Hamas yarusha makombora katika mji wa Ashkelon kusini mwa Israel

Wanamgambo hao walianzisha mashambulizi yao ya hivi punde huku idadi ya vifo vya Israel ikifikia 1,000 na mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya Gaza yakiendelea.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi and Yusuf Jumah

  1. Kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Milipuko yaripotiwa katika mji karibu na Ukanda wa Gaza

    Mwandishi wa BBC Alice Cuddy amekuwa akiangazia taarifa za milipuko huko Ashkelon - kufuatia tishio la wanamgambo wa Hamas kushambulia mji huo.

    Hii hapa ramani inayoonyesha eneo la jiji hilo kusini mwa Israeli - karibu na Ukanda wa Gaza, ambao ni eneo la Wapalestina.

    Ramani
  3. Tembo aliyepotea katika mbuga ya Virunga auawa na kuliwa

    Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga inawapa tembo nafasi salama katika eneo la migogoro

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga inawapa tembo nafasi salama katika eneo la migogoro

    Tembo aliyetoroka kutoka mbuga ya wanyama ya Virunga mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameliwa na wakazi wa kijiji jirani.

    "Ni kama bahati ilianguka kutoka mbinguni kwa ajili yetu," kikundi cha wahifadhi kilinukuu watu "walioshangilia" kutoka kijiji cha Katwiguru wakisema.

    Shirika lisilo la kiserikali, ambalo linafanya kazi na mamlaka ya wanyamapori ya nchi hiyo Congolese Institute for the Conservation of Nature(ICCN), lilituma ujumbe kwenye mtandao wa X, zamani ikifahamika kama Twitter kwamba haijabainika ikiwa ni waasi au wanakijiji waliomuua mnyama huyo.

    Uzio wa umeme unachozunguka mbuga hiyo wiki kadhaa zilizopita uliharibiwa na "vijana" kuwaruhusu tembo wawili kupotea siku ya Jumatatu, shirika la habari la AFP linaripoti ICCN.

    Hatima ya tembo wa pili haijulikani. Virunga ni mbuga maarufu ya wanyamapori katikati ya eneo linalokabiliwa na mapigano ambapo vikundi kadhaa vya wanamgambo vinafanya kazi karibu na mpaka wa Rwanda na Uganda.

    Juhudi za uhifadhi zimesababisha vikosi vya waasi kutoka katika mbuga hiyo - ambayo ina urefu wa kilomita za mraba 7,800 (maili za mraba 3,000) - na kuunda eneo salama kwa tembo.

    Kulingana na tovuti ya mbuga hiyo, tembo 580 walihamia kwenye mbuga hiyo mnamo 2020 na kuunda kundi la takriban 700.

  4. Hamas yawaonya wakazi wa Ashkelon kuondoka mjini

    Hamas imetishia kushambulia mji wa Ashkelon nchini Israel kujibu mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram, Hamas ilisema wakazi wa mji huo, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, wana hadi saa 17:00 kwa saa za huko (15:00 BST) kuondoka.

    Onyo hilo lililotolewa na Hamas linafuatia onyo la awali lililotolewa kwa wananchi wa Gaza na jeshi la Israel katika siku chache zilizopita kuhusu maeneo wanayokusudia kushambuliwa.

    Zaidi ya makombora 4,500 tayari yamesharushwa kutoka Gaza hadi Israel tangu Jumamosi, jeshi la Israel linasema.

  5. Habari za hivi punde, Mwanajeshi wa Israel na wanamgambo wauawa kwenye makabiliano kwenye mpaka wa Lebanon

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Afisa mmoja mkuu wa Israel aliuawa katika makabiliano na wanamgambo kwenye mpaka na Lebanon siku ya Jumatatu, jeshi la Israel limethibitisha.

    Jeshi lilisema wanajeshi na ndege ziliwaua "wavamizi wa kigaidi" wawili ambao walikuwa wamevuka katika ardhi ya Israeli.

    Kundi la Palestinian Islamic Jihad lilidai kuwa walikuwa wanachama wake.

    Baadaye, takriban wanamgambo watatu wa vuguvugu la Hezbollah la Lebanon waliuawa wakati wanajeshi waliposhambulia maeneo ya Lebanon kujibu mashambulizi ya makombora .

    Ilikuwa ni siku ya pili mfululizo kwa mashambulizi kuanzishwa kutoka Lebanon, na ilienda sambamba na vita kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina huko Gaza.

    Marekani imeionya Hezbollah, ambacho ni kikosi chenye nguvu zaidi cha kijeshi nchini Lebanon na kilipigana vita na Israel mwaka 2006, kutofungua mkondo wa pili wa vita.

    Ghasia za Jumatatu zilianza wakati watu wenye silaha walivuka mpaka karibu na mji wa Dhayra nchini Lebanon na kuuawa na wanajeshi wa Israel, wakiungwa mkono na helikopta, jeshi la Israel lilisema.

    Wawili kati ya wanamgambo hao waliuawa na mmoja alitoroka na kurudi Lebanon, iliongeza.

  6. Wanajeshi wa kwanza wa Ufaransa wameondoka Niger - ripoti

    Wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa nchini humo wakisaidia kupambana na wapiganaji wa Kiislamu

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa nchini humo wakisaidia kupambana na wapiganaji wa Kiislamu

    Ufaransa imeanza kuondoa wanajeshi wake kutoka Niger kwa amri ya utawala wa kijeshi, shirika la habari la AFP linaripoti.

    "Wanajeshi wa kwanza wameondoka," msemaji wa mkuu wa majeshi wa Ufaransa amenukuliwa akisema.

    Hapo awali, jeshi la Niger lilisema wataanza kuondoka Jumanne wasindikizwa na vikosi vya Niger.

    Mvutano kati ya nchi hizo mbili ulianza mwezi Julai baada ya mapinduzi ambapo rais aliyechaguliwa kidemokrasia na mshirika wa Ufaransa Mohamed Bazoum kuondolewa madarakani.

    Takriban wanajeshi 1,500 wa Ufaransa wamekuwa wakisaidia katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu.

  7. Mtanzania atunukiwa tuzo ya heshima ya malkia Elizabeth II

      • Author, Sam Mahela
      • Nafasi, BBC, London Uingereza
    th

    Chanzo cha picha, Prudencia Paul Kimiti

    Mtanzania Prudencia Paul Kimiti ametunukiwa tuzo ya heshima ya malkia Elizabeth II kutokana na mchango wake mkubwa katika masuala ya jamii katika hafla iliyoongozwa na binti mfalme Anne katika kasri la Windsor nchini Uingereza.

    Prudencia Paul Kimiti akikabidhiwa tuzo ya heshima maarufu kama (MBE) na mfalme Charles III. Hii imekuwa kama ndoto kwa mzaliwa huyu wa mkoa wa rukwa,magharibi mwa Tanzania ambaye sasa anaishi uingereza.

    Tuzo hiyo ilitokana na mchango wa binti huyo wa Kitanzania katika masuala ya jamii hasa watu weusi na watu wanaotoka bara la Asia waishio nchini Uingereza.

    Prudencia kwa sasa anaishi nchini Uingereza, na anafanya kazi kama mkuu wa kitengo cha upelelezi cha mamlaka ya mapato ambapo anahusika na mambo ya forodha na usalama wa mipaka ya Uingereza.Yeye pia ni mwanaharakati wa watu weusi.

    TH

    Chanzo cha picha, Prudencia Paul Kimiti

    th

    Chanzo cha picha, Prudencia Paul Kimiti

    th

    Chanzo cha picha, Prudencia Paul Kimiti

  8. Habari za hivi punde, Uingereza na Ireland kuwa mwenyeji wa Euro 2028

    th

    Chanzo cha picha, PA Media

    Mashindano ya Euro 2028 yatafanyika Uingereza, Ireland Kaskazini, Jamhuri ya Ireland, Scotland na Wales.

    Waziri wa Michezo Stuart Andrew amesema:“Nimefurahia Uingereza na Ireland itakuwa mwenyeji wa Uefa EURO 2028. Tuna uzoefu, viwanja na muhimu zaidi baadhi ya mashabiki wa soka wenye ari kubwa zaidi duniani.

    Katibu wa Utamaduni Lucy Frazer alisema:“Nina furaha kwamba tumepata Uefa EURO 2028. Litakuwa tukio kubwa zaidi la michezo kuwahi kuandaliwa kwa pamoja nchini Uingereza na Ireland.

    Baadhi ya takwimu kuhusu Euro 2028

    • Takriban tikiti milioni tatu zitapatikana - zaidi ya michuano yoyote ya awali ya Uropa
    • Wastani wa uwezo wa kucheza viwanja 58,000 hivyo mashabiki wengi zaidi kuliko hapo awali watahudhuria mechi.
    • Takriban mashabiki milioni 2.5 wanatarajiwa kuhudhuria matukio yanayofaa familia na ya kufurahisha katika bustani za mashabiki.

    Italia na Uturuki kuandaa michuano ya Euro 2032

    Na wenyeji wanaofuata pia wametangazwa kwa ombi la pamoja ya Italia na Uturuki kushinda haki ya hatua ya Euro 2032.

    Kama ilivyotokea kwa zabuni ya Uingereza na Ireland kwa 2028, hii ilikuwa zabuni ya mwisho iliyosalia kwa hivyo haishangazi hata kidogo.

    Viwanja vya Euro 2028

    Haya ndio maeneo 10 ambayo yamepangwa kuandaa mechi wakati wa Euro 2028.

    th

    Chanzo cha picha, BBC Sport

  9. Habari za hivi punde, Hamas: Hatutajadiliana kuhusu mateka hadi mapigano yatakapomalizika

    Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, anasema kundi hilo halitajadiliana na Israel kuhusu mateka ambao wanashikiliwa hadi mapigano yatakapomalizika.

    "Tumeziarifu pande zote zilizowasiliana nasi kuhusu wafungwa wa adui wanaoshikiliwa na upinzani kwamba faili hili halitafunguliwa kabla ya kumalizika kwa vita," anasema.

    "Na itakuwa tu kwa masharti ambayo upinzani utakubali."

    Kama tulivyoripoti awali, Israel inakadiria Hamas inawashikilia kati ya watu 100 na 150 ambao walitekwa nyara kutoka kusini mwa Israeli siku ya Jumamosi.

  10. Mwanamfalme Mohammed Bin Salman akariri uungaji mkono wa Saudia kwa Wapalestina

    Mohammed Bin Salman, pichani mwezi uliopita

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mwanamfalme Mohammed Bin Salman, Mtawala Mkuu wa Saudi Arabia

    Mtawala mkuu wa Saudi Arabia - Mwanamfalme Mohammed Bin Salman - amezungumza na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas kwa simu.

    Bin Salman alisema kuwa nchi yake itaendelea "kusimama pamoja na watu wa Palestina ili kufikia haki zao halali za maisha bora, kufikia matumaini na matarajio yao, na kufikia amani ya haki ya kudumu," Shirika rasmi la Habari la Saudi liliripoti.

    Pia alimwambia Abbas kuwa anafanya kazi na pande zote za kimataifa na kikanda kuzuia "kuendelea" kwa mzozo huo.

    Inafaa kukumbuka kuwa Abbas na Hamas, ambayo inadhibiti Ukanda wa Gaza, ni wapinzani wa kisiasa.

    Abbas anaongoza vuguvugu la Fatah, linalodhibiti Ukingo wa Magharibi. Pia ni mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO).

    Lakini uungaji mkono wa Saudi Arabia kwa Wapalestina ni muhimu, kwani inakuja kinyume na msingi wa mazungumzo ya pande tatu yaliyokuwa yakiendelea kati ya Israel, Saudi Arabia na Marekani ili kurejesha uhusiano kati ya Riyadh na Tel Aviv.

    Wachambuzi wanasema kuwa mzozo huo unaoongezeka umetoa pigo kubwa kwa mazungumzo ya kuhalalisha.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi baada ya shambulio la Hamas, Saudi Arabia iliishikilia Israel kuhusika na ongezeko hilo.

    Ilisema kuwa imetoa "tahadhari za mara kwa mara za hatari ya mlipuko wa hali kutokana na kuendelea kukaliwa kwa mabavu, na kuwanyima watu wa Palestina haki zao halali, na kurudiwa kwa uchochezi wa kimfumo dhidi ya matakatifu yake".

  11. Pigo kwa Mwakinyo baada ya kufungiwa mwaka mmoja kupanda ulingoni

    th

    Bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo amefungiwa mwaka mmoja kushiriki mapambano mbalimbali ya ngumi ndani na nje ya taifa hilo.

    Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi nchini Tanzania (TPBRC) George Lukindo amesema, mbali na adhabu hiyo Mwakinyo anatakiwa kulipa faini ya shilingi Milioni Moja kwa shirikisho hilo.

    Adhabu ya Mwakinyo inaanza leo Oktoba 10, 2023 hadi Oktoba 10, 2024.

    Mwakinyo amepewa adhabu hiyo kwa kushindwa kupanda ulingoni kwenye pambano liloandaliwa Septemba 29 mwaka huu kwa kile bondia huyo alichodai kuwa ni “kutoelewana na promota” wa pambano hilo.

    Mwakinyo sasa ana siku saba za kukata rufaa dhidi ya adhabu hiyo.

    Unaweza pia kusoma

  12. Habari za hivi punde, Idadi ya waliouawa huko Gaza sasa ni 770

    Wizara ya Afya ya Palestina inasema watu 770 sasa wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi yake ya kulipiza kisasi siku ya Jumamosi. Takriban 4,100 wamejeruhiwa.

    Kufuatia hatua ya Israel ya kukata huduma ya usambazaji wa mafuta, umeme na maji katika Ukanda wa Gaza, Shirika la Afya Ulimwenguni limeungana na Unicef ​​kutoa wito wa kufunguliwa kwa ukanda wa kibinadamu katika eneo hilo.

    Naye mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk - huku akilaani mashambulizi ya Hamas - alisema hatua ya Israel kuizingira Gaza inakiuka sheria za kimataifa.

  13. Human Rights Watch yaishutumu Rwanda kwa kuwaua wakosoaji

    Ripoti hiyo inatolewa wakati Mahakama ya Juu ya Uingereza ikitafakari hatima ya mpango tata wa kuwapeleka baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Ripoti hiyo inatolewa wakati Mahakama ya Juu ya Uingereza ikitafakari hatima ya mpango tata wa kuwapeleka baadhi ya waomba hifadhi nchini Rwanda.

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeishutumu Rwanda kwa kutumia mbinu za ukandamizaji kuwalenga wakosoaji wake nje ya nchi, wakiwemo wale ambao wametafuta ulinzi wa kimataifa.

    "Mchanganyiko wa unyanyasaji wa kimwili, ikiwa ni pamoja na mauaji na kupotea kwa watu kutekelezwa, ufuatiliaji, matumizi mabaya ya sheria - za ndani na za kimataifa - unyanyasaji dhidi ya jamaa nchini Rwanda ... ni juhudi za wazi za kuwatenga wakosoaji wanaoweza kuwakosoa," inasema.

    Ripoti hiyo imechapishwa wakati Mahakama ya Juu ya Uingereza ikisikiliza rufaa ya serikali ya Uingereza dhidi ya uamuzi unaozuia mipango yake ya kuwafukuza wanaoomba hifadhi nchini Rwanda.

    Uingereza haipaswi kuchukulia Rwanda kama nchi salama, ilisema. "[Matokeo] yanabainisha kuwa Rwanda si nchi ambayo Uingereza inapaswa kutegemea kushikilia viwango vya kimataifa au utawala wa sheria linapokuja suala la wanaotafuta hifadhi," alisema Yasmine Ahmed, mkurugenzi wa HRW wa Uingereza.

    Rwanda inakanusha madai hayo, huku msemaji wa serikali Yolande Makolo akishutumu HRW kwa "kupotosha ukweli" na "kuendeleza ajenda ya kisiasa".

    Katika ripoti yake, HRW ilisema kuwa iliwahoji takriban watu 150 kote duniani katika kipindi cha tangu ushindi wa Rais Paul Kagame mnamo 2017.

    Ilisema imeandika dhuluma dhidi ya Wanyarwanda wanaoishi Australia, Ubelgiji, Canada, Ufaransa, Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda, Uingereza na Marekani, pamoja na jamaa zao nchini Rwanda.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Wapalestina 17 waliuawa katika mapigano ya Ukingo wa Magharibi

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mbali na Gaza, Wapalestina 17 wamefariki katika mapigano na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu tangu Jumamosi, kulingana na Umoja wa Mataifa.

    Miongoni mwa waliofariki ni watoto wanne, huku watu 295 pia wakijeruhiwa.

    Ukingo wa Magharibi ni tofauti na Gaza na haudhibitiwi na Hamas.

    Wengi wa majeruhi hao walitokana na mapigano na vikosi vya usalama, lakini watu 23 walijeruhiwa kufuatia mashambulizi ya walowezi wa Israel, wakisindikizwa na vikosi, Umoja wa Mataifa unasema.

    th

    Takriban mateka 150 huko Gaza - balozi

    Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Gilad Erdan, anasema "kati ya mateka 100 na 150" wanazuiliwa huko Gaza, baada ya kutekwa nyara kutoka Israel.

    Makadirio ya hapo awali yameweka takwimu katika "dazeni" na karibu 100.

    Leo asubuhi, msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alisema familia za mateka 50 zimearifiwa na jeshi.

    Familia zaidi zitaarifiwa wakati jeshi likithibitisha habari, alisema.

    Jana usiku, Hamas ilisema itawanyonga mateka iwapo Israel itaanzisha mashambulizi ya anga bila ya onyo.

  15. ''Tunaibusu mikono ya waliotekeleza shambulio''- Ayatollah Ali Khamenei

    Kiongozi mkuu wa Iran akizungumza katika hafla iliyofanyika wiki iliyopita

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Kiongozi mkuu wa Iran akizungumza katika hafla iliyofanyika wiki iliyopita

    Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amekanusha kuhusika kwa Iran katika mashambulizi mabaya yaliyoanzishwa na Hamas siku ya Jumamosi.

    Lakini - kwa mujibu wa tafsiri ya Reuters - alisema: "Tunabusu mikono ya wale waliopanga mashambulizi dhidi ya utawala wa Kizayuni."

    Katika hotuba yake ya kwanza iliyoonyeshwa kwenye televisheni tangu mashambulizi hayo ya Jumamosi alisema: "Tetemeko hili la ardhi limeharibu baadhi ya miundo muhimu [katika Israeli] ambayo haitarekebishwa kwa urahisi," Ayatollah Ali Khamenei alisema.

    "Vitendo vya utawala wa Kizayuni wenyewe ndio wa kulaumiwa kwa maafa haya."

    Iran inasadikiwa kufadhili Hamas, kutoa mafunzo na silaha kwa wanamgambo.

    Maelezo zaidi:

    • Je, Iran inaunga mkono Hamas kufanya operesheni ndani ya Israel?
    • Kwa nini Israel ilichukua muda mrefu kukabiliana na mashambulizi ya Hamas?
    • Maswali 8 kuuelewa mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina
  16. Usiku mgumu zaidi katika miaka yangu 20 ya kuripoti kuhusu Gaza

      • Author, Rushdi Abu Alouf
      • Nafasi, BBC News, Gaza City
    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Tukio katika Jiji la Gaza Jumanne asubuhi

    Usiku kulikuwa na mashambulizi makubwa ya anga. Nilikuwa katika eneo la Jiji la Gaza ambako majengo mengi yaliharibiwa.

    Kulikuwa na sauti za kutisha za milipuko angani, na moshi mwingi na miali ya moto usiku kucha.

    Ninaishi katika jengo la makazi na karibu familia 20. Watoto walikuwa wakipiga kelele usiku kucha na hakuna mtu aliyekuwa na usingizi wa muda.

    Katika miaka 20 ya kuripoti habari za eneo hili, usiku wa jana ulikuwa mgumu zaidi ambao nimeushuhudia.

    Leo asubuhi nilifanikiwa kutoka. Nilikuwa nikiendesha kwenye vifusi kila mahali.

    Majengo yanaporomoka mtaani na vitongoji vizima vimebomolewa.

    Majengo ya serikali na vyuo vikuu, miundombinu, misikiti na vituo vya polisi vimeharibiwa.

    Baadhi ya majengo ninayoyatambua. Lakini mengine huwezi kuyatambua kutokana na ukubwa wa uharibifu katika kitongoji hiki.

  17. Habari za hivi punde, Mzozo wa Israel na Hamas: Ving'ora vya mashambulizi ya roketi yasikika kusini mwa Israel

    Ving'ora vya mashambulizi ya anga vinasikika tena katika miji kadhaa kusini mwa Israel, jeshi la Israel linasema.

    Maelfu ya maroketi yamerushwa kwa Israel kutoka Gaza tangu wimbi hili la mashambulizi kuanza siku ya Jumamosi.

  18. Jeshi la Israel lina vikosi 35 kwenye mpaka wa Gaza

    g

    Chanzo cha picha, EPA

    Msemaji wa jeshi la Israel (IDF) Richard Hecht anasema jeshi la nchi yake "linajenga miundombinu kwa ajili ya operesheni za siku zijazo" na kwamba batalioni 35 zimetumwa kwenye mpaka na Gaza.

    Kikosi kwa ujumla kinaundwa na mamia ya askari.

    Israel inatarajiwa kuanzisha operesheni kubwa ya ardhini huko Gaza, kujibu mashambulizi ya siku ya Jumamosi.

    Jana usiku, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema mashambulizi ya anga huko Gaza ni "mwanzo tu".

    Unaweza pia kusoma:

    • Mohammed Deif: Mfahamu kiongozi wa Hamas anayewanyima usingizi Israel
    • Masuala muhimu unayopaswa kujua kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina
    • Je, ni nini kilichotokea 1967 wakati israel ilipokabiliana kijeshi na mataifa matatu ya kiarabu katika vita vya siku sita?
    • Fahamu chanzo cha uhasama kati ya Israel na Palestina
    • Tunachojua kufikia sasa kuhusu raia wa Israel waliotekwa na Hamas
  19. Mzozo wa Israel na Hamas kwa picha: Majengo yalivyoporomoshwa na mashambulizi ya anga ya Israel

    Tumepokea picha za watu wa Gaza wakitathimini uharibifu uliotokana na mashambulizi ya anga ya Israel usiku kucha.

    Jeshi la anga la Israel linasema lilipiga shabaha za wanamgambo 200 kwa usiku mmoja.

    Takribani watu 700 huko Gaza wamekufa katika mashambulizi ya anga tangu Jumamosi, mamlaka za mitaa zilisema.

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    j

    Chanzo cha picha, Reuters

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

  20. Mzozo wa Israel na Hamas:Yanayojiri hivi punde

    Tumekuwa tukikupatia taarifa kuhusu mzozo wa Israel na Hamas tangu asubuhi na kwa muhtasari haya ndiyo yaliyojiri hivi punde;

    • Hatimaye Israel imefunga mpaka na Gaza, ambao wanamgambo wa Hamas waliuvunja siku ya Jumamosi kuzindua mawimbi yao ya mashambulizi mabaya.
    • Jeshi la anga la Israel linasema lilipiga shabaha 200 usiku kucha katika Ukanda wa Gaza
    • Siku ya Jumatatu jioni, Hamas ilionya kuwa itawaua mateka iliowachukua kutoka Israel ikiwa mashambulizi ya anga yataendelea bila ya onyo
    • Jeshi la Israel liliwashauri watu wa Gaza kuondoka kupitia kivuko kinachodhibitiwa na Misri - lakini baadaye wakasema kivuko hicho kimefungwa.
    • Unicef ​​imetoa wito wa kuwepo kwa ukanda wa kibinadamu ndani na nje ya Gaza, kwani Israel imepunguza usambazaji wa mafuta, umeme na maji.
    • Israel inasema imepata miili ya wanamgambo 1,500 tangu mashambulizi hayo kuanza Jumamosi asubuhi