Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mshirika wa Rais Tshisekedi ateuliwa kuwa spika mpya
Christophe Mboso N'Kodia Pwanga mwenye umri wa miaka 78 ndiye Spika mpya wa Bunge, nchini DRC.
Wadhifa huo ameupata baada ya kupata wingi wa kura kutoka kwa wabunge katika uchaguzi uliofanyika jana Jumatano na hivyo kuchukua nafasi ya spika wa zamani, Jeanine Mabunda aliyeondolewa, mapema mwezi Desemba kwa madai ya ubadhilifu wa fedha za Bunge.
Spika mpya atajiunga na wabunge 391 kuunda serikali mpya ya Rais wa sasa wa DRC, Felix Tshisekedi.
Uchaguzi wa spika huyo mpya unadaiwa kuwa ishara mpya kuwa siasa za DRC zinaweza kubadilika na matakwa ya raia kuafikiwa.
Kwa sasa, Rais Felix Tshisekedi anaweza kuchagua waziri mkuu na serikali ambayo iko huru bila kuingiliwa na mtangulizi wake.
Ni zaidi ya miaka miwili tangu Joseph Kabila aondoke madarakani.
Lakini kutokana na idadi kubwa ya wabunge kutoka chama chake, alibaki kuwa na nguvu kubwa katika taifa hilo na kuweza kusimamia wizara nyingi muhimu.
Tshisekedi amekuwa akiwatimua washirika wa mtangulizi wake tangu alipovunja muungano mwezi Disemba mwaka jana kufuatia kuongezeka kwa tofauti kuhusiana na mageuzi ya usalama, mahakama, tume ya uchaguzi na mashirika mbalimbali ya taifa.
Rais Tshisekedi - kwa sasa amefanikiwa kufanya maamuzi yake bila kuingiliwa na Kabila - hivyo anatarajiwa kuwa ataweza kufanikiwa kufanya mabadiliko na kutimiza ahadi zake ikiwa ni pamoja na kumaliza ghasia katika maeneo ya madini.
Sababu zilizopelekea spika wa awali kuondolewa madarakani
Jeanine Mabunda aliondolewa katika nafasi yake baada ya wabunge kupiga kura ya maoni dhidi yake iliyowasilishwa bungeni na Upinzani.
Miongoni mwa wabunge 484 katika Bunge hilo kura 281 zilisema kwamba kiongozi huyo wa muhimili aondoke katika nafasi yake.
Zaidi ya wabunge mia mbili kati ya wabunge mia tano waalifanya kikao cha kupiga kura ya kumuondoa madarakani Spika wa bunge Jeanine Mabunda kutoka chama cha Joseph kabila.
Mwandishi wa BBC, nchini DRC alisema; Upande wa chama cha Kabila tayari kulikuwa na mzozo katika vyama vilivyokuwa vinamuunga mkono, hivyo hiyo inaweza kuwa sababu ya kuanguka kwao.
Na hatua inayofuata ni waziri mkuu kujiuzulu sasa kwasababu rais atamchagua mtu atakayeunganisha vyama bungeni hivyo nia ya rais ni kuvunja muungano huo.
Lakini kilichoshangaza ni ilikuwaje spika huyo ashindwe kupata kura za kutosha kumtetea wakati wabunge wa chama chake ni wengi zaidi.
Tuhuma zilimwendea rais wa zamani Joseph Kabila kwa kumchagua mtu dhaifu ambaye hajawahi kuwa kiongozi au kusimamia watu wowote.
Hata kutoka kwa wafuasi wake Kabila waliona kuwa nafasi ile ilihitaji mtu ambaye ana uzoefu wa kisiasa, tofauti na spika aliyeondolewa.
Huku wabunge wa upande wa rais aliyeko madarakani Felix Tschisekedi walimtuhumu kwa uongozi mbaya.
Aidha spika mpya aliyechaguliwa sasa Christophe Mboso ,aliwahi kuwa mbunge wakati bunge likiwa chini ya utawala wa Kabila na kutimuliwa kwa kosa la uzembe.