Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kenya: Mwizi wa watoto wachanga afungwa miaka 25 jela baada ya ufichuzi wa BBC

Mfanyakazi wa hospitali ya Kenya ambaye alifichuliwa na BBC akiuza mtoto kwenye masoko ya siri amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.

Moja kwa moja

  1. Paris: Hofu ya uvamizi wa kunguni yaongezeka kabla ya Olimpiki ya 2024

    Mlipuko wa kunguni umekumba Paris na miji mingine ya Ufaransa, na kusababisha hofu kubwa ya wadudu hao na kuzua maswali kuhusu afya na usalama wakati wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka ujao.

    Hivyo ndivyo kwa mapana jinsi jambo hilo limeelezewa katika vyombo vya habari vya Kifaransa - na sasa vya kimataifa.

    Kwa sehemu fulani kuna ukweli ndani yake. Lakini upande mwingine sivyo.

    Hali ilivyo ni kwamba idadi ya kunguni imeongezeka katika wiki zilizopita - na kwamba mwelekeo huo wa kuongezeka unarudi nyuma miaka kadhaa.

    "Kila majira ya mwisho wa kiangazi tunaona ongezeko kubwa la kunguni," anasema Jean-Michel Berenger, mtaalamu wa wadudu katika hospitali kuu ya Marseille na mtaalam mkuu wa Ufaransa wa les punaises .

    "Hiyo ni kwa sababu watu wamekuwa wakizunguka Julai na Agosti, na wanarudi nao kwenye mizigo yao.

    "Na kila mwaka, ongezeko la idadi ya wanaojitokeza wakati wa msimu ni kubwa kuliko la mwaka uliotangulia."

    Ripoti kwamba hivi karibuni kunguni wamekuwa wakionekana kwenye kumbi za sinema hazijathibitishwa, lakini zinachukuliwa kwa uzito. Kadhalika madai kwamba watu wameumwa kwenye treni.

    Na sasa baraza la Jiji la Paris na serikali ya Rais Emmanuel Macron wanataka hatua zichukuliwe. Ni kipimo cha jinsi wanavyochukulia suala hilo kwa uzito - na jinsi wanavyohitaji kulinda taswira ya Paris mfano wa uvumbuzi kwenye mitandao ya kijamii.

    Kwa sababu hiyo pia ni sehemu ya simulizi fulani.

    Simulizi za kutisha zinasambaa mtandaoni kwa haraka sana hivi kwamba wanageuza kile ambacho zamani kilikuwa utani wa kwenye magazeti kimegeuka na kuwa dharura ya kitaifa.

    Wamiliki wa sinema - ambao tayari wana wasiwasi kuhusu kupungua kwa idadi ya watakao hudhuria – wanaingia hofuu kweli wakati video zinaposambaa zikionyesha wadudu zisizojulikana kwenye kiti cha treni. Watu kwenye metro wameanza kuchunguza bidhaa zao huku wengine wakiwa wanapendelea kusimama.

    Bw Berenger anasema, "Ni jambo zuri kwa namna fulani kwa sababu linasaidia kuwafahamisha watu kuhusu tatizo hilo, na kadiri unavyochukua hatua dhidi ya kunguni ndivyo inavyokuwa bora zaidi.

    "Lakini kwa ukubwa wake, tatizo linatiliwa chumvi."

    pia unaweza kusoma:

    • Kunguni sasa ni sugu kwa dawa
  2. Wabunge wa Canada wachagua Spika wa kwanza mweusi wa Bunge la Wawakilishi

    Canada imemchagua Mbunge wa Liberal Greg Fergus kuwa Spika mpya wa Bunge la Wawakilishi baada ya yule wa awali kujiuzulu huku kukiwa na mzozo wa Wanazi bungeni.

    Bw Fergus - mtu mweusi wa kwanza kushikilia wadhifa huo - alichaguliwa na wabunge 338 baada ya kura ya siri siku ya Jumanne.

    Alisema ni "heshima kubwa" kuchaguliwa kwa jukumu hilo.

    Spika huyo wa zamani alijiuzulu baada ya kumwalika mwanamume wa Ukraine aliyepigania kitengo cha Nazi bungeni.

    Anthony Rota alisema hakujua uhusiano wa mkongwe huyo wa Nazi.

    Wagombea saba walikuwa kwenye kinyang'anyiro cha kuchukua nafasi yake Jumanne.

    Katika matamshi yake ya kwanza, Bw Fergus aliwataka wenzake kuheshimiana katika Bunge, mahali ambapo alisema ni kwa "mijadala yenye shauku".

    "Tutawaonyesha siasa ni taaluma yenye ungwana," alisema.

    Waziri Mkuu Justin Trudeau alisema kuchaguliwa kwake "kunapaswa kuwa na msukumo kwa Wakanada wote, haswa vizazi vichanga vinavyotaka kujihusisha na siasa".

    Uteuzi wake ulipingwa na baadhi ya wanachama wa Conservative.

  3. Takriban watu 21 wafariki baada ya basi kuanguka kutoka kwenye daraja

    Takriban watu 21 wakiwemo watoto wawili wamefariki baada ya basi kuanguka kwenye barabara ya juu karibu na mji wa Venice nchini Italia na kuwaka moto, maafisa wamesema.

    Basi hilo lilivunja kizuizi na kutumbukia karibu na njia za reli katika wilaya ya Mestre, ambayo imeunganishwa na Venice kwa daraja.

    Miongoni mwa waliofariki ni raia watano wa Ukraine, Mjerumani mmoja na dereva wa Italia, gavana wa jiji Michele Di Bari alisema.

    Meya wa Venice Luigi Brugnaro alisema "janga kubwa" limetokea.

    "Hakuna maneno yanayoweza kueleza tukio hilo," alisema kwenye mtandao wa kijamii.

    Basi hilo linafikiriwa kukodishwa kuchukua watalii kati ya Venice na eneo la kambi katika wilaya ya karibu ya Marghera.

    Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 19:45 (17:45 GMT) huku basi hilo likiripotiwa kuwarudisha watalii kwenye kambi hiyo.

    Baadhi ya ripoti zinasema basi hilo lilikuwa linatumia gesi ya methane na kuangukia kwenye njia za umeme na kuwaka moto.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Matteo Piantedosi alionya kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.

    Chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na waokoaji wanaendelea na kazi nayo katika eneo la tukio.

    Takriban watu 18 wamejeruhiwa, watano kati yao vibaya sana.

    Kituo cha mapokezi chenye watalaam wa kisaikolojia na magonjwa ya akili kimeanzishwa katika hospitali iliyo karibu ili kutoa msaada kwa familia za waathiriwa.

    Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisema anafuatilia matukio na akatoa rambirambi zake.

    "Mawazo yetu ni kwa waathiriwa na familia zao na marafiki," alisema.

    Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema anasimama na viongozi wa Italia "wakati huu wa maumivu makali".

    Mnamo mwaka wa 2013, watu 38 waliuawa baada ya dereva kushindwa kudhibiti njia karibu na mji wa Monteforte Irpino kusini mwa Italia, na kugonga magari mengine kadhaa kabla ya kuanguka kwenye korongo.

    Pia unaweza kusoma:

    • Ajali ya basi yawaua 38 nchini Italy
  4. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya leo ikiwa ni tarehe 04/10/2023