Claude Gakwaya aibuka mshindi wa mbio za magari za kimataifa za Rally des Mille Collines

Chanzo cha picha, YVES BUCYANA BBC
- Author, Yves Bucyana
- Nafasi, BBC
- Iliyochapishwa
Mnyarwanda Claude Gakwaya ameibuka mshindi wa mashindano ya kimataifa ya mbio za magari maarufu Rally des Mille Collines 'ambayo ni mkondo wa mwisho kwenye kalenda ya mashindano ya mbio za magari barani Afrika.Claude Gakwaya akiendesha gari aina ya Subaru N TEN aliwashinda waendeshaji magari mahiri kutoka Uganda, Burundi na wenzake kutoka Rwanda walioshiriki mashindano hayo ambayo kwa siku 2 yalizunguka barabara za nje ya jiji la KigaliMuitaliano Mitraros Elfterios anaeshirikiana na Paolo Paganin wakiendesha gari aina ya Subaru N TEN walishindwa kumfukuza Gakwaya kwenye nafasi ya kwanza na kuridhika na nafasi ya pili wakiwa nyuma kwa dakika 24 na sekunde 12.

Mashabiki wa mbio za magari wamefurahia kiwango hicho.
Bwana Olivier ni shabiki sugu wa mbio za magari:"Tunashuhudia kiwango kizuri cha mbio za magari, madereva wako tayari na waliandaa vizuri magari yao. Barabara ziko safi ingawa ni kipindi cha mvua.Shida tu ni moja kwamba walishiriki washindani wachache.Tunaomba viongozi wa chama cha mbio za magari wafanye mipango ya kuzidisha idadi ya magari yanayoshiriki''.
Ni magari 6 tu yaliyoweza kupasi jaribio la kwanza la kuyawezesha kushiriki mbio za Mille Collines mwaka huu.Pamoja na kushinda shindano la Mille Collines ,Claude Gakwaya, pia alitawazwa bingwa wa Rwanda wa mwaka huu 2019.








