Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mgogoro wa Ethiopia:Kwanini mamia ya malori yamekwama?
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu hali ya chakula nchini Ethiopia katika eneo la Tigray, huku kukiwa na madai ya maroli ya kusambaza chakula kukwama huko na hivyo kushindwa kusafirisha bidhaa muhimu.
Umoja wa mataifa umesema mamia ya malori ya misaada ambayo yamefanya safari mpaka Tigray kutoka maeneo mengine ya Ethiopia katikati ya mwezi Julai na Septemba hayajarudi.
Tumekuwa tukifuatilia kile ambacho kimewakwamisha wakati msaada unahitajika sana.
Malori ya misaada yamepatwa na nini?
Njia kuu ya kupeleka misaada Tigray imekuwa barabara, kupitia eneo la Afar.
Mashirika ya misaada Umoja wa Mataifa yamekadiria kuwa malori takribani 100 ya chakula, vifaa visivyo vya chakula na mafuta , tunahitaji kuingia Tigray kila siku.
Ndani ya miezi miwili mpaka Septemba 16 , malori 466 yameingia Tigray kupitia eneo la Afar, lakini ni malori 38 tu ndio yameweza kurudi , kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
"Kwa sasa , hiki ndicho kikwazo cha msingi kinachozuia misaada kufika Tigray.
"Tunashindwa kujipanga kwa safari zaidi kutokana na uhaba wa malori," msemaji wa Shirika la chakula duniani WFP alisema.
Kwanini malori hayarudi kutoka Tigray?
Tumeuuliza Umoja wa Mataifa , malori yako wapi lakini wameshindwa kutoa maelezo.
Wapiganaji wa Tigray wanapigana na serikali ya Ethiopia na washirika wake wametupa lawama kwa serikali ya Ethiopia.
"Madereva wa malori wanapewa mafuta ambayo yanawatosha kwa ajili ya safari moja tu ya kwenda Tigray. Hawapewi mafuta ya kurudia au mafuta ya akiba katika safari kama hizi,"chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) kilisema hivyo katika taarifa yake.
Taarifa hiyo inasema pia kuwa madereva wengi wa malori wana asili ya Tigraya- na hivyo wanakabiliana na unyanyasaji na vitisho katika vituo vya ukaguzi ambavyo vinasimamiwa na jeshi la Ethiopia na maafisa wa usalama wa ndani kutoka nje ya Tigray.
Hivyo wanasema hawako tayari kupitia mateso waliyopitia wakati wa kurejea.
Kuna marufuku katika kiasi cha fedha cha kubeba, huku huduma ya benki ikiwa imesitishwa ndani ya Tigray, hakuna pesa kwa ajili ya wao wakifika.
Serikali ya Ethiopia imekubali kuwa kushindwa kurudi kwa malori yaliyo Tigray yameathiri usambazaji wa misaada ya chakula.
Lakini tume ya kushughulikia majanga kitaifa, Mitiku Kassa, amekataa madai ya kuishiwa kwa mafuta ndio sababu iliyowafanya madereva kushindwa kurudi.
Kumekuwa na madai kutoka kwa maofisa wa serikali kuwa labda malori yametekwa na TPLF.
Mpaka sasa hakuna ushahidi kuhusu hilo, ingawa wanajeshi wa Tigray waliingia eneo la jirani la Afar mwishoni mwa mwezi Julai, njia ambayo malori mengi yanapita.
Tunafahamu nini kuhusu hali ya mafuta?
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uratibu wa misaada ya kibinadamu (OCHA), imeweka wazi kuwa sababu zilizotajwa madereva kushindwa kurudi ni "ukosefu wa mafuta na kuhofia usalama wao."
Umoja wa Mataifa una baadhi ya sauti zikieleza suala la upatikanaji wa mafuta eneo la Tigray,na awali kulikuwa na malalamiko kuhusu tenki za mafuta kutoruhusiwa kuingia katika eneo hilo.
"Idhini ya kuruhusu malori ya mafuta kwenda Tigray iliripotiwa kukataliwa na mamlaka katika mkoa wa Afar, "UN ilisema hayo mapema mwezi huu.
Mkutano wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada mwishoni mwa mwezi Agosti, ulitaja suala la kuishiwa fedha na mafuta kuwa ndiyo changamoto inayoyafanya maroli yashindwe kurudi , ukizingatia kuwa hawakuruhusiwa kubeba mafuta ya kuingia nayo katika eneo waliloenda.
Mashirika hayo yalisema kutokana na vizuizi hivyo vya fedha imewawia vigumu kwao kupata mafuta.
Ni changamoto kubwa kurudisha malori katika mji mkuu wa Mekelle.
UN umekisia kuwa lita 200,000 za mafuta yanahitajika kila wiki na kusema tangu Julai 12, lita 300,000 tu ndio zimewasili Tigray.
Tenki la mwisho kuwasili Tigray ilikuwa Julai 29 na akiba ya mafuta iliisha tangu Septemba 17, Umoja wa mataifa umesema.
Matenki tisa yamekwama Semera, mji mkuu wa e Afar, wakati yakisubiri idhini ya serikali kuingia Tigray.
Hali ya usalama je ?
Afisa wa misaada ya kibinadamu eneo la Tigray aliliambia shirika la habari AFP hivi karibuni kuwa madereva wengi wa malori wamefanyiwa unyanyasaji katika vituo vya ukaguzi nje ya eneo hilo.
UN ilisema miongoni mwa sababu ambazo madereva walizitaja ni kuhofia usalama wao kwa kuwa walipigwa, walinyanyaswa na kupewa vitisho wakati wakisafiri kutoka Semera kwenda Mekelle."
Taarifa ya UN ya mwezi Agosti inasema matukio ya unyanyasaji , ni jambo ambalo wanalichunguza ambapo lawama zinawaendea polisi wenye silaha wa Afar.
Serikali ya Ethiopia imesema itapunguza vituo vya ukaguzi kutoka saba mpaka viwili ili kuboresha usambazaji wa msaada.
"Ingawa suala hili lilitajwa ili kusaidia misaada kupelekwa bila changamoto lakini bado hakuna mabadiliko," alisema Billene Seyoum, msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu.