Nini kitatokea baada ya mapigano ya Gaza na watu wake?

Chanzo cha picha, EPA
Joyce kutoka Ghana anauliza: Je, uvamizi wa ardhini huko Gaza unaofanywa na Israel ni unyakuzi wa eneo hilo au ni vita vya kuwaondoa Hamas?
Je, makaazi yatajengwa ili kuwahudumia Wagaza baada ya vita?
Israel inasema inataka tu kuiondoa Hamas, na hakuna sababu ya kufikiri kwamba inataka kukalia tena eneo ililojiondoa karibu miaka 20 iliyopita.
Wengine upande wa kulia wa Israeli wanaweza kutaka, lakini uvamizi kutoka 1967 hadi 2005 ulikuwa wa gharama kubwa na haukupendwa.Israel haitaki kurejea kuwa watawala wa kila siku wa Wapalestina zaidi ya milioni mbili wenye kinyongo.
Bila shaka, maonyo ya Israel kwa Wapalestina kuondoka makwao bila shaka yanazua hofu katika Ukanda wa Gaza kwamba Israel ina ajenda iliyofichwa - na kwamba hii inaweza kuwa marudio ya "Naqba" ("janga") ya 1948, wakati mamia ya maelfu ya Wapalestina walikimbia au kufukuzwa kutoka kwa nyumba zao na vikosi vya Israeli.
Kuhusu suluhu ya baada ya mzozo, hiyo inaonekana kuwa mbali kwa sasa.Afisa mmoja wa zamani wa jeshi la Israel alisema anatumai Israel, mataifa ya Ghuba na jumuiya ya kimataifa zitaungana ili kuijenga upya Gaza.
Na kuna mazungumzo ya kuirejesha mamlakani Mamlaka ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi - ililazimika kuondoka baada ya makabiliano mafupi na ya umwagaji damu na Hamas mwaka 2007.
Kwa kuzingatia uharibifu hadi sasa, kujenga upya Gaza itakuwa kazi kubwa.


















