Bunge la Kenya limeidhinisha mpango tata wa serikali
kupeleka takriban maafisa 1,000 wa polisi nchini Haiti kusaidia kukomesha
ghasia za magenge.
Hii ni licha ya amri ya mahakama inayozuia askari hao
kutumwa nchini haiti, ikisubiri matokeo ya pingamizi la kisheria mahakamani.
Wabunge wa upinzani walilaani kura hiyo, lakini chama tawala
kilitumia wingi wake kuunga mkono serikali kufuatia mjadala mkali.
Haiti ilikuwa imeomba msaada wa kimataifa ili kukabiliana na
ongezeko la uvunjaji sheria.
Ofa ya Kenya ilipata kibali cha Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa mwezi uliopita, lakini mpango huo umepingwa na chama kikuu cha
upinzani.
Takriban magenge 300 yanafanya kazi nchini Haiti na asilimia
80 ya mji mkuu, Port-au-Prince, uko chini ya udhibiti wa magenge hayo.
Makundi haya yamechukua udhibiti mkubwa wa mji huo tangu
mauaji ya rais wa nchi hiyo mnamo 2021 yalipoiweka Haiti katika mzozo wa
kisiasa.
Katika upigaji kura wa Alhamisi katika bunge la Kenya,
wabunge wanaounga mkono hoja hiyo walisema kuwa nchi hiyo ni sehemu ya jumuiya
ya kimataifa na haiwezi kupuuza maombi ya kuomba msaada kutoka kwa mataifa
mengine.
Pia walisema kuwa taifa hilo la Afrika Mashariki lina
historia ya misheni za kulinda amani kama vile Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo na Sierra Leone.
Bunge liliidhinisha mpango huo katika muda mfupi wa kupiga
kura kabla ya Mahakama Kuu kuanza
kusikiliza kesi hiyo.
Chama kidogo cha upinzani, Thirdway Alliance, kimeongoza
changamoto hiyo ya kisheria, kikisema mpango huo haukuwa wa katiba kwa sababu
ni wanajeshi pekee wanaoweza kutumwa nje ya nchi.
Serikali imekataa
hoja hiyo, na inatetea kesi hiyo.