Virusi vya corona: Jinsi Rwanda na Afrika Kusini zinavyojimudu bila watalii

Iliyochapishwa

Uwepo wa vivutio vingi vya utalii barani Afrika kuanzia kwenye hifadhi za wanyama, fukwe na maeneo ya kihistoria, Afrika ni bara ambalo hutembelewa na wageni wengi, lakini idadi ya wageni hao ilishuka ghafla kwa kiwango kikubwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, anaandika Larry Madowo.

Maria Maile ambaye alikuwa anapokea wageni usiku na mchana nchini Afrika Kusini kwa miaka 22 iliyopita ameshuhudia sasa uhaba mkubwa wa wageni.tangu mwezi Machi.

"Wageni hawaji hivyo kipato nnachokipata ni msaada tu ambao nnapokea kutoka serikalini," alisema akiwa nyumbani kwake mjini Cape Town

Aliongeza kusema kwamba ana miaka 70. Na anahitaji fedha lakini afya yake inakuja kwanza.

Hali ya Bi. Maile' wakati wa mlipuko katika sekta ya utalii Afrika, imewaacha mamilioni wa watu bila ajira.

Hofu kwa wasafiri

Baadhi ya mataifa yameanza kuruhusu tena ndege za kimataifa.

Lakini hali ya njia panda imejitokeza, kufungua utalii kwa haraka kunaweza kuleta mlipuko wa corona tena na kusalia kufunga kwa muda mrefu maisha yataendeleaje bila kazi.

Athari za mlipuko huu,zimeleta majanga makubwa , alisema bwana Naledi Khabo, mkurugenzi wa Jumuiya ya Utalii Afrika.

"Sidhani kama utalii unaweza kurejea kuwa kama awali."

Afrika ilipokea watalii milioni 71.2 mwaka 2019 na sekta iliajiri watu karibu milioni 25, kwa mujibu wa Umoja wa mataifa.

Sekta ya usafirishaji na utalii inachangia asilimia tisa ya kipato cha uchumi wa Afrika duniani.

Tayari mataifa ya Afrika yamepoteza karibu dola bilioni 55bn (£43bn) katika uchumi wake mpaka sasa kwa mujibu wa Umoja wa Afrika.

"Watu hawaoni kuwa watakuwa salama kusafiri na hata wengi walipoteza ajira katika kipindi hiki hivyo ni ngumu kuwa na kipato kwa ajili ya likizo," alisema Eche Emole, ambaye anamiliki kampuni ya sherehe na usafirishaji 'Afropolitan Group'.

Tayari amesitisha safari za kwenda Kenya, Tanzania, Ethiopia na Ghana.

Na sasa tukio la kila mwishoni mwa mwaka mjini Accra, ambalo lililovutia watalii karibu 100,000 mwaka 2019, anaweza kusitisha safari za kwenda huko pia.

"Lengo lililopo sasa ni kubaki mzima, chochote kile ambacho unaweza kukipoteza unaweza kukipata tena," Bwana Emole alisema.

Kuna muda mrefu wa kurejesha hali ya awali

Tanzania na Tunisia, mataifa ambayo ni maarufu kwa hifadhi za wanyama na fukwe ndio mataifa pekee ya Afrika ambayo yamefungua mipaka yake ya kimataifa na kukaribisha watalii.

Morocco na Mauritius,zote zimemaliza marufuku ya kutoka nje lakini bado wageni hawaruhusiwi kuingia.

Kenya, Seychelles na Rwanda zitarudisha ndege za kimataifa kuanzia Agosti 1, kwa masharti ya wageni wote wawe wamepima virusi vya corona na kukutwaa hawana maambukizi.

"Tunatarajia kipato cha utalii kitashuka mwaka 2020 kwa asilimia 50 na 70%," Clare Akamanzi, mkurugenzi wa bodi ya maendeleo nchini Rwanda alitoa maelezo.

Katika taifa hilo dogo la Afrika mashariki, ambako kuna kivutio kikubwa cha sokwe, iliripotiwa mwaka 2019 kuwa wageni walifika milioni 1.63 na taifa hilo kupata dola milioni 498.

Ni mwezi mmoja baada ya shughuli za utalii kurejea tena nchini Rwanda ,mamlaka ya maendeleo ya ya taifa hilo umetangaza kwamba utalii wa ndani umeanza kushika kasi.

Sekta ya utalii ambayo inaingizia Rwanda fedha nyingi ni miongoni mwa sekta zilizoathiriwa zaidi na janga la corona. Mwandishi wa BBC Yve Bucyana anasema Rwanda ililazimika kushusha gharama za utalii wa sokwe kwa kiwango cha asilimia 86 kama njia ya kuwavutia watalii wa ndani.

''Sokwe wanaweza kuzungumza baina yao kwa kutumia sauti au pia alama,mfano wakisema namna hii mmmhhh….....na mimi nikasema namna hii mmmhhh….….ni kama kuwasalimia na wao wanajibu namna hii Ahmhhh………. Ni kama kuwasalimia.''

Utalii unaovutia watu wengi nchini Rwanda ni utalii wa sokwe, Familia moja ya sokwe kwa jina Sa-Binyo yenye sokwe 17 wageni wanaelezwa kuacha mwanya wa mita 10 kati yao na sokwe na hii ni kutokana na masharti ya kudhibiti maambukizi ya covid-19 ingawa zamani hali ilikuwa tofauti na watu walikuwa wanaacha mwanya wa mita 7 kati yao na sokwe".

Afisa mkuu wa mbuga ya sokwe ya Volcano Prosper Uwingeri ameiambia BBC kwamba kuna hali ya matumaini baada ya milango ya sekta ya utalii kufunguliwa tena.

''Tumekwishapokea watalii 227 tangu shughuli za utalii kurejea. Watali hao wote ni wa ndani, wenyeji na raia wa kigeni wanaoishi hapa Rwanda.

Si vibaya ukizingatia athari za covid19 kwa sekta nzima ya utalii, matumaini yapo kwa sababu wengine zaidi ya 450 wameshaomba kibali cha kutalii,tunawasubiri.

Hali si kama zamani kabla ya virusi vya corona ambapo tulikuwa na watalii zaidi ya 150 kwa siku.''

Hii ndio sababu mamlaka ya maendeleo ya taifa iliharakisha kushusha bei ya kutalii kuona sokwe wa volcano kwa kiwango cha asilimia 86 kama njia ya kuwavutia watalii katika kipindi hiki cha Covid19.

''Kabla ya Covid-19 bei ya kutalii sokwe ilikuwa dolla 1500 kwa mtu, sasa ni dolla 500 kwa raia wa kigeni na dolla 200 kwa raia wa Rwanda, tulilazimika kushusha bei ili kuwavutia watalii wa ndani wakati huu ambapo mipaka imefungwa na hasa viwanja vya ndege. Ni vizuri kuwazowesha wananchi kuwa na desturi ya kutalii nchini kwao''

Danny Rugabira ni mmoja wa watalii yeye anasema, ''Nilitaka kutalii sokwe tangu zamani lakini gharama ilikuwa juu sana nikawa najiuliza nitatoa wapi dolla elfu 1 na mia 5.

Lakini kwa kuwa sasa bei ilishushwa ,hii ilinivutia sana nikasema ngoja niende kuona sokwe hao''

Hata hivyo kabla ya kutalii sehemu yoyote ,watalii lazima wawe na cheti cha kuwa hawana virusi vya Corona na kabla ya kuingia katika mbuga ya Volcano lazima wafanyiwe vipimo vya joto na kufuata taratibu zote za kujilinda,

Sekta ya utalii ndiyo ya kwanza kuingizia Rwanda kipato kikubwa kwa mujibu wa mamlaka ya maendeleo ya taifa mwaka 2017 ,utalii uliingiza dolla milioni 438.

Afrika kusini ndio taifa la Afrika ambalo liliathirika zaidi na Covid-19 na linaweza kutokuwa na wageni kwa mwaka wote huu wa 2020.

Inadhaniwa kuwa inaweza kuchukua miaka miwili mpaka mitatu kwa taifa hilo kufikia kiwango cha watalii waliofika Afrika Kusini cha milioni 10.2 kwa mwaka 2019.

Waafrika Kusini wengi walituma taarifa mtandaoni mwanzoni mwa mlipuko wa corona walidanganya kuwa idadi kubwa ya maambukizi mjini Cape Town yalisababishwa na utalii wa wageni.

Lakini Enver Duminy, mkurugenzi wa utalii Cape Town alisema kesi ya kwanza ya Covid-19 ilitoka kwa raia wa Afrika Kusini ambaye alikuwa ametoka ughaibuni.

"Karibu 83% ya biashara zilizokuepo haziwezi kuendelea kwa kipindi cha miezi sita kama hali ikiendelea kuwa hivi huku 56% ya biashara zimeweza kufanya mipango mingine maeneo mengine," bwana Duminy aliiambia BBC.

Namibia, Kenya na Rwanda ni muongoni mwa mataifa ambayo yameanza kuhamasisha utalii wa ndani kwa idadi ya watu wachache.