aliye na nia ya kukufuatilia
Paladin, ambayo ni idara inayopinga watu kufuatilia, inasema kampuni za teknolojia zinastahili kujitahidi kuwalinda waathiriwa iwapo teknolojia itatumiwa vibaya.
Rachel Horman-Brown kutoka idara hiyo anasema waathiriwa wengine wanafuatiliwa kupitia simu zao.
Suala kuu
Farah Nazeer, anaamini kuwa suala la usalama haliwezi kutatuliwa kwa teknolojia pekee: "huku teknolojia kama vile programu za usalama kwenye simu na saa za mkononi zinaweza kuwafanya wanawake wahisi kuwa salama, hizi ni za muda tu, zinazopuuza chanzo kamili cha unyanyasaji dhidi ya wanawake.
Wanawake uhisi kutokuwa salama katika mitaa, sio kwa sababu ya ukosefu wa taa au programu , lakini kwa sababu ya tamaduni ya ubaguzi wa kijinsia na chuki dhidi ya wanawake hali inayofanya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kuwa mwingi.
"Ni lazima tuangazie katika kukabiliana na ubaguzi huu ili wanawake waweze kutembea kwenda nyumbani wakihisi salama na kulindwa.