Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Pakistan yalaani shambulizi baya la makombora la Iran katika ardhi yake

Iran imefanya shambulizi la kombora ambalo linaonekana kulenga vituo vya wanamgambo magharibi mwa Pakistan na kusababisha vifo vya watoto wawili, maafisa wa Islamabad wamesema.

Moja kwa moja

Yusuf Jumah and Dinah Gahamanyi

  1. Mlipuko wa Ibadan: Mlipuko mbaya waathiri vitongoji kadhaa vya jiji la Nigeria

    Mlipuko mkubwa uliotokea katika mji wa Ibadan nchini Nigeria umeua watu wawili na kuwajeruhi wengine 77 usiku kucha.

    Juhudi za uokoaji zinaendelea katika vitongoji saba vya jiji la tatu kwa idadi kubwa ya watu nchini Nigeria.

    Chanzo cha mlipuko huo bado hakijafahamika, lakini mamlaka inashuku kuwa huenda ulichochewa na vilipuzi vya uchimbaji madini vilivyohifadhiwa ndani ya nyumba.

    Picha zinaonyesha majengo yamegeuzwa kuwa vifusi na magari yaliyoharibiwa na mlipuko.

    Video zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, huku shahidi mmoja akielezea duka moja kuharibiwa katika eneo la Bodija, wilaya ya makazi ya jiji hilo.

    "Tunasikia kishindo kikubwa mwendo wa 07:30pm. Dominoes Pizza na Ace Mall huko Bodija ziliharibiwa," alisema.

    Polisi wameahidi uchunguzi wa haraka kuhusu mlipuko huo.

    "Uchunguzi wa awali wa vyombo vya usalama umebaini kuwa wachimbaji haramu waliokuwa wakimiliki moja ya nyumba za Bodija walikuwa wamehifadhi vilipuzi vilivyosababisha mlipuko huo," mkuu wa mkoa huo Seyi Makinde alisema.

  2. Mahakama yaamuru Mackenzie, wengine 30 kufanyiwa uchunguzi wa kiakili kabla ya kesi ya mauaji

    Mahakama kuu mjini Malindi imeupa upande wa mashtaka siku 14 kufanya tathmini ya afya ya akili kwa Paul Mackenzie na washtakiwa wengine 30 kabla ya kusomewa mashtaka kwa madai ya mauaji ya watu wengi huko Kilifi.

    Takriban watoto 238 walikuwa miongoni mwa miili 429 ya watu iliyotolewa katika msitu mkubwa wa Shakahola.

    Walikufa baada ya kudaiwa kulazimishwa kufunga kwa wiki.

    Kuna madai kwamba baadhi ya waathiriwa walinyongwa hadi kufa.

    Baada ya uchunguzi wa miezi tisa, Mkurugenzi wa Mashtaka alisema Mackenzie na wengine 30 walihusika na vifo vya watu hao ,wengi wao wakiwa watoto.

    Mackenzie na washtakiwa wenzake walifikishwa mahakamani Jumatano, lakini DPP aliomba wiki mbili kufanya uchunguzi wa kiakili kabla ya kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

    Timu ya utetezi ikiongozwa na Wycliff Makasembo ilipinga maombi hayo.

  3. Jeshi la Israel linasema limemuua afisa wa kitengo cha kijasusi cha Hamas

    Jeshi la Israel lilisema kuwa mashambulizi y yake yaliyoanza Ukanda wa Gaza katika saa chache zilizopita yalisababisha mauaji ya wapiganaji sita wa Kipalestina, akiwemo kiongozi wa Hamas ambayhe aliyehusika kuwahoji majasusi.

    Taarifa iliyotolewa na jeshi la Israel ilisema kuwa mauaji ya Bilal Nofal, anayehusika na shughuli za ujasusi, "yataathiri pakubwa uwezo wa Hamas."

    Hata hivyo hakuna maoni yoyote kutoka kwa Hamas kuhusiana na madai ya Israel.

    Unaweza pia kusoma:

    • Ni silaha gani zinazotumiwa na Hamas dhidi ya Israel katika vita vya sasa?
    • Je, vita vya dunia vinaweza kutokea iwapo mzozo wa Israel na Gaza utasambaa?
    • Matukio makubwa katika siku kumi za vita vya Israel na Hamas
    • Waandishi wa BBC wanajibu maswali yako kuhusu mzozo wa Israel na Hamas
  4. Ufaransa yasema haitashiriki mashambulizi dhidi ya Wahouthi yanayoongozwa na Marekani ili kuepuka mzozo zaidi

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macro amesema kwamba nchi yake imeamua "kutojiunga" na muungano unaoongozwa na Marekani katika kuanzisha mashambulizi dhidi ya Wahouthi nchini Yemen ili "kuepusha kuongezeka" katika eneo hilo, akisisitiza wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

    Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulizi katika maeneo ya Wahouthi nchini Yemen mwishoni mwa juma lililopita katika juhudi za kukomesha mashambulizi ambayo Wahouthi wanasema "wanaanzisha mshikamano na Wapalestina Gaza’’.

    Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne, Macron alisema: "Ufaransa iliamua kutojiunga na muungano ambao ulisababisha vita dhidi ya Wahouthi kwenye ardhi zao. Kwa nini? Kwa sababu msimamo wetu hasa unatafuta kuepuka kuzidisha aina yoyote," ya mzozo, akisisitiza kuwa suala hilo sio la "kijeshi" bali " ni la kidiplomasia.

    Rais huyo wa Ufaransa pia alionya kwamba kuendelea kwa Israel kwa operesheni zisizo sahihi za kijeshi katika Ukanda wa Gaza kunaleta "hatari kwa usalama wake kwa muda mrefu ‘’.

    Aliongeza kuwa: "Tutaendeleza mipango ya kidiplomasia, maamuzi na majadiliano ya kutaka kusitishwa kwa mapigano."

    Macron alisisitiza kwamba kila juhudi itafanywa na mamlaka za Israel "na Qatar, ambayo ina jukumu muhimu katika suala hili" na washirika wengine wengi kuwaachilia mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

    Unaweza pia kusoma:

    • Ni silaha gani zinazotumiwa na Hamas dhidi ya Israel katika vita vya sasa?
    • Je, vita vya dunia vinaweza kutokea iwapo mzozo wa Israel na Gaza utasambaa?
    • Matukio makubwa katika siku kumi za vita vya Israel na Hamas
    • Waandishi wa BBC wanajibu maswali yako kuhusu mzozo wa Israel na Hamas
  5. Mswada wa wahamiaji wa Uingereza Rwanda: Rishi Sunak akabiliwa na kura kuu baada ya Naibu mwenyekiti wa Conservative kujiuzulu

    Rishi Sunak anakabiliwa na kura muhimu kuhusu mswada wake wa Rwanda, baada ya manaibu wenyeviti wawili wa chama cha Conservative na msaidizi wa waziri kujiuzulu na kuasi suala hilo.

    Siku ya Jumanne Lee Anderson, Brendan Clarke-Smith na Jane Stevenson walijiuzulu ili kupiga kura kwa ajili ya mabadiliko ambayo walisema yangeimarisha sheria.

    Katika pigo kwa mamlaka ya Waziri Mkuu, Wabunge 60 wa chama cha Conservative waliunga mkono marekebisho ya wapinzani wa mswada huo.

    Ofisi ya waziri mkuu (Namber 10) ina uhakika kwamba muswada huo kwa ujumla bado utapita baadaye, lakini inadhaniwa kuwa huenda inajiandaa kutoa msimamo wa maafikiano.

    Wabunge wanatazamiwa kuendelea kujadili mapendekezo ya mabadiliko ya sheria - ambayo yanalenga kuzuia kufufuliwa kwa a mpango wa serikali wa kutuma baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda - katika bunge siku ya Jumatano, huku mswada huo ukitarajiwa kupigiwa kura baadaye iwapo hautarekebishwa.

    Ikiwa takriban wabunge 30 wa wafuasi wa chama cha Conservative watajiunga na vyama vya upinzani katika kupiga kura dhidi ya mswada huo katika kizingiti chake cha mwisho cha Bunge, unaweza kushindwa.

    Angalau wabunge wanne wa Conservative - ikiwa ni pamoja na mawaziri wa zamani Robert Jenrick na Suella Braverman - wamesema hadharani wako tayari kupiga kura dhidi ya mswada huo ikiwa hautaboreshwa.

    Lakini haijulikani ni wangapi zaidi wanaweza kujiunga nao.

    Unaweza pia kusoma:

    • Uhamiaji: Kwanini Uingereza inataka kuwapeleka waomba hifadhi Rwanda?
    • 'Mpango wa Uingereza wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda 'ni kinyume cha Mungu' - Welby
    • Rwanda: Tupo tayari kuwapokea waomba hifadhi kutoka Uingereza
  6. Rekodi za Dunia za Guinness kutathmini upya taji la 'mbwa mzee zaidi duniani'

    Mbwa wa Ureno aitwaye Bobi aligonga vichwa vya habari mwaka jana alipotawazwa kuwa mbwa mzee zaidi kuwahi kutokea duniani na Guinness World Records (GWR) - akiipiku rekodi ya awali iliyodumu kwa karne moja.

    Bobi alifariki mwezi Oktoba akiwa na umri rasmi wa miaka 31 na siku 165.

    Lakini sasa taji lake limetiliwa mashaka, baada ya baadhi ya madaktari wa mifugo kutilia shaka ushahidi wa umri wa Bobi.

    Maafisa wa Rekodi ya dunia ya Guiness (GWR) sasa wamesitisha taji hilo na kuanzisha uchunguzi upya.

    Bobi alikuwa mbwa wa aina ya Rafeiro do Alentejo - aina ambayo ina wastani wa kuishi miaka 12 hadi 14.

    Umri wake mkubwa ulithibitishwa na hifadhidata ya wanyama wanaofugwa nyumbani ya serikali ya Ureno, ambayo inasimamiwa na Muungano wa Kitaifa wa Madaktari wa Mifugo, GWR ilisema mwaka jana.

    Lakini kadri habari za kuvikwa taji lake zilivyoenea haraka - ndivyo pia tuhuma za kulipinga zilivyozidi.

    Uchunguzi wa jarida la Wired uligundua kuwa Bobi alikuwa amesajiliwa kwenye hifadhidata ya wanyama wanaofugwa nyumbani nchini Ureno kuwa alizaliwa mwaka wa 1992, lakini "halikuwa na usajili au data inayoweza kuthibitisha au kukataa taarifa hii".

    Pia kulikuwa na maswali juu ya picha za zamani za mnyama huyo ambazo zilionyesha alama tofauti kwenye manyoya yake, huku wengine wakisema kuwa ni mbwa tofauti kabisa na huyu aliyevikwa taji.

  7. Apple yaipiku Samsung kama mtengenezaji mkuu wa simu duniani

    Apple sasa ina sehemu kubwa ya soko la kimataifa la simu mahiri, na kuiondoa Samsung katika nafasi ya kwanza kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12.

    Kampuni hiyo kubwa ya simu ya Marekani ilichangia zaidi ya moja ya tano ya simu zilizosafirishwa mwaka jana, kulingana na data kutoka Shirika la Kimataifa la Data (IDC).

    Samsung ilichukua 19.4% ya hisa ya soko huku watengenezaji simu wa China Xiaomi, OPPO na Transsion wakifuata nyuma.

    Uuzaji wa simu mahiri umekuwa ukidorora huku mauzo yakiboreka zaidi katika janga hili.

    IDC inaripoti kuwa karibu simu bilioni 1.2 ziliuzwa mwaka jana – ikionyesha kushuka kwa zaidi ya 3% ya mwaka uliopita. Ni kiasi cha chini kabisa kilichouzwa katika muongo mmoja, huku watumiaji wengi wakiimarisha mikoba yao kutokana na changamoto za kiuchumi na viwango vya juu vya riba. Wataalam wanatabiri soko litaimarika mwaka huu.

    Bado, IDC ilisema Apple - ambayo iliuza zaidi ya simu milioni 234 mwaka jana - ndio "mshindi mkubwa zaidi".

    "Sio tu kwamba Apple ndiye mchezaji pekee katika 3 Bora kuonyesha ukuaji chanya kila mwaka, lakini pia inashika nafasi ya 1 kila mwaka kwa mara ya kwanza kabisa," alisema Nabila Popal wa IDC.

    "Haya yote licha ya kukabiliwa na ongezeko la changamoto za udhibiti na ushindani mpya kutoka kwa Huawei nchini China, soko lake kubwa zaidi."

    Hivi majuzi Huawei imepiga hatua katika kutengeneza chips zake, baada ya kupigwa marufuku kununua chips ambazo zilitengenezwa kwa kutumia teknolojia ya Marekani kwa madai kuwa kampuni hiyo inahatarisha usalama wa taifa la Washington.

  8. FBI wachunguza madai ya ngono dhidi ya bosi wa zamani wa Abercrombie

    FBI imeanza uchunguzi baada ya BBC kufichua madai kwamba Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Abercrombie & Fitch (A&F) aliwanyanyasa kingono na kuwadhulumu wanaume katika hafla alizoandaa kote ulimwenguni.

    Mike Jeffries na mshirika wake wa Uingereza pia wanakabiliwa na kesi ya madai kuwa waliendesha shughuli ya biashara ya ngono.

    Maafisa waFBI sasa wanahoji na kutoa wito kwa mashahidi watarajiwakujitokeza ,BBC inaelewa.

    Wakili wa Bw Jeffries alikataa kutoa maoni yake.

    Uchunguzi huo unaongozwa na maajenti wa FBI waliobobea katika madai ya uhalifu wa ngono, na waendesha mashtaka wa shirikisho kutoka Wilaya ya Mashariki ya New York, kulingana na vyanzo kadhaa.

    FBI na Ofisi ya Mwanasheria wa Marekani zote zilikataa kutoa maoni.

    Mnamo Oktoba, kipindi cha BBC kilifichua madai kwamba Mike Jeffries na mwenzi wake Matthew Smith walikuwa wamewanyanyasa vijana kwa ngono katika hafla walizoandaa katika makazi yao ya New York na ulimwenguni kote katika hoteli za kifahari.

    Wanaume wanane waliambia BBC kuwa walihudhuria hafla hizi katika miji kama London, Paris, na Marrakesh kati ya 2009 na 2015.

    Walidai Bw Jeffries na Bw Smith wangeshiriki ngono nao au "kuwaelekeza" kufanya ngono waowenyewe.

    Nyaraka zilizofichuliwa na BBC, ikiwa ni pamoja na tikiti za ndege na ratiba za matukio, zilifichua kuwa kulikuwa na operesheni iliyopangwa sana iliyohusisha mtandao wa waajiri na mtu wa kati, James Jacobson.

  9. Afcon: Namibia yaishtua Tunisia kwa ushindi wa 1-0

    Namibia ilileta mshtuko mkubwa wakati Deon Hotto alifunga kwa kichwa dakika ya 88 kupata ushindi dhidi ya Tunisia katika mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2023.

    The Brave Warriors - iliyoorodheshwa katika nafasi ya 115 duniani na bila ushindi katika mechi yoyote kati ya tisa za awali za Afcon - walikuwa washindi wanaostahili mjini Korhogo.

    Matokeo hayo ya kushangaza yanamaanisha kuwa Namibia wanashika nafasi ya pili kwenye jedwali kwa tofauti ya mabao kufuatia ushindi wa 2-0 wa Mali dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kundi E uliochezwa baadaye Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly.

    Bertrand Traore alifunga mkwaju wa penalti dakika ya 96 na kuifanya Burkina Faso kuishinda kwa taabu Mauritania katika mechi ya ufunguzi ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika Kundi D.

    Mechi za Leo:Jumatano 17 Januari

    Kundi F: Morocco vs Tanzania, Laurent Pokou Stadium, San Pedro (17:00)

    Kundi F: DR Congo vs Zambia, San Pedro (20:00)

    Unaweza pia kusoma

  10. Pakistan yasema watoto waliuawa katika shambulizi la Iran

    Pakistan inasema watoto wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulio la nchi jirani ya Iran siku ya Jumanne.

    Iran ilisema ililenga vituo viwili vinavyohusishwa na kundi la wanamgambo la Jaish al-Adl, kwa mujibu wa shirika la habari lenye uhusiano na jeshi la nchi hiyo.

    Lakini Pakistan ilikataa hili, na kuiita "kitendo haramu" ambacho kinaweza kusababisha "matokeo makubwa".

    Pakistan ni nchi ya tatu, baada ya Iraq na Syria, kukumbwa na shambulizi la Iran ndani ya siku chache zilizopita.

    Shambulio la kombora lililofanywa na Iran dhidi ya Pakistan ni jambo ambalo halijawahi kutokea. Shambulizi la Jumanne lilipiga kijiji kikubwa kusini-magharibi mwa jimbo la Balochistan, ambalo linapakana na nchi hizo mbili.

    Katika taarifa yenye maneno makali, wizara ya mambo ya nje ya Pakistan ililaani vikali "ukiukaji usio na msingi wa anga yake unaofanywa na Iran".

    Ilitaja tukio hilo kuwa "halikubaliki kabisa", na kuongeza kuwa "ilihofisha zaidi kwamba kitendo hiki haramu kimefanyika licha ya kuwepo kwa njia kadhaa za mawasiliano kati ya Pakistan na Iran".

    Pakistan imelalamika kwa "afisa mkuu anayehusika" katika wizara ya mambo ya nje ya Iran katika mji mkuu wake Tehran, na kuongeza kuwa "ukiukwaji huu wa wazi wa uhuru wa Pakistani na kwamba uwajibikaji wa matokeo ya hatua hiyo utakuwa na Iran".

  11. Ethiopia : Takriban watu 225 wafariki kwa njaa huko Tigray - maafisa

    Zaidi ya watu 200 wamekufa kwa njaa tangu Julai katika mji wa Edaga Arbi, katika eneo la Tigray lililokumbwa na ukame na vita, mamlaka za mitaa zilisema.

    Wengine 16 wamefariki katika mji wa karibu wa Adwa.

    Maafisa huko Tigray wanaonya eneo hilo liko kwenye ukingo wa njaa kwa kiwango cha mwisho kuonekana mnamo 1984, na kusababisha hafla ya kimataifa ya kuchangisha pesa ya muziki Live Aid mwaka uliofuata.

    Lakini njaa ni neno nyeti sana nchini Ethiopia.

    Serikali kuu mjini Addis Ababa inakanusha njaa ipo na kusema inajitahidi kutoa misaada.

    Hata hivyo madaktari na wasaidizi wa kibinadamu wanasema misaada haiji haraka vya kutosha, na kuwaacha wakiwa hoi kuokoa maisha.

    Wengi wa wanaokufa ni watoto na vijana.

    Mkazi wa Tigray Abrehet Kiros anakiambia kituo cha televisheni cha eneo hilo kuwa mara kwa mara humuangalia jirani yake mzee, ambaye hana familia iliyosalia ya kumsaidia baada ya mjukuu wake kufariki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe hivi majuzi.

  12. Karim Benzema awasilisha kesi ya kumharibia jina dhidi ya waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa

    Nyota wa soka wa Ufaransa Karim Benzema amewasilisha kesi ya kuharibiwa jina dhidi ya waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa kwa kumtuhumu kuwa na uhusiano na Muslim Brotherhood, vyombo vya habari vya nchini humo vimeripoti.

    Gérald Darmanin alisema mnamo Oktoba kwamba Bw Benzema "ana uhusiano mbaya" na kundi la Kiislamu la Sunni.

    Maoni hayo "yanadhoofisha" heshima na sifa yake, wakili wa Bw Benzema alisema.

    Kundi la Muslim Brotherhood limepigwa marufuku katika nchi kadhaa zikiwemo Misri, Urusi na Saudi Arabia.

    Maoni ya Bw Darmanin mwezi Oktoba yalikuja baada ya mchezaji huyo kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa anaunga mkono watu wa Gaza kama "waathiriwa tena wa mashambulizi ya kidhalimu ya mabomu ambayo hayawaachi wanawake wala watoto".

    Akibainisha kushindwa kwake kuonesha huruma kama hiyo kwa wahanga 1,300 wa Israel waliouawa na Hamas tarehe 7 Oktoba, Bw Darmanin alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Ufaransa "anajulikana sana kwa uhusiano wake na Muslim Brotherhood".

    "Tunapambana na zimwi ambalo ni Muslim Brotherhood, kwa sababu inajenga mazingira ya jihadi," mwanasiasa huyo alikiambia kituo cha televisheni cha kihafidhina cha CNews.

    Karim Benzema, 36, ambaye anacheza nchini Saudi Arabia na ni Muislamu, alikanusha haraka na kutishia hatua za kisheria dhidi ya waziri huyo kwa kashfa.

  13. Vita vya Gaza: Israel na Hamas zaafikia makubaliano kuhusu msaada kwa Gaza, pamoja na mateka

    Israel na Hamas wamefikia makubaliano ya kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu katika Gaza iliyoharibiwa na vita, wapatanishi wa Qatar wanasema.

    Wanasema kuwa chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Qatar na Ufaransa, dawa zitatolewa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

    Kwa upande wake Israeli itaruhusu vifaa zaidi vya msingi kuingia Gaza. Hali ni mbaya katika eneo hilo baada ya zaidi ya miezi mitatu ya mashambulizi ya Israel.

    Wakati huo huo Marekani inasema ina matumaini kuwa mazungumzo zaidi yanaweza kusababisha kuachiliwa kwa mateka zaidi.

    Mjumbe wa Marekani wa Mashariki ya Kati amekuwa Qatar kujadili uwezekano wa makubaliano hayo, msemaji wa usalama wa kitaifa wa White House John Kirby alisema Jumanne.

    Majadiliano yalikuwa "mazito sana na ya kina", aliongeza. "Tunatumai itazaa matunda hivi karibuni."

    Hapo awali, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed Al Ansari alitangaza makubaliano hayo kuhusu msaada.

    Chini ya makubaliano hayo, misaada ya kibinadamu itaondoka katika mji mkuu wa Qatar, Doha, kuelekea Misri siku ya Jumatano. Kisha msaada huo utapelekwa Gaza, ili kukabidhiwa kwa raia, huku dawa zikiwafikia mateka wa Israel.

    Zaidi ya mateka 132 wanakisiwa kuwa bado wanazuiliwa huko Gaza.

    Unaweza pia kusoma:

    • Ni silaha gani zinazotumiwa na Hamas dhidi ya Israel katika vita vya sasa?
    • Je, vita vya dunia vinaweza kutokea iwapo mzozo wa Israel na Gaza utasambaa?
    • Matukio makubwa katika siku kumi za vita vya Israel na Hamas
    • Waandishi wa BBC wanajibu maswali yako kuhusu mzozo wa Israel na Hamas
  14. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja