Virusi vya corona: Je Rais Kenyatta atafungua uchumi ama kuzingatia afya ya Wakenya?

Wakenya wanasubiri kwa hamu hotuba ya rais Uhuru Kenyatta kwa taifa leo ikiwa ni siku ya mwisho ya masharti yaliowekwa na serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya kulikuwa na maoni tofauti kufikia usiku wa Jumapili iwapo ni wakati wa rais Uhuru Kenyatta kuondoa masharti yaliowekwa kuzuia ongezeko la maambukizi ya vurusi vya corona.
Taifa linaelewa kwamba kufikia usiku wa Jumapili, serikali ya kitaifa ilikuwa imejiandaa kuruhusu watu kutembea kutoka kaunti moja hadi nyingine, kwa masharti kwamba serikali za kaunti zitachukua jukumu la hatari hiyo kisiasa, liliandika gazeti hilo.
Kulikuwa na mazungumzo yaliokuwa yakiendelea, huku magavana wakitakiwa kukubali kuhusu jinsi watu watasafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine na kuchukua jukumu la usimamizi na kuwatibu walioambukizwa.
Lakini kulikuwa na makubaliano kwamba kiwango cha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo kilikuwa cha chini licha ya kupewa fedha za jukumu hilo.
Gazeti la The Nation pia linaelewa kwamba makanisa,misikiti na maeneo mingine ya kuabudu yataendelea kufungwa hadi wakati kwamba itifaki na mifumo ya kuwalinda waumini itawekwa.
Kuhusu elimu, ilikuwa imekubalika kwamba wanafunzi wataendelea na masomo mnamo mwezi Septemba huku wengine wakitarajiwa kufungua baada ya mwezi Januari.


Huku wanauchumi wakipigana kuhakikisha kuwa masharti hayo yanaondolewa mjini Nairobi na Moyale lakini sio Mombasa, wataalam wa afya walidaiwa kupigania kuwekwa kwa masharti makali kutokana na idadi kubwa ya maambukizi ilioripotiwa mwezi Juni pekee.
Rais anatarajiwa kufanya uamuzi huo, lakini wataalam wameshauri kwamba maambukizi ni sharti yakabiliwe na yamalizwe kabla ya kuamua kuondoa masharti yoyote.
Ya pili ni kwamba, mfumo wa Afya ni sharti ujiande kukabiliana na ongezeko la maambukizi iwapo utatokea.
Na tatu, kitengo cha usalama na mamlaka ya Afya ni sharti ziwe una uwezo wa kuwatafuta wale waliokaribiana na watu walioambukizwa.
Lengo ni kulinda afya ya raia lakini wakati huohuo kukabiliana na athari mbaya zinazokabili uchumi.
Masharti yanayofikiriwa ni pamoja na kupigwa marufuku kwa mikutano, kufungwa kwa taasisi za elimu, kuzuia usafiri, kudhibiti mipaka, kuendelea kufunga safari za ndege, kutotoka nje nyakati za usiku kuwekwa kwa masharti ya kutotoka nje mbali na uvaaji wa barakoa katika maeneo ya umma.
Pia unaweza kutazama
Mchanganyiko wa masharti haya umepunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa na katika mchakato huo kusaidia kuzuia maambukizi zaidi chini ya kiwango kilichotabiriwa na wanasayansi.
Athari zake dhidi ya uchumi na maisha ya watu zimekuwa kubwa.
Tayari hazina ya fedha duniani IMF imesema kwamba uchumi wa Kenya unatarajiwa kushuka kwa mara ya kwanza tangu 1990 kufikia asilimia 0.3 kutokana na mlipuko huo wa corona.
Hofu ya Uchumi kuathirika
Wakati huo huo, Benki ya Dunia katika makadirio yake ya hivi karibuni imesema kwamba uchumi wa Kenya utapungua 2020 suala ambalo halijawahi kutokea.
Hatahivyo kulingana na gazeti la Nation wataalam wameonya kwamba bila kufikiria kuhusu masuala haya muhimu, kuondoa masharti hayo kwa silimia 20 kutasababisha maambukizi 200,000 na vifo 30,000 kufikia mwezi Disemba.
Ongezko kubwa la maambukizi katika kipindi cha wiki moja iliopita linaonesha kwamba taifa hili liko mbali kufikia kilele chake.
Kulingana na gazeti hilo, cha kutia wasiwasi zaidi ni kwamba idadi ya waliopona imekuwa ikipungua katika kipindi cha wiki zilizopita.
Katika wiki ilioisha Jumamosi, Kenya ilishuhudia mara mbili ya idadi ya maambukizi huku visa 1,557 na watu 232 wakipona, ikiwa ndio idadi ndogo zaidi katika kipindi cha wiki nne.
Idadi ya watu waliothibitishwa kupona kabisa ilishuka kwa asilimia 62 kwa siku hadi asilimia 33 katika kipindi cha wiki hata wakati ambapo idadi ya waliothibitishwa na ugonjwa huo ilipanda hadi 222 kutoka 125 katika kipindi kama hicho.
Hii inamaana kwamba mfumo wa afya wa Kenya ambao tayari una mzigo huenda katika kipindi cha wiki chache zijazo ukashindwa iwapo kitu hakitafanyika kuzuia hilo kutokea.
Ukilinganisha na matifa kama vile Marekani na Itali, ambayo yamezidiwa na maambukizi na vifo katika kipindi cha miezi miwili pekee , Kenya imekuwa na wakati kudhibiti maambukizi bali pia kuandaa mfumo wake wa afya.
Mataifa ya Afrika kama vile Rwanda na Uganda yamefanikiwa kudhibiti maambukizi na sasa yanajiandaa kufungua uchumi wake.
Hatahivyo magavana wanasukuma kufunguliwa kwa uchumi polepole kutokana na wasiwasi wa jinsi raia wa kawaida wanavyotaabika mbali na wafanyabiashara.
Hivyobasi kwa rais Uhuru Kenyatta, tangazo la leo Jumatatu litakuwa chaguo kati ya kulinda maisha ya Wakenya ama biashara zao.














