Liver v Man City: Kocha wa City, Pep asema hasimu wake kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amemfanya kuwa 'kocha mzuri'

Pep Klopp

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola anasema hasimu wake kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amemfanya kuwa "kocha mzuri".

Man City wanakutana na Liverpool leo saa 12:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki katika mchezo wa ligi kuu ya England, City wakiwa nyuma ya Liverpool kwa alama moja na alama tatu nyuma ya vinara wa ligi kuu Chelsea, waliowabagaza Southampton 3-1 hapo jana.

Wakati pekee ambao City ilishindwa kutwaa taji la ligi kuu katika miaka minne iliyopita ni msimu wa 2019-2020 ambapo Liverpool ilifanikiwa kulitwaa.

"Tangu nimekuja hapa - labda sio mwaka wa kwanza - Liverpool wamekuwa washindaji wakubwa," alisema Guardiola.

Mhispania huyo, alijiunga na City katika majira ya joto ya mwaka 2016, lakini alikutana na Klopp, ambaye alijiunga na Liverpool October 2015, wakati huo Pep akiwa kocha wa Bayern Munich na Mjerumani Klopp akiinoa Borussia Dortmund.

Pep

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Pep

Guardiola amepoteza michezo minane katika mashindano yote aliyokutana na Klopp, ambayo ni mingi kuliko kocha yoyote aliyewahi kukutana nae.

"Timu zinazonolewa na Jurgen Klopp zimenisaidia kuwa kocha mzuri," alisema Guardiola, ambaye kikosi chake kinakutana na Liverpool baada ya kutoka kuwafunga Chelsea kwenye ligi kuu na kuchapwa na PSG katika mechi ya makundi ya ligi ya mabingwa Ulaya.

"Amenifanya kuwa kwenye anga zingine kabisa, kufikiria, na kuonyesha uwezo wangu, kuwa kocha mzuri. Hiyo ndio sababu mpaka leo nipo naendelea kufundisha.

"Miaka minne iliyopita, wakati wote, tunashindana. Na kitu kizuri kwamba klabu zetu pia zinashindana kileleni.

"Lakini kwenye ligi kuu England hakuna timu moja au mbili, kuna timu nyingi ambazo zinaweza kuwania ubingwa wa ligi kuu."

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Klopp akisalimiana na Pep (kulia)

Liverpool alichapwa 4-1 katika uwanja wake wa nyumbani Anfield kwenye ligi kuu mwezi Februari wakati timu hizo zilipokutana mara ya mwisho na Klopp anafahamu fika kikosi chake kinahitaji kuwa kwenye kiwango chake kizuri ili kuifunga City.

"Mchezo huu ni wa kipekee kila mwaka. Unahitaji kuwa kwenye kiwango chako bora, hapo ndipo , utakuwa na nafasi ya kushinda," alisema Klopp.

n

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Klopp amefanikiwa kumfunga Pep mara 8 tangu wakutane mwaka 2015

Klopp anaongeza kuwa "tunahitaji kucheza mchezo mzuri ili kupata matokeo, lakini usisahau ni Anfield. Tunausubiri kwa hamu mchezo huu.

"City huenda ndio timu bora Ulaya kwa sasa. Wiki iliyopita walicheza dhidi ya Chelsea na kila mtu alikuwa anazungumzi kuhusu ubora wa Chelsea, ambao wanao kweli, lakini City walikuwa bora siku hiyo.

"Tunahitaji kushinda mchezo huu na kufunga mabao mengi lakini tunahitaji kujilinda kwa kiwango cha juu ili ili kuhakikisha mabao tuliyofunga yanaleta tofauti (kutupa matokeo)."