Wakati Tanzania, Kenya zikihaha kuandika Katiba, kuna mataifa yasiyokuwa na katiba ya kuandika

Mchakato wa kuandika ama kubadili Katiba nchini Kenya umekumbwa na maswali mengi juma lililopita baada ya Mahakama nchini humo kusema kwamba Rais Uhuru Kenyatta alikiuka katiba katika kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba kupitia mpango wa BBI.
Kwa uamuzi huo wakenya sasa wako njia panda, wenye kuunga mkono kuandikwa kwa katiba mpya ama kubadili kwa kiwango kikubwa katiba inayotumika sasa ya mwaka 2010, wanaona ilikuwa fursa muhimu ya kumaliza ukabila nchini humo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wale wanaokataa mabadiliko hayo kupitia mchakato wa BBI, wanatetea hoja yao ya kwamba BBI inakuja kuongeza mzigo zaidi kwa wananachi kutokana na kuweka vyeo vingi vya juu kwenye mamlaka.
Wakati Kenya ikiiingia katika sintofahamu hiyo, majirani zao Tanzania mchakato wa katiba ulikwama tangu mwaka 2014, miaka minne baada ya kuanzishwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa nchi hiyo Jakaya Kikwete. Lakini mchakato huu umekwama bado na hii ni kutokana na pande mbili kutokukubaliana katika baadhi ya maeneo ya katiba mpya iliyotarajiwa.
Licha ya makelele ya baadhi ya wanaotaka mchakato wa katiba uliokwama uanze upya ama kuendelea, Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa bunge la katiba lililoishia njiani ameweka bayana kwamba kuandika katiba mpya Tanzania si kipaumbele chake kwa sasa licha ya kukiri kwamba Katiba ni muhimu. Anasema kwa sasa anajielekeza zaidi katika kuifungua nchi hiyo na kujenga uchumi.
Sasa michakato yoye hii ya kuandika katiba mpya ama kurekebebisha katiba katika nchi yoyote kwa mifano ya nchi jirani za Kenya na Tanzania hugharimu mamilioni ya dola ukiachilia mbali muda na nguvu.
Katiba ya nchi ni kitu gani?

Chanzo cha picha, HISANI
Kwa tafsiri ya kawaida, Katiba ya nchi ni sheria mama ama sheria kuu inayoainisha misingi mikuu ya kisiasa, madaraka na majukumu ya mihimili iliyopo pamoja na haki za msingi za wananchi.
Kwa mujibu wa Kikundi cha Sheria na Haki za Binadamu cha TIFPA Katiba ya nchi ni muafaka wa kitaifa unaoanisha namna taifa linavyohitaji kujitawala katika mambo yote na kuendesha mambo yake.
Kwa sababu inagusa wananchi, Katiba ya nchi hutungwa na wananchi wenyewe kama watu huru ili kupata muafaka wa taifa lao na namna gani wangependa kujitawala.
Sasa zipo katiba ambazo haziandiki na zipo zinazoandikwa katika nyaraka kuu moja, ambapo karibu asilimia 99 ya mataifa mengi duniani yana katiba ya aina hii, iliyoandikwa katika nyaraka moja ikitumika kama msingi wa utungaji wa sheria na kanuni zingine.
Katiba isiyoandikwa inafananaje?
Katiba isiyoandikwa kwa kitaalamu inaitwa "uncodified constitution' kwa mujibu wa mtandao wa worldatlas. Ni katiba inayoundwa na sheria mbalimbali zinazopatikana katika nyaraka tofauti tofauti, kwa kifupi ni haziko katika nyaraka moja kuu rasmi.
Nyaraka hizi tofauti tofauti zinaweza pia kupatikana kwa wataalam wa sheria au mahakama na nyaraka zote za kisheria zilizotungwa na vyombo vya utungaji wa sheria kama bunge hutumika kama rejea za kuendesha shughuli za serikali, bunge na mahakama.
Ingawa kitaalam wapo wanaopinga 'uncodified constitution' kuitwa katiba isiyoandikwa, wakisema imeandikwa sema imeandikwa katika nyaraka mbalimbali na sio nyaraka moja kuu kama ilivyozoeleka
Faida kubwa ya kutokuwa na katiba ya nchi iliyoandikwa kwenye nyaraka kuu moja ni kwamba ni rahisi kufanya marekebisho ya sheria yoyote kulingana na jambo ama mazingira yaliyopo. Haina mchakato mrefu wala kuhitaji gharama kubwa za kurekebisha sheria kuhusu jambo fulani. Hiyo ni kwa mujibu Lauren Wade kupitia chapisho lake la oktoba mosi, 2019 kwenye mtandao wa legit.ng.
Wade anasema hasara ya kuwa na katiba isiyoandikwa ni kukosekana kwa sheria mama itakayokuwa muongozo wa sheria na kanuni zozote zitakazotungwa za nchi. Lakini pia mgawanya wa madaraka na mamlaka ya mihili inakutana na mgagaziko na mwisho kila mmoja anaweza kuitafsiri sheria ya kawaida kwa anavyoona, kwa hivyo ni rahisi kukutana na sheria zinazogongana kwenye tafrisi na misingi, na kuleta ugumu kwa sababu ya kutokuwepo kwa sheria mama ya kurejea.
Pamoja na hasara hizo, mataifa haya kwa mujibu wa mtandao wa Atlas yana Katiba ya nchi isiyo andikwa;
Israel

Taifa la Israel linaendeshwa kwa katiba isiyoandikwa, na kwa maamuzi yanayoitwa 'Harari' ya Juni 30, 1950, ambayo yaliridhiwa na bunge la nchi hiyo.
Israel pia imeanzisha sheria mbalimbali za msingi zilizojielekeza mahususi kwenye haki za binadamu na usimamizi wa shughuli za serikali.
Sheria hizi zilizoitwa kwa pamoja 'The Basic Laws of Israel' sheria za msingi za Israel zilitumika na kuchukuliwa kama katiba ya nchi hiyo kati ya mwaka 1995 na 2006 wakati wa utawala wa Aharon Barak, rais wa mahakama ya juu ya Israel
Tangu mwaka 1948 kumekuwa na majaribio kadhaa ya kuandika katiba ya nchi hiyo lakini yamekwama kwa sababu mbalimbali ikiwemo tofauti za kisiasa na kiitikadi.
New Zealand
Katiba ya New Zealand ni muunganiko wa sheria na kanuni mbalimbali zinazotafsiri nchi na wananchi wake. Katiba hiyo inaangalia uhusiano ulioko kati ya mtu binafsi na taifa hilo na hasa namna gani serikali inapaswa kuendeshwa.
New Zealand haina nyaraka moja kama katiba, badala yake inategemea nyaraka mbalimbali zilizotungwa nyakati totaufti na zinazobadilika kila wakati. Nyaraka hizi ni pamoja na ile ya sheria ya katiba ya mwaka 1986 (Constitution Act of 1986), Sheria ya bunge na maamuzi ya Mahakama.
Mihimili mitatu ya serikali nchini New Zealand na majukumu yao yanapatikana katika sheria ya katiba ya mwaka 1986.

Saudi Arabia
Mfumo wa sheria za Saudi Arabia umejiegemeza zaidi kwenye 'Sharia' ama sheria zinazofuata misingi ya kiislamu.
'Sharia' zinakubalika na kutumika Saudi Arabia kama katiba lakini kwa mtindo wa nyaraka tofauti na si nyaraka moja iliyokusanya misingi ya uwepo wake. Lakini zipo sheria ndogo ndogo zingine zinazotungwa kwa amri za kifalme zinazozingatia masuala yanayojitokeza ikiwemo sheria za kibiashara na miliki. Wakati mwingine sharia hizi huwa na tofauti za tafsiri kulingana na anayetafsiri na hapo mzozo wa utekelezaji wake unapoanza.
Uingereza

Chanzo cha picha, Getty Images
Uingereza ni taifa lingine lisilo na katiba ya moja iliyoandikwa, yenyewe inatumia sheria na kanuni mbalimbali kutafsiri mambo na namna ya kuendesha nchi.
Sheria hizo mbalimbali na kanuni kwa Uingereza zimejielekeza kuangalia uhusiano wa watu na serikali ama taifa, shughuli za bunge, mahakama na serikali.
Kwa muktadha huo katiba ya Uingereza inapatikana kutokana na sheria za kawaida, maazimio ya kisiasa, na shughuli za kawaida za serikali. Lakini sheria hizi hutungwa na kupitishwa na bunge ambalo lina mamlaka ya kufanya marekebisho.
Canada

Katiba ya Canada na yenyewe ni muunganiko wa sheria zilizoandikwa na zisizo andikwa. Ziko nyingi zinazotungwa na vyombo vya kutunga sheria na zingine ni matamko na maazimio ya kisiasa yenye maslahi kwa umma.
Inabainisha mfumo wa serikali ulivyona haki za msingi za raia na watu wote wanaoishi na kufanya kazi nchini humo.
Katiba hii inajumuisha sheria ya Canada inayoitwa Canada Act 1982, Sheria ya katiba ya mwaka 1867 na marekebisho yake pamoja na sheria zingine na masharti yanayopatikana katika ibara ya 52(2) ya sheria ya katiba ya mwaka, 1982.















