Virusi vya Corona: Wahudumu wa Afya watumia mifuko ya plastiki kijikinga

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku idadi ya waliokufa ikiendelea kuongezeka, hospitali zote Uingereza zinaendelea kuhakikisha kuna vitanda vya kuhudumia wale ambao ni wagonjwa zaidi.
Akizungumza na BBC, daktari mmoja wa kitengo cha wagonjwa mahututi alieleza kuwa changamoto kubwa ni ukosefu wa vifaa kwa baadhi ya wahudumu wa afya Uingereza.
Licha ya changamoto wanazopitia katika huendakazi wao hawakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari.
Daktari mmoja wa chumba cha wagonjwa mahututi huko Midlands alikuwa tayari kutoa taarifa lakini alitaka majina yake halisi kulindwa.
Daktari Roberts anaelezea jinsi hospitali aliyopo inavyotoa huduma zake wakati wa janga hili la ugonjwa wa Corona.
Vyumba vya wagonjwa mahututi tayari vimejaa wagonjwa wa virusi vya corona.

Upasuaji wote kwa sasa hivi unachukuliwa kuwa sio jambo la dharura pamoja na kliniki zote za wagonjwa wa saratani zimeahirishwa.
Kuna upungufu wa wahudumu, ukosefu wa vitanda katika chumba cha wagonjwa mahututi, ukosefu wa dawa za kukabiliana na bakteria yaani vijiuwa sumu na mashine za kusaidia kupumulia.

Yote hayo ukijumuisha na hali ya sintofahamu ya coronavirus itakapofika kilele chake ambapo inatarajiwa kuwa April 14 na 25, kukimaanisha wahudumu wa hospitali tayari wameanza kulemewa na majukumu.
Hatahivyo, Daktari Roberts anaelezea kwamba ni jambo la kutia hofu kuona kwamba wahudumu hawa wanaoangalia wagonjwa sana kwa saa 13 kila siku wanalazimika kutafuta njia mbadala za kujilinda kimavazi ambazo ni mifuko ya plastiki, aproni za plastiki, na miwani ya jua.
Huku wananchi wakiendelea kuchukuwa tahadhari ya kutosongeleana umbali wa mita mbili, wahudumu wengi wa afya Uingereza wanatakiwa kufuatilia wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na virusi vya Corona umbali wa sentimita 20 bila vifaa vya kujilinda.
Hili likiwa linaongeza hatari ya kutokea kwa vifo, daktari Roberts amesema idara kadhaa ndani ya hospitali yake wanahofia kile kitakachofuata na kuanza kujifichia dawa kwa ajili yao binafsi iwapo watashikwa na virusi vya corona.

"Siyo suala la kutaka kufikia lengo fulani. Wauguzi katika kitengo cha wagonjwa mahututi wanahitaji usaidizi wa dharura. Wanafanya michakato ambayo inahatarisha usambazaji wa virusi.
Lakini wameambiwa kwamba watavalia kofia za kawaida tu kama wanavyokwenda kufanya upasuaji ambazo zinamatundu kwa muundo wake na hivyo haziwezi kuwakinga na maambukizi ya virusi".
"Hilo halikubaliki na ndio sababu tumeamua kuvaa mifuko ya plastiki na aproni vichwani."
Serikali imetambua tatizo hilo lakini imesema kwamba timu ya kusambaza vifaa vya kujikinga kwa wahudumu yenye kusaidiwa na vikosi vya jeshi, itajitahidi kukabiliana na upungufu uliopo.
Aidha, wizara ya afya Uingereza pia imesema zaidi ya barakoa milioni 1 zilisambazwa Aprili Mosi, lakini haikubainika ni vifaa vingapi vya kujikinga usoni na magauni ya mikono mirefu inahitajika.
Dr Roberts anasema bado hospitali hazijapokea vifaa vyovyote kutoka kwa serikali na kile walichonacho kinazua wasiwasi.

"Barakoa tunazotumia kwa sasa zimebandikwa tena vibandiko vinavyoonesha siku ya mwisho ya kutumika. Jana nilipata kimoja chenye vibandiko vitatu.
Kimoja kinaonesha Siku ya mwisho ya kuitumika ni 2009, cha pili kinaonesha 2013 na cha tatu ambacho kilikuwa juu kilionesha mwaka 2021."
Aidha wizara ya afya Uingereza imesema vifaa vyote vilivyowekwa vibandiko tena vimetimiza vigezo vilivyowekwa na ni salama kutumiwa na wahudumu wa afya ingawa Daktari Roberts hajaridhishwa na kauli hiyo.












