Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Fahamu mashtaka yanayotarajiwa kuwasilishwa na Donald Trump
Mgombea wa Democrat Joe Biden ametangazwa kama rais mtarajiwa, lakini rais Donald Trump bado anapanga kupinga matokeo ya uchaguzi kisheria katika baadhi ya majimbo muhimu.
Wakili wake Rudy Giuliani ameliambia shirika la Fox News itakuwa makosa ikiwa Trump atakiri kuwa ameshindwa kwasababu: "Kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa katika majimbo angalau matatu au manne au hata pengine 10, kura ziliibwa."
Kampeni ya Trump bado haijatoa "ushahidi thabiti" lakini inasema inapanga kufungua kesi mahakamani katika majimbo mengi muhimu Jumatatu.
Hiki ndicho tunachokifahamu hadi kufikia sasa:
Pennsylvania
Bwana Giuliani anasema kuwa mashtaka zaidi yatafunguliwa juu ya vituo kutoweza kufikika na waangalizi wa uchaguzi katika jimbo hilo.
Hawa ni wale ambao kazi yao ni kufuatilia zoezi la kuhesabu kura lengo likiwa ni kuhakikisha uwazi. Katika majimbo mengi huwa wanaruhusiwa mradi tu wawe wamesajiliwa kabla ya siku ya uchaguzi.
Katika baadhi ya maeneo mwaka huu, kulikuwa na masharti yaliowekwa kabla ya siku ya kupiga kura kwasababu ya virusi vya corona.
Chumba cha ukubwa wa mita 6 kiliwekwa huko Philadelphia kituo cha kuhesabu kura lakini hilo likapingwa mahakamani Alhamisi na kusemekana kuwa kipunguzwe hadi fiti 6 mradi waangalizi wawe wanafuata kanuni za ugonjwa wa Covid-19.
Kampeni ya Trump imewasilisha kesi inayoshtumu maafisa wa uchaguzi kwa kukiuka agizo la mahakama.
Bwana Giuliani alisema: "Hata kama agizo la mahakama lilitolewa kuruhusu wakaguzi wa Republican kuwa kwa karibu umbali wa fiti sita, walisongeza wale wanaohesabu kura umbali wa fiti sita zaidi."
Lakini maafisa wa uchaguzi wanasisitiza kwamba walikuwa vile inavyohitajika.
Novemba 5, Katibu wa jimbo Pennsylvania Kathy Boockvar alisema: "Kila mgombea na chama cha siasa kinaruhusiwa kuwa na mwakilishi aliyeruhusiwa katika chumba hicho kufuatilia hali inavyoendelea.
Baadhi ya mamlaka ikiwemo ya Philly pia wanaonesha mchakato wao moja kwa moja kwenye mtandao ili kila mmoja aweze kufuatilia mchakato wa kuhesabu kura."
Mashtaka yanayopangwa kuwasilishwa huko Pennsylvania baadhi yao yanajikita katika uamuzi wa kuhesabu kura zilizopigwa kwa njia ya posta siku ya uchaguzi lakini zikawasilishwa kwenye kituo cha kuhesabu kura siku tatu baadae. Republicans wanataka kukata rufaa.
Matthew Weil, mkurugenzi wa kituo cha pande mbili cha Utafiti wa Sera ya ubashiri wa uchaguzi, anasema ana wasiwasi juu ya mzozo uliojitokeza kwasababu mahakama ya juu zaidi nchini humo ilikwama katika suala hilo hata kabla ya uchaguzi.
Hiyo ilikuwa ni kabla Jaji Amy Coney Barrett, aliyeteuliwa na rais Trump, alipoidhinishwa.
"Nafikiri kuna hatari baadhi ya kura zilizopigwa kwa njia ya posta lakini zikawa hazijapokelewa hadi Ijumaa zikatupiliwa mbali", amesema.
Lakini Bwana Weil akaongeza: "Ninavyofikiria mimi ni kwamba zitakazokataliwa hazitakuwa kura nyingi," hivyo basi uchaguzi huo "matokeo yake yatakuwa ya karibu mno".
Michigan
Bwana Trump alishinda jimbo hili mwaka 2016 kwa kura kidogo - zaidi tu ya kura 10,700 - na Bwana Biden amekuwa akitabiriwa kuibuka na ushindi katika uchaguzi huu wa mwaka 2020.
Novemba 4, kampeni ya Trump iliwasilisha kesi kusitisha zoezi la kuhesabu kura kwa madai ya ukosefu wa uangalizi wa shughuli hiyo.
Hakimu alitupilia mbali kesi hiyo akisema kumekosekana ushahidi wa kutosha kwamba kwa ujumla, michakato haifuatwi.
Wisconsin
Kampeni ya rais imesema kuwa itaomba kura zihesabiwe tena katika jimbo la Wisconsin "kwasababu ya matukio yasio ya kawaida yalioshuhudiwa" siku ya kupiga kura, ingawa hilo halitahitaji kesi kuwasilishwa mahakamani.
Bado haijafahamika ni lini zoezi la kuhesabu tena kura litafanyika kwasababu kwa hilo kutokea hadi pale maafisa watakapomaliza kupitia tena kura.
Siku ya mwisho ya kutekelezwa kwa hatua hiyo ni Novemba 17.
Profesa wa chuo kikuu cha sheria cha Columbia profesa Richard Briffault anasema zoezi la kuhesabu tena kura lilitokea huko Wisconsin mwaka 2016 na mabadiliko yakawa ni karibu "kura mia kadhaa".
Nevada
Chama cha Republican huko Nevada kiliandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter na kusema: "Kumebainika maelfu ya wapiga kura walioonekana kukiuka sheria za upigaji wa kura baada ya kuondoka Nevada."
Timu ya sheria ya rais ilitoa orodha ya majina ya watu inaodai kuwa walikuwa wameondoka nje ya jimbo hilo lakini walipiga kura.
Lakini inasemekana kwamba kutoa tu orodha pekee hakudhihirishi kuwa sheria ilikiukwa.
Watu waliohama jimbo hilo ndani ya siku 30 kabla ya uchaguzi bado wanaweza kupiga kura. Wanafunzi kutoka Nevada - ambao wanasoma kwingineko pia wanaweza kupiga kura.
Kesi hiyo imelenga wapiga kura katika kaunti ya Clark lakini msajili wa kaunti hiyo amesema: "Hatufahamu kuhusu hatua zozote kinyume na upigaji kura zinazotekelezwa."
Georgia
Kesi iliwasilishwa Georgia kaunti ya Chatham kusitisha zoezi la upigaji kura, kwa madai ya matatizo ya mchakato wa kupiga kura.
Mwenyekiti wa chama cha Republican huko Georgia David Shafer aliandika ujumbe kuwa waangalizi wa chama walimuona mwanamke "akichanganya zaidi ya kura 50 kwenye rundo la kura za wasiokuwepo".
Novemba 5, jaji alitupilia mbali kesi hiyo akisema hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kuchanganywa kwa kura.
Arizona
Timu ya kampeni ya Trump imewasilisha kesi huko Arizona Jumamosi ikidai kuwa baadhi ya kura halali zilikataliwa.
Kesi hiyo inapitiwa lakini Katibu wa Jimbo la Arizona inasema kuwa inachunguza kesi hiyo.
Je inaweza kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu zaidi?
Mapema Jumatano, Bwana Trump alidai kuwa kuna wizi wa kura - bila kutoa ushahidi wowote - na kusema: "Tutakwenda katika mahakama ya juu zaidi".
Ikiwa uchaguzi huu utapingwa, kwanza timu za sheria zitahitajika kupinga matokeo katika mahakama za ngazi ya majimbo.