Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: 'Nilimchukia mtoto alipozaliwa bila kujua sababu'
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
- Iliyochapishwa
Suzzy Kahema aliishi maisha ya kawaida yenye matumaini tele akiwa mdogo, lakini katika ujana wake alipitia matukio ambayo karibu yasambaratishe maisha yake.
Mwaka 1996, akiwa na miaka 22 alishika mimba ila kwa kuwa hakuwa kwenye ndoa alihisi kana kwamba alikuwa ametenda dhambi kuu. Aidha, aliona aibu machoni mwa watu.
Wakati huo hakuelewa ni kwanini alihisi hivyo ila ilikuwa ndio mwanzo wa safari ndefu kama mzazi.
Aliathiriwa na tatizo la sonona, lakini anashukuru kwamba mwishowe alipata msaada na kufanikiwa kujinasua.
"Nilihisi kana kwamba nisingeendelea kuishi katika mazingira ya nyumbani kwetu kwani nilijiona kama mwanamke aliyetenda dhambi kuu kwa kushika mimba kwa umri niliokuwa nao," anasema.
"Kwa bahati nzuri, mtu aliyenipa ujauzito alikuwa amekubali kuwajibika na kwa hivyo tulikubaliana kuwa ingelikuwa busara mimi kusafiri hadi nyumbani kwao kuishi kule."
Kwa hiyo ilibidi mwanamke huyu kusafiri hadi mjini Mombasa ili kuishi na wakwe zake. Hata hivyo, kinyume na alivyotarajia, anasema hakukaribishwa kama mke.
Alihisi alikuwa anabaguliwa kwa misingi ya kikabila na asili yake. Kwa hiyo kwa kipindi cha ujauzito wake alipitia changamoto za kukosa uhusiano wa ukaribu na wale mashemeji wake.
Siku ziliendelea kusonga na hatimaye wakati wa kujifungua ukawadia.
Kujaliwa mtoto bila hisia
Alijaliwa mtoto wa kiume lakini badala ya mwanamke huyu kujawa na msisimko na furaha inayoandamana na kujifungua, yeye alikuwa ana huzuni iliyopita kiasi.
"Nakumbuka nikimtazama mtoto wangu wakati amezaliwa na nikawa kama niliyeshutuka nisijue la kufanya. Nilijiuliza moyoni kama mimi ndiye nitakayekuwa na majukumu ya kumpakata na kumyonyesha. Mambo hayo niliyaona kama mzigo mkubwa ambao nilihisi nisingeuweza," anakumbuka Susan.
Baada ya siku kadhaa waliondoka hospitalini na kurejea nyumbani kwa baba yake mtoto.
Anasema alishangaa kuwakuta shemeji zake wakiwa na msisimko na furaha kinyume na hali ilivyokuwa hapo awali.
Walifurahi hata zaidi kufahamu kuwa yule mtoto alikuwa wa kiume.
Ila kwa mwanadada huyu hakuwa na mapenzi kabisa kwa mtoto wake.
Licha ya kuwa angemnyonyesha na pia kuhakikisha alimtosheleza mahitaji yake yote, alikuwa hana hisia za mapenzi naye.
Kwa kiasi kuwa hata baba ya mtoto aliwahi kumuuliza ni kwanini Suzzy hakuwa na msisimko wa mwanamke aliyejifungua mtoto.
"Kwa kawaida ya wanawake waliojifungua utapata kuwa wanatabasamu na kuchezacheza na watoto wao wachanga kama njia ya kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya mama na mtoto umejengeka ila kwangu ilikuwa tofauti, nilikosa ukaribu au hamu ya hata kumbusu yule mtoto," anakumbuka Suzzy.
Miaka ilisonga kwa haraka na mtoto wake alipotimiza miaka miwili alianza kuwa na ugonjwa ambao ulichangia yeye kuwa hospitalini mara kwa mara.
Ugonjwa huo ulianza kuwa chanzo cha mama kumsogelea mtoto wake kihisia na kibinadamu kinyume na hapo awali.
"Nakumbuka kuwa ugonjwa wa mwana wangu kwa jina Babu Magwaro ulianza kunileta karibu na yeye mno. Ni mimi tu niliyekuwa nampa huduma , na kuhakikisha kuwa anapata matibabu pamoja na dawa zilizohitajika,"anasema Suzzy.
Pigo la kupoteza mtoto
Ila alipotimiza miaka saba mwanawe aliaga dunia.
Suzzy alipatwa na mshtuko mkuu na kujawa na huzuni ambayo hakuwa anaielewa. Alishikwa na sonona na wakati huo ukawa wa kiza kikuu.
"Nakumbuka huo ulikuwa wakati wa huzuni kuu kwangu. Nilikuwa najifungia chumbani mwangu mchana kutwa nikiwa nimefunga pazia na kutamani tu kuishi bila kuzungumza na yeyote. Niliwazia tu mwanangu niliyempoteza, nisijue wa kumgeukia," Suzzy anakumbuka.
Marehemu Babu ndiye aliyekuwa mtoto wa kipekee wake Susan, kwani anasema kuwa miaka kadhaa baadaye alifunuliwa na wataalam wa afya ya uzazi kuwa ana changamoto ya kizazi na kwa hivyo ni vigumu kwake kujaliwa mtoto mwingine .
Miaka mwili baada ya mwanawe kuaga dunia, Suzzy naye alishikwa na ugonjwa ambao uliathiri mwili wake.
Alianza kwenda hospitali kila mara akijaribu kutafuta tiba. Mumewe alijitenga naye kipindi hicho kitu ambacho mwanamke huyu hakukitarajia wakati huo.
Suzzy anasema kuwa hali hiyo ilimsukuma zaidi kusononeka, akijilaumu mno kwa matukio ya huzuni yaliyokuwa yanafanyika katika maisha yake.
Ilibidi watengane ila kwa uchungu mwingi. Suzzy anasema alihisi kwamba alikuwa kwenye shimo lenye kina kirefu lenye giza totoro.
Kila mara alipojaribu kujitoa kwenye lile shimo alihisi kulikuwa na jambo baya lililokuwa linafanyika.
"Nakumbuka siku mmoja nilikuwa natazama runinga na mpwa wangu, tukitizama runinga, ila mimi sikumbuki mengi yaliyofanyika usiku huo. Usiku huo sikupata hata lepe la usingizi na wala sikuwa nazungumza na yeyote ila nilikuwa na tabia ya kulialia kila wakati," Susan anasema.
Ni yule mpwa wake aliyezungumza na dadake Suzzy, kuhusu tabia yake ya kulia lia kila wakati na kukaa kivyake kwa muda mrefu bila kuzungumza na yeyote.
Ni hapo ndipo tatizo lake la sonona lilipogunduliwa.
Jamaa zake walimsukuma kutafuta usaidizi wa mwanasaikolojia kwani sonona aliyokuwa nayo ilikuwa inamsukuma na kumpa fikira za kutaka kujidhuru au kujitoa uhai.
Kujinusuru
Matibabu yake yalihusu Suzzy kuzungumza na mwanasaikolojia kuhusiana na mambo yaliyokuwa yanamsumbua akilini mwake hasa kifo cha mwanawe na kuachwa na mumewe.
"Nilikuwa nimeficha sana uchungu wa kumpoteza mwana wangu, na vile vile nilikuwa nimeficha mno siri za misukosuko ya ndoa yangu," anasema.
"Mwanzoni, ndoa yetu ilikuwa shwari ila miaka iliyofuata kulikuwa na vitimbi ambavyo sikuwa na ujasiri wa kuvizungumzia na yeyote. Naamini ni mambo haya ambayo yalikuwa chanzo cha mimi kuwa na sonona," Susana anakumbuka.
Kwa hatua za kila siku za kuanza kuachilia machungu mengi katika maisha yake, pamoja na kuwasamehe watu, alianza uponyaji wa hisia na kwenye akili yake kwanza.
Susan alipata mwanga mpya kutokana na matatizo aliyoyapitia, na akaamua kusomea taaluma ya uanasaikolojia kuanzia cheti cha msingi, stashahada na mwishowe akasomea shahada ya uzamivu.
Ana mpango wa kuendeleza na masomo yake na kuwa profesa, haya yote yakilenga kusaidia watu ambao hupitia msongo wa mawazo, au hata wanaopitia magumu na hawajui wafanyeje.