Virusi vya corona: Taasisi za utafiti Marekani zatahadharishwa juu ya wizi wa data unaodaiwa kuhusisha China

Chanzo cha picha, Getty Images
Wadukuzi wanaohusishwa na China wanalenga mashirika yanayofanya utafiti wa janga la Covid-19, Maafisa wa Marekani wanasema.
Shirika la ujasusi la Marekani FBI limesema kuwa limeshuhudia majaribio ya udukuzi yaliyolenga tafiti zake za chanjo, kinga na vipimo vya virusi vya corona.
Marekani kwa muda mrefu imekua ikiishutumu serikali ya China kuifanyia udukuzi wa kimtandao, kitu ambacho serikali ya China inakana.
Janga la Corona limeleta wasiwasi zaidi baina ya nchi mbili, ambazo kwa pamoja zimekua zikishutumiana kwa kushindwa kudhibiti mlipuko.
Zaidi ya watu milioni 4.3 kote duniani wameathiriwa na Covid-19, huku vifo 83,000 vikithibitishwa na Marekani na vifo 4,600 vikitokea nchini China kwa mujibu wa Cho Kikuu cha Johns Hopkins.
Ofisi ya shirikisho ya Upelelezi na usalama wa kimtandao na Shirika la usalama wa miundombinu (Cisa), kitengo cha idara ya taifa ya usalama, wametoa onyo la pamoja la nadra Jumatano.
Katika kile kilichotangazwa kama tangazo la huduma kwa umma, walisema "huduma ya afya, maduka ya dawa na sekta ya utafiti wanaoshughulikia janga la Covid-19 wanapaswa wote kujua kuwa ni walengwa wa kwanza " wa wadukuzi''
Wezi wa kimtandao wamekua "wakichunguza kujaribu kutambua na kuchukua kwa njia haramu haki miliki na taarifa za afya" juu ya tiba ya virusi vya corona, taarifa yao iliongeza kusema.
China imekanusha kwa mara nyingine tena madai kwamba inaipeleleza Marekani.
Mapema wiki hii, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Zhao Lijian alisema: "Tunaongoza utafiti wa dunia wa tiba na chanjo ya Covid-19 . Ni ukosefu wa maadili kuilenga China kwa uvumi na uongo wakati hakuna ushahidi wowote''.

Chanzo cha picha, Reuters
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu, Donald Trump alielezea kuhusu madai ya Uchina ya udukuzi wa kimtandao.
"Kuna kipya kingine kwa China? Ninailaumu China maana ugonjwa ulipoanza, ungezuiwa ," alisema.
"Sasa unaniambia wanadukua. Kipi kipya? Tunafuatilia kwa karibu sana."
Maafisa wa Marekani waliishutumu China kwa kudukua na wizi wa haki miliki.
Mwaka 2009, Marekani ilidai kuwa wadukuzi wenye uhusiano na China waliweza kupenya katika taarifa za siri kutoka katika ndege yake ya kivita ya -'Lockheed Martin F-35 fighter jet'.
Muda mfupi baadae, China ilitangaza kuwa ilikua inatengeneza ndege sawa na hiyo -Shenyang J-31.
Maafisa wa intelijensia pia miaka iliyopita waliishutumu China kwa kutumia '' wakusanyaji wa data wasiofahamika ", kuiba teknolojia kutoka kwenye makampuni ya Marekani
Bill Evanina, mkurukenzi wa kituo cha kupambana na ujasusi na usalama nchini Marekani, amesema kuwa wizi wa China wa haki miliki una thamani ya dola bilioni 400 kwa mwaka.


Uchambuzi
Uingereza na Marekani tayari wametoa taarifa ya pamoja wakionya kuhusu nchi nyingine zinalenga utafiti wao tarehe 5 Mei.
Wakati huo, hawakutaja rasmi majina lakini duru zilisema China, Urusi na Iran walikuo miongoni mwa wale wanaohusika.
Sasa, katika hatua kubwa, Marekani imeamua kuitaja China katika taarifa yake ya habari.
Hadi sasa bado hawajaungana na Uingereza na taarifa mpya haina maelezo ya kina ya kile kilichofanyika.
Hiyo ina maana hii inaweza kueleweka kama njia ya kuufahamisha umma wa ndani ya nchi na kuongeza shinikizo kwa Uchina kama sehemu ya kuongezeka kwa wasiwasi kati ya Washington na Beijing.













