Yanga yamtimua kocha Luc Eymael kwa kosa la kutoa kauli za kibaguzi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 1

Klabu ya mpira wa miguu nchini Tanzania, Yanga imeamua kumfukuza kazi Kocha wake, Luc Eymael kwa madai ya 'kutoa kauli za kibaguzi na zisizo za kiungwana'.

Kocha huyo ambaye ni raia wa Ubelgiji anadaiwa kutoa matamshi ya kibaguzi hapo jana.

Uongozi wa Yanga umeomba radhi kwa mashabiki wa Yanga viongozi wa shirikisho la mpira nchini Tanzania pamoja na wadau wote wa soka.

Taarifa ya Yanga iliyochapishwa kwenye mtandao twitter, imesema imesikitishwa na kauli zake zisizo za kiungwana na kibaguzi zilizotolewa na kocha huyo na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Katika video hiyo iliyosambaa mitandaoni , Kocha Eymael anasema kuwa timu hiyo haijafuata makubaliano yao ya mkataba.

Kwanza hafurahii kukaa katika nchi hii, hana gari, hawajampangishia nyumba nzuri, mashabiki hawajaelimika wanapiga kelele kama nyani, sihitaji kubaki hapa na timu ambayo haina uelekeo wowote

''Sina gari , Sifurahii kukaa nchi hii, sina Wifi (intaneti) sina DSTV, mke wangu hafurahii uwepo wake hapa, mashabiki wa Yanga hawana elimu na hupiga kelele kama 'Nyani', ni sehemu ya matamshi yake hadharani alipozungumza na wanahabari.

Kocha Eymael amefutwa kazi kuanzia leo 27.07.2020 na kusema kuwa itahakikisha kuwa anaondoka nchini haraka iwezekanavyo.