Uchaguzi Uganda 2021: Idadi ya vifo vya ghasia za kampeni yafikia 16 Kampala

Chanzo cha picha, Getty Images
Idadi ya waliopoteza maisha katika siku mbili za maandamano kupinga kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulani maarufu Bobi Wine yafikia 16.
Polisi wanasema zaidi ya watu 60 wamejeruhiwa kwenye vurugu hizo. Zaidi ya watu 300 wamekamatwa.
Bobi Wine bado anashikiliwa na polisi na mpaka sasa bado hajashtakiwa.
Shirika la Msalaba Mwekundu Uganda limesema kuwa wafanyakazi wake waliwasaidia watu 11 waliokuwa na majeraha ya kupigwa risasi.
Wakati huohuo, Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine atakapoachiwa huru.
Wagombea hao wamesema ni vigumu kwao kuendelea na kampeni huku mgombea mwingine akiwa anaendelea kunyanyaswa na polisi kwa madai yasiyo na msingi.

Chanzo cha picha, AFP
Bobi Wine alikamatwa jana Jumatano, Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.
Na punde tu baada ya wafuasi wake kupata taarifa, walianza kuandamana wakidai aachiliwe huru.
Taarifa ya polisi haikusema watu hao wamefariki vipi ingawa video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinaonesha watu waliotapakaa damu huku wengine wakioneshwa kutoweza kufanya lolote yaani wamepigwa risasi na kufariki dunia.
Polisi pia imesitisha matukio kadhaa ya kampeni ya wagombea wa upinzani.
Mawakili wa Bobi Wine wanasema bado mteja wao hajafikishwa mahakamani.
Mgombea mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia alikamatwa na kuachiwa huru.
Mikutano ya kampeni ya Bobi Wine imekuwa ikizuiwa na polisi katika matukio kadhaa.
Marekani imeshutumu ghasia zilizojitokeza katika mji mkuu wa Kampala na miji mingine nchini Uganda kufuatia kukamatwa kwa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.
Ujumbe wa Marekani umesema kuwa "pande zote zipinge vita" na kuchukua hatua za kupunguza hofu iliyotanda nchini humo.
Bobi Wine alikamatwa wakati wa mkutano wa kampeni kwa madai ya kukiuka miongozo ya kukabiliana na virusi vya corona iliyowekwa na Tume ya uchanguzi.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye wafuasi wake walianza maandamano wakidai aachiliwe huru.
Uganda itafanya uchaguzi wa urais mnamo mwezi Januari 2021.













