Waridi wa BBC: 'Daktari alitabiri nitakufa ndani ya siku saba'

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa

Rosemary Choma Kashaga ni mwanamke ambaye alizaliwa kawaida kama walivyo watoto wengine wa kike , na kulelewa maisha ya kawaida nchini Tanzania. Ila maisha yake yalichukua mkondo tofauti alipofikisha umri wa miaka miwili na nusu, Rosemary anasema kuwa maisha yake yalianza kuwa na misukosuko na mahangahiko mengu tu .

"Wakati ninakua siku za karaha na kero zilipita siku ambazo angalau nilipatwa na hata chembechembe za furaha , mahangaiko makuu yalitokana na maumbile yangu ambayo yalihitaji msaada mkuu wa watu waliokuwa karibu nami'.Anakumbuka Rosemary

Rosemary anasema kwamba alizaliwa mzima bila matatizo yoyote ya kiafya na wakati anakua maisha yaliendelea vizuri kama anavyosimuliwa na wakubwa zake. Mwanamke huyu anasema kuwa alipooza mwili mzima asiweze kufanya lolote alipofikisha umri wa kuanzia miaka miwili na nusu.

"Kwa kipindi cha miaka miwili tangu nilipopooza mwili mzima nilikuwa hospitalini Muhimbili, miezi mitatu ya kwanza nilielezwa kwamba nilikuwa nimezimia kabisa nisiwe na uwezo wa kulia, kucheka au kufanya lolote , kwanzia wakati ninaondoka hospitalini ndipo iligundulika kwamba nilikuwa nimepoteza uwezo wa kutumia sehemu ya kuanzia kiuno changu hadi chini." Rosemary anakumbuka.

Kwa hiyo wakati Rosemary anaanza kupata ufahamu na kujielewa , ilikuwa hawezi kutumia miguu yake mwenyewe bila usaidizi wa aina ya viatu maalumu vijulikanavyo kama Calipers -ni viatu vinavyomuwezesha mtu mwenye ulemavu kuwa na uwezo wa kutembea mwenyewe pamoja akipewa uhimili na mikongojo.

Mwanamke huyu anasema kwamba miaka mingi baadaye bado yuko hai licha ya utabiri huo ambao ulikuwa umewaacha watu wa jamii yake vinywa wazi wasijue cha kufanya. Anasema kwamba kwake ni muujiza kutoka kwa mwenyezi Mungu , Kwani sio kawaida ya mtu kuzimia miezi mitati na kisha kupata fahamu zake .

Pilikapilika za masomo

Wakati alipokuwa ilianza maisha ya shuleni, na anasema kuwa haikuwa rahisi kwani wakati huu wote hadi anapoanza masomo katika shule ya msingi , alikuwa hana habari kwamba alikuwa anaishi na ulemavu wa miguu.

Rosemary anasema kwamba katika mazingira alilelewa alihakikishiwa kwamba alikuwa binti wa kawaida. Pale shuleni ndipo alianza kuona utofauti wa maumbile kutoka kwa wanafunzi wenzake , japo alijiunga na shule iliyokuwa na wingi wa watu wenye ulemavu mbalimbali.

Rosemary anasema kwamba aibu aliyokuwa nayo wakati anaingia shuleni ilikuwa imemzingira asijue la kufanya ila siku baada ya nyingine alijituma na kuendelea kujikubali na hali yake .

Wakati wa likizo ulikuwa pia na changamoto zake aghalab kulingana na jinsi Rosemary anasema kwamba hakuwa na sehemu maalumu ya kuishi na wakati huo wa likizo alihimili yote hadi akamaliza chuo kikuu.

Kuingia Chuo kikuu anasema kwamba alikuwa anaishi kwa kukosa mahitaji maalumu kama binti , anasema kwamba hakuwa anadiriki kusema mahitaji yake kwa watu kutokana na ile aibu aliokuwa nayo tangu mwanzo .

Matukio kama haya yaliendeela kutokea hadi wakati anamaliza shule na kuingia chuo kikuu , lakini hakukata tamaa ya kujiendeleza na kupata masomo licha ya kuwa alihangaika sana .

Maisha ya ndoa

"Hii picha inaukumbusho mkubwa. Hii picha nilipiga kabla sijaolewa. Na kwa imani nilijinenea hayo maneno niliyoyachapisha kwenye hiyo picha na huku moyoni nikiamini kuwa iko siku Mungu atanipatia muujiza wangu. Kupata mume wa kunioa kwa ndoa Takatifu kanisani ilikuwa Moja ya muujiza. Maisha yangu yote ni muujiza. Ndio maana nikiandika na kuishi ile zaburi ya 23 ambayo nikaitafakari " anasema Rosemary.

Baada ya Rosemary kuwa na shauku ya ndio hatimaye maombi yake yalijibiwa.

Wakati Rosemary alikutana na barafu yake ya roho ambaye ni mume wake Andrew , Rosemary alijawa na furaha isiyona kifani , kwanza akitambua kwamba aliyemchumbia alikuwa ni binadamu aliyekuwa hana mapungufu yeyote ya mwili , na kwa upande mwengine yeye alikuwa ameishi na hali ya ulemavu wa miguu, mchumba wake alimkubali kwa moyo wote .

Ndoa yao imedumu zaidi ya miaka 15 na kila siku inazidi kunawiri aghalab kama anavyosema Rosemary . Ila jamii iliyowazunguka baadhi yao walikuwa hawajakubali kwamba Rosemary angekuwa mwanamke ambaye angetunza nyumba yake .

"Wakati ninaanza maisha ya ndoa yangu nilipitia changamoto sio haba , cha kwanza kuna watu ambao walikuwa wanaeneza tetesi kwamba ni vipi mwanamke ambaye hana uwezo wa kutembea atatunza mume , na je ni vipi atakuwa na uwezo wa kushika mimba na kujifungua kama wanawake wengine? maswala mengi mno yaliibuka ila hatukukata tamaa ya kuendela kuishi kama mume na mke , kila siku huwa nina mshukuru mume wangu kwa kunikubali na kuniunga mkono katika juhudi zangu zote "Rosemary anasema

Katika ndoa yao Rosemary na mumewe Andrew wamejaaliwa mtoto wa kiume. Licha ya misukosuko ya maisha Rosemary anasema kwamba amejipa nguvu .

Uandishi wa kitabu chake

Rosemary anasema kwamba kitendo cha kuandika kitabu chake kwa jina 'THIS IS ME' kimezaliwa kwa hali ya machungu na misongo ya mawazo ambayo ameishi nayo tangu utotoni , Rosemary anasema kwamba ilikuwa njia mmoja ya kupunguza maumivu ya misongo ya mawazo na machungu ambayo yamekuweko hasa kupitia changamoto na unyanyapaa mwingi ambao amekumbana nao katika mazingira mbalimbali.

"Kwa mfano nilipokuwa kwenye ajira mbalimbali nilishuhudia sio mara mmoja au mbili nikipitia unyanyapaa katika madhila ya hali ya ulemavu , na nikaanza kuwa na moyo ambao umeumizwa , moyo ambao una machungu. Kingine ambacho kimenishangaza pia, mara nyingi utasikia watu wanaponitazama pengine mara ya kwanza huniuliza vipi? Ulipata ajali ? na mimi nashangaa kwanini watu wanashughulika na muonekano wangu hivyo ?Rosemary anasema.

Hali kama hizi ndizo zilikuwa gurudumu kuu la kitabu chenye kuangazia historia yake ya kuishi na ulemavu na jinsi ambavyo amepambana na maisha hadi sasa .

Rosemary ni mmojawapo ya viongozi wakereketewa nchini Tanzania wanaotumia hali zao, kuteteta maslahi ya watu wanaoishi na ulemavu.