Anhony Martial: Mzozo wazuka kati ya kocha mpya Ralf Rangnick na mshambuliaji wa Man United

Martial

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Mshambuliaji wa Ufaransa Anthony Martial amekataa madai ya kocha wa muda wa Manchester United, Ralf Rangnick kwamba alikataa kushirikishwa kwenye kikosi cha kucheza na Aston Villa.

United waliachia uongozi wa mabao mawili kwa moja na kulazimika kutoka sare ya 2-2 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England Uwanja wa Villa Park Jumamosi.

Martial tayari amemwambia Rangnick anataka kuondoka United mwezi huu na Sevilla wanataka kumsajili.

"Sitakataa kamwe kuichezea Man Utd mechi," alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 katika chapisho la mtandao wa kijamii.

"Nimekuwa hapa kwa miaka saba na sikuwahi kudharau na sitawahi kudharau klabu na mashabiki."

Sevilla wameshindwa kufikia mishahara ya Martial au kutoa ada ya mkopo ambayo United wanataka ili kumsajili fowadi huyo.

Martial hajaanza mechi ya Premier League tangu tarehe 2 Oktoba na hajashiriki kabisa tangu ushindi wa 3-2 dhidi ya Arsenal tarehe 2 Desemba.

Hajachaguliwa kwenye vikosi vya hivi majuzi.

Hata hivyo kutokana na majeraha pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika na Covid-19 Rangnick alikuwa na wachezaji sita tu wa nje wa mchezo huo uliopigwa Villa Park.

.

Ralf Rangnick

Chanzo cha picha, Getty Images

KOcha huyo alimuuliza Martial iwapo alitaka kuhusika na kudai jibu lilikuwa hasi.

"Hakutaka kuwa kwenye kikosi," Rangnick alisema.

"Angekuwa kwenye kikosi kama kawaida lakini hakutaka na hiyo ndiyo sababu iliyomfanya asisafiri nasi jana (Ijumaa)."

Martial amefunga mabao 56 katika mechi 173 za Premier League akiwa na United.

Kukataa kwa klabu hiyo kuidhinisha mauzo yake katika msimu wa joto wa 2018 ilikuwa moja ya sababu za kudorora kwa uhusiano na Jose Mourinho ambayo hatimaye ilisababisha Mreno huyo kuondoka katika klabu hiyo.

Mnamo Januari 2019, chini ya Ole Gunnar Solskjaer, fowadi huyo alitia saini mkataba mpya ambao utaendelea hadi 2024.